UKOO WA MONGI.

– Mongi ni ukoo mashuhuri wa wachagga wenye ngome yao katika kijiji cha Samanga, Marangu. Huu ni ukoo mkongwe sana unaohesabu vizazi vinavyokwenda mpaka miaka ya zamani sana kutokea kwa mchagga wa zamani zaidi wa ukoo huu anayekumbukwa. Mongi ni ukoo uliotoa wachagga wengi mashuhuri wanaofanya vizuri katika sekta mbalimbali. Wachagga wa ukoo wa Mongi pia ndio walioleta uislamu kidogo sana unaopatikana Marangu na kujenga msikiti katika kijiji cha Samanga kwenye eneo linalojulikana kwa jina maarufu la headquarter.

– Kutoka kwenye historia Mongi ni ukoo uliokuwa na nguvu sana na uliokuwa na himaya yake peke yake inayojitegemea ndani ya Marangu ambayo ilidumu kwa muda mrefu bila kuingiliwa. Kwani hata baada ya wamangi wa Marangu kutawala maeneo yote ya Marangu mpaka kufikia karne ya 18, eneo la Samanga ambalo ndio ngome ya ukoo wa Mongi liliendelea kuwa ni eneo huru linalojitawala mpaka mwishoni mwa karne ya 19.

– Eneo la mwisho kuangushwa na kuingizwa kwenye himaya ya umangi Marangu lilikuwa ni Mshiri iliyokuwa ngome ya ukoo wa Mtui lakini pamoja na Marangu yote kutiishwa eneo la Samanga chini ya ukoo wa Mongi Liliendelea kuwa imara. Wakati wa utawala wa Mangi Horombo wa kutokea Keni, Rombo aliyetawala Rombo na Vunjo yote mwishoni mwa karne ya 18 mpaka mwanzoni mwa karne ya 19 eneo la Samanga ndipo lilipoteza mamlaka yake kwa kukaliwa na Mangi Horombo na hata Mangi aliyetawalishwa na Horombo kutawala eneo la Samanga wakati huo alitokea Lyamrakana kwenye familia ya umangi Marangu ambaye ni ndugu yake na Mangi Itosi aliyeitwa Nderima.

– Nderima alipewa upendeleo na Mangi Horombo kutawala Samanga kwa sababu alionyesha ujasiri mkubwa tofauti na kaka yake Itosi. Hata hivyo baada ya ule utawala wa Mangi Horombo kuanguka baada ya kifo chake Samanga ilirudi mikononi mwa ukoo wa Mongi ambao waliendelea kuwa huru na kujitawala. Takwimu za kihistoria zinaonyesha kwamba mpaka kufikia mwaka 1887 wakati mjerumani von Hohnel alipotembelea Kilimanjaro aliitaja Samanga kama moja ya himaya huru za Uchagga, Kilimanjaro zilizokuwa zikijitawala na kumtaja Mangi wa Samanga wa wakati huo akiitwa Mangi Muono au Mnanu.

– Babu wa zamani zaidi wa ukoo wa Mongi anayekumbukwa na historia za wachagga wenyewe mpaka kufikia karne ya 19 inasemekana aliitwa Manzi na inasemekana alianzia maisha katika kijiji cha Mshiri katika eneo lililokuwa linajulikana kama Komkonja kabla ya baadaye kushuka chini zaidi. Mtawala huyu na Mzee wa zamani zaidi wa ukoo wa Mongi kwa kuhesabu vizazi inaonekana aliishi Marangu mwishoni mwa miaka ya 1500 au mwanzoni mwa miaka ya 1600 yaani mwishoni mwa karne ya 16 au mwanzoni mwa karne ya 17. Mzee wa ukoo wa Mongi mpaka kufikia katika ya karne ya 20 aliitwa Samanya.

– Kutoka kwenye historia Samanga inaonekana ilikuwa himaya inayojitegemea mpaka miaka ya 1880’s kwa mujibu wa mwandishi wa kujerumani von Hohnel. Lakini kwa mujibu wa mwandishi mwingine wa kijeruman Widenmann kufikia mwaka 1899 himaya ya Samanga haikuwepo tena kwenye orodha ya himaya za Uchagga, Kilimanjaro ikimaanisha kwamba ilikuwa tayari imekuwa sehemu ya himaya ya umangi Marangu. Hiyo ndio kusema kwamba himaya ya Samanga iliingizwa Marangu wakati wa utawala wa Mangi Ndegoruo Marealle.

– Kwa mujibu wa masimulizi ya wachagga zamani (oral traditions) ni kwamba Marangu na Mamba walikubaliana kushirikiana pamoja kuvamia Samanga na kuiangusha kisha kugawana eneo hilo kwa himaya zote mbili iwasaidie pia waweze kufungua lango la upande wa kusini ambapo lilikuwa ni muhimu katika kijiimarisha kibiashara kwa misafara inayotokea upande wa kusini. Kilichopelekea kuamua kushirikiana kwa himaya ya Marangu na Mamba dhidi ya Samanga ni kwa sababu Samanga ilikuwa na nguvu sana hivyo ilikuwa vigumu kuiangusha ngome ya ukoo wa Mongi ambao walikuwa wana nguvu sana na wanajilinda sana.

– Hata hivyo inasemekana kwamba baada ya Marangu na Mamba kuiangusha Samanga na kukamilisha mpango huo Marangu waliwadhulumu Mamba na kuichukua Samanga yote. Hilo lilipelekea Mamba kuendelea kubaki kuwa na eneo dogo la ardhi na hata kushindwa kufungukia upande wa kusini ili kujiimarisha kibiashara kwa misafara kutokea nje ya Kilimanjaro. Mpaka leo Mamba imeendelea kubaki bila kuwa na nuka yao wenyewe kwani imezibwa na Marangu na Mwika kwa upande wa Kusini.

– Ukoo wa Mongi japo haukuendelea kusambaa sana lakini umeendelea kuhakikisha kwamba Samanga inabaki kuwa ni ngome yao hata mpaka leo hii. Hata hivyo ukoo wa Mongi waliendelea kusambaa katika vijiji vingine vichache vya Uchagga, Kilimanjaro kutokea katika ngome yao Samanga ambayo ni moja kati ya vijiji bora kabisa Uchaggani, Kilimanjaro vyenye mazingira mazuri na yanayovutia sana ikiwa ni eneo lenye rutuba nyingi sana pia.

– Hivyo ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Rauya, Marangu.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kiasi katika kijiji cha Sembeti, Marangu.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi sana sana katika kijiji cha Samanga, Marangu.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Ashira, Marangu.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi kiasi katika kijiji cha Kimbogho, Mamba.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa uchache sana katika kijiji cha Mkolowony, Mamba.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Kiria, Mamba.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Kimangaro, Mamba.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Lekura, Mamba.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi kiasi katika kijiji cha Kondeni, Mwika.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa wingi kiasi katika kijiji cha Kiruweni, Mwika.

– Ukoo wa Mongi unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Mawanjeni, Mwika.

Ukoo wa Mongi umekuwa ni ukoo wa watu jasiri walioweza kulinda himaya yao kwa kipindi kirefu sana katika historia lakini hata hivyo bado taarifa za kuangushwa kwake hazifahamiki kwa usahihi sambamba na taarifa nyingine muhimu kuhusiana na ukoo huu mkongwe sana Uchaggani, Kilimanjaro. Tunahitaji msaada wa taarifa zaidi kuhusiana na ukoo huu ili kuweza kuchangia kwenye tafiti zinazoendelea na hata kuweza kuhifadhi maudhui haya kwa manufaa ya kizazi cha sasa na uzao wa baadaye. Maudhui haya yatasaidia pia kujenga hamasa na mashikamano katika kuendelea kufanya makubwa kwa ngazi ya mmoja mmoja na wachagga kwa ujumla.

Karibu kwa mchango zaidi wa Mawazo kuhusu ukoo wa Mongi.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mongi?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Mongi?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mongi?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Mongi una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu?

5. Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

6. Wewe ni Mongi wa kutokea kijiji gani?

7. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Mongi kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

8. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mongi?

9. Wanawake wa ukoo wa Mongi huitwaje, na kwa nini?

10. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Mongi?

11. Ni watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Mongi?

12. Kuna mnyama yeyote ambaye labda ni mwiko kuliwa na wachagga wa ukoo wa Mongi?

13. Kuna ukoo ambao hawaruhusiwi kuoana na Wako-Mongi kwa sababu zilizowahi kuwepo miaka ya zamani au nyingine zozote?

Karibu kwa Mchango zaidi au maswali.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

www.wachagga.com

Urithi Wetu Wachagga (Facebook).

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *