*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*
Uchambuzi by Mary Assenga.
MAFUNDISHO YA SHIGHA NA MREGHO.
-Msichana anapoendelea kukua alifundishwa mambo mbalimbali ya kuhusu nafasi yake kama mwanamke hasa katika ndoa, mafundisho haya yaliitwa “shigha” na “mregho” ambapo waliweza kujifunza mambo mengi ambayo yaliwasaidia katika maisha yao. Msichana ambaye hakufundishwa “shigha” na “mregho” tunaweza kumfananisha na mtu ambaye hajasoma na yule ambaye alifundishwa mambo haya alipata heshima kubwa sana katika jamii. Wanaume walifundishwa mafundisho ya “ngasi” na waliweza kujifunza “mregho” wakiamua.
-Kuna mchoro uliokuwa kama fimbo uliokuwa na maeneo mawili moja ya juu kama mfuniko uliitwa “MSHINGO” na eneo la chini ambalo ndio sehemu kubwa liliitwa “MREGHO”, ambayo ilikuwa na sehemu nyingi zilizogawanyika zenye michoro aina tofauti tofauti na kila mchoro ulikuwa na maana yake. Vijana hawa walifundishwa namna ya kuchora mchoro huu wa “mregho” ambao ulichorwa katika mti ulioitwa “mringonu” kwa kukata michoro kwenye maganda yake ungali mbichi na kuacha ukakauka. Urefu wake ni kama mkongojo mzima, unaweza kuwa mfupi zaidi, bora tu michoro iweze kuenea na kusomeka.
-Kila aina ya mchoro huu una maana yake ambao huelezwa kwa mafumbo. Imegawanyika katika sehemu mbalimbali kadiri ya maeneo ya uchagga yaliyokuwa na michoro yao. Sehemu zenyewe za fimbo hii ni kama zifuatazo;-
i. Kirongocha: Huu ni mchoro wa upande wa chini wa fimbo ambako kumepekechwa tundu mbili ndogo fupi, moja ni kubwa kuliko nyingine. Wachagga huitaja sehemu hii hivi: “Kirongocha kilekurongocha cha lilya wakeku(bibi wakubwa) akurongocha kawada njia yeende mana, ma kima alalewada njia yeende mana nyi kwui awu na wama wawechiida wache ilufee?”
Tafsiri yake: “Kirongocha ni kipekecho kilichopekechwa kama vile bibi alivyoumbwa akawa na viungo vya uzazi akaweza kumzaa baba na mama, kwa sababu kama hakuwa na njia ya uzazi asingaliweza kuwazaa wazazi wetu. Ufafanuzi wake; Farji ya mwanamke.
ii. Moselu: Hii ni picha ya kitu kilichochongeka, nayo husemwa hivi; Moselu alikuseluo cha lilya mendi awu na wama waseluo nyi ambo(kisu cha kutahiri) lilya mendi warino wakayeremka mbiu yawo wakawa wandu warine, wakakundana, wakaalikana, naaho wakafee wana wakaghorokia uruka lu na Mangi yawo meendi ghalya neenu”.
Tafsiri yake: “Moselu ni kkitu kilichochongeka kama vile wazazi walivyotahiriwa kwa kile kisu cha kutahiria walipokuwa katika ujana wao wakatakata, wakapendana, wakaoana wakazaa na wana ambao wamesimamia nchi wakasaidiana na Mangi wao mpaka hivi leo.
Ufafanuzi wake: “Tohara ya wazazi ni takaso kabla ya ndoa”.
-Sehemu ya 3, 11, na ya 15 zote huitwa kwa jina la “MSHINGO”, maana yake ni kizibo. Mshingo wa kwanza husemwa hivi; “Mshingo ulekushinga cha Msanya akushinga lya Ndaalyio lya mendi au wusunyi”.
Tafsiri yake: “Kizibo kimejiziba kama vile Msanya(jina la mwanamke) alivyojiziba alipokuwa na mimba ya mtoto wake Ndaalyio”.
Ufafanuzi wake: “Mwanamke mwenye mimba haingii mwezini”.
Sehemu nyingine za mshingo zinazidi kueleza kwa mafumbo kama fumbo hili mambo yanayohusu mwanamke kuingia mwezini.
iv. Sehemu ya 4, 6, 8, 10, 12, 16 na ya 18 huitwa kwa jumla “MREGHO” maana yake “Mchoro”. Zote zina miviringo ambayo jumla yake ni miviringo 65. Hueleza habari za mtoto anavyopata viungo vyake katika tumbo la mama yake. Kila mviringo unataja kiungo kimoja na kazi yake jinsi mifano ifuatayo inavyotuonyesha.
a. “Mregho ulekuregha cha kiki, ulekuregha cha ili mndu mka akurega na monoke usunyi, more ochiumba kaghamba lako nyi ashimbo nyi ndewu numa kakoya nyi more.
Tafsiri yake: “Mchoro umejichora kama vile mwanamke mzito anapokuwa na mimba ya kwanza akadhani kwamba amevimbiwa, lakini kwa sababu ya kujua “Shigha” na “Mregho” akafahamu kwamba hakuvimbiwa bali kichwa cha mtoto kinaumbwa katika tumbo lake. Ufafanuzi wake: Kichwa cha mtoto kinaumbwa katika tumbo la mama.
b. “Mregho ulekuregha cha kiki, ulekuregha cha simba ikakuregha na monoyo ikawara mawoko maapfinya ikaowesha mando goose ikawona nyama”.
Tafsiri yake: “Mchoro umejichora kama vile simba jike mwenye mimba alivyojitunza hivi kwamba mtoto aliye tumboni akapata mikono yenye nguvu, akatisha wanyama wote porini, akapata nyama za kula”. Ufafanuzi wake: “Mikono ya mtoto inaumbwa tumboni mwa mama yake ili apate kufanya nayo kazi ajipatie riziki yake.
c. “Mregho ulekuregha cha kiki, ulekuregha cha kilodanga(sungura) akuregha na monoke karosa maru gearanyia”.
Tafsiri yake: “Mchoro umejichora kama sungura aliye na mimba alivyomlea mwanawe tumboni akaota masikio ya kusikiliza”.
Ufafanuzi wake: “Mtoto anaota masikio tumboni mwa mama yake”.
d. “Mregho ulekuregha cha kiki, ulekuregha cha njofu ikuregha na monoyo ikalya na mara ga mtsuru ilyi iwei na uroo woyo imana lyikawada madende maapfiya gechumia ipfo ngurunyi.
Tafsiri yake: “Mchoro ulijichora kama vile tembo alivyolea mimba yake kwa kula majani ya msituni, mtoto wake akapata miguu ya nguvu ili aweze kutembea msituni”. Ufafanuzi wake: “Mchoro unaonyesha miguu ya mtoto inaumbwa tumboni mwa mama yake”.
e. “Mregho ulekuregha cha kiki, ulekuregha cha mbeta ikuregha na ialeya lyalo likachewara meso makaramtsu yekuringa na mlasi”.
Tafsiri yake. Mchoro umejichora kama njiwa alivyojichora na makinda yake yakapata macho ya kumwezesha apate kujificha mwindaji anapokaribia.
Ufafanuzi wake: “Macho yanakuwa tumboni mwa mama yake”.
Michoro hii ya Mregho huendelea kutajwa hivi kwa mafumbo, kila mviringo ukatajiwa mnyama fulani mwenye uzuri wa mwili au kiungo kinachopatana na uzuri au kiungo kile cha mtoto kinachoumbwa katika tumbo la mama.
Sehemu ya 5, nay a 7 huitwa “MOLEMA”. Maana yake ni mchoro ulikunjwa. Huitwa hivi kwa sababu kila sehemu ina michoro saba iliyokunjika, hivi jimla ya michoro ni kumi na mine. Kila mmoja wa michoro hii unaeleza kwa mafumbo habari, kazi na taratibu za utawala wa Mangi, kama mifano ifuatayo inavyotuonyesha.
a. “Molema ulekulema cha Mangi alema uruka kalusanyia handu hamwi lulanyanyarike”.
Tafsiri yake: “Mchoro umekunjika kama Mangi alivyokunja nchi akaikusanya pamoja ili isitawanyike”.
Ufafanuzi wake. “Mangi ndiye mlinzi wa nchi, huzunguka nchi yake akajishughulisha hivi ili watu wake wasitawanyike, bali wawe pamoja chini yake. Hivi Mangi huikunja nchi akaikusanya”.
b. “Molema ulekulema cha njofu ikulema ikashaa mana kawada membe, Mangi kawutaho membe tso karing natso uruka na wusuri woke”.
Tafsiri yake: Mchoro umejikunja kama ndovu alivyojikunja akazaa mtoto, akaota pembe, Mangi akazichukua pembe hizi akalinda nchi na utajiri wake”.
Ufafanuzi wake: “Pembe za tembo ni zenye thamani sana, kwani kwazo Mangi hulinda nchi pamoja na utajiri wake(kwa mfano watu wakichukuliwa mateka Mangi hulipa pembe za tembo ili kuwakomboa; au ikiwa nchi ina deni la nchi nyingine Mangi hulipa pembe za tembo.
c. “Molemo ulekulema cha uruka lo Mangi lukulema na marasa yalo na ngyuruka tsa mrasenyi”.
Tafsiri yake: “Mchoro umejikunja kama nchi ya Mangi ilivyojikunja mipakani inapopakana na nchi za majirani”.
Ufafanuzi wake: “Matengenezo ya utawala kati ya nchi za majirani”.
d. “Molema ulekulema cha Mangi na njama tsake kulya mengenyi yake kasungusiapfo wandu na moondu yawo woose, uruka lukoramia”.
Tafsiri yake. “Mchoro umejikunja kama vile Mangi aketivyo na raia zake kwenye uwanja wa baraza, akaweza kuonana na kuamua mashauri ya raia wote.
Ufafanuzi wake: Kuamua mashauri ya watu.
Michoro hii huendelea kutaja mafundisho ya namna hii kwa mafumbo.
Sehemu ya 9, 13 na ya 17 huitwa “MONJARO”, maana yake ni “Michoro” au “Mchoro” wa mkwaruzo. Hii ni michoro ambayo katika sehemu zote imo jumla ya michoro 25. Kila mmoja hueleza kwa mafumbo mbalimbali, shughuli zote zinazohusu raia wa nchi na ubora wake, kama ukulima, biashara, ufugaji, mapishi na vinginevyo. Mifano ifuatayo inaonyesha jinsi mafumbo haya yanavyotajwa.
a. Monjaro alekucharuo cha wandai, ma sile wandai nyi kwi muwechirema shelya”
Tafsiri yake: “Mchoro umejikwaruza kama ardhi ilivyotokea kwani ardhi isingalikuwako tungelilima wapi tupate chakula?”. Ufafanuzi wake: “Ukulima”
b. Monjaro alekucharuo cha mtsana o menya akucharua na ng’anya yake lilyamandi alutsanyia ng’ori ikalasa umbe waka wakanyo mlaso”.
Tafsiri yake: “Mchoro umejikwaruza kama vile mhunzi alivyojikwaruza alipokuwa akitufulia chuma cha mshale ya kutobolea vena ya ng’ombe akiwa hai ili wanawake wazazi wapate damu yake yenye nguvu wainywe.
Ufafanuzi wake: “Uhunzi”.
c. Monjaro alekucharuo cha mmbe ikucharuo kulya mmba ko Msanya(jina la mwanamke) ikashaa lukanyopfo maruwa, na sari yealyia nginda”.
Tafsiri yake: “Mchoro umejikwaruza kama vile ng’ombe alivyojikwaruzo kwenye nyumba ya Msanya akazaa, tukapata mazima ya kunywa na mbolea ya kustawisha mashamba yetu.
Ufafanuzi wake: “Kwa ufugaji wa ng’ombe tunapata maziwa ya kuwapa mama wazazi na mbolea ya kustawisha mashamba yetu”.
Sehemu ya 21 “MOFULU” , hii ndio mwisho wa fimbo na ni tundu dogo iliyopekechwa ndani, nayo husemwa hivi: “Mofulu ulekufuluo cha lyilyendi womoo ekufee kofuluka kulya ndewunyi kosongora mroe uwefeo, kocha na mafuo ghapfo”.
Tafsiri yake. “Mchoro umejitengeneza kama vile mama alipokuwa akikuzaa, ukageuka tumboni mwake ukatanguliza kichwa ulipokuwa ukizaliwa, ukaja duniani u mzima na viungo vyako vyote”.
Ufafanuzi wake. “Mtoto mzima anazaliwa na viungo vyake vyote”.
-Katika tundu ya hii Mofulu huwekwa udongo mwekundu uitwao “kimaande”; maana yake tendo hili ni kwamba wasichana wa rika wakiisha soma michoro hii na kuhitimu wakatembea na fimbo iliyokwisha chorwa hushindana na wasichana wengine au wavulana wajuao kwani yalikuwa mambo makubwa na ya kujivunia miaka hiyo. Msichana ambaye hakujifunza hayo alifanana na mtu ambaye hajasoma wa miaka hii. Inaonyesha kuhitimu katika masomo ya ujana.
-Mwisho wa mafundisho haya ya “Shigha” na “Mregho” Mwalimu wa haya mafundisho husema “Wana wako ngamempfunda mapfundo ghang’anyi, ngama nanyoe mupfunde wananyu. Hoi Ruwa malele, hee”.
Tafsiri yake. “Wanangu nimewafundisha mafundisho makuu nanyi mpate kuwafundisha wadogo zenu. Ee Mungu na iwe hivyo milele”.
-Mambo mengi ya aina hii na mafundisho mengi haya yalitokea katika karne za 17, 18 mpaka 19 hivi lakini wakati kitabu hiki kinaandikwa miaka ya 1940’s mambo mengine yalikuwa yameanza kupotea. Hapa unaweza kuona kwamba Wachagga miaka ya nyuma kabisa hata kabla ya Wamisionari na Wakoloni waliweza kuwa na utaratibu wa kupeana elimu iliyotanua sana fikra zao na kukuza busara yao katika kukabiliana na mambo mengi ya maisha japo mengine ilihitaji kuboresha zaidi au kupatiwa mfumo mzuri zaidi katika kuitoa. Lakini pia mafundisho haya yalitolewa kwa lugha ya maandishi ya kichagga.
-Katika kila rika linaloingia katika utaratibu wa Wachagga miongoni mwa vijana wa rika huchaguliwa vijana kumi na wawili ambao hufundishwa siri za michoro juu ya mawe. Vijana wakiisha fundishwa mambo hayo hupelekwa kwa Mangi wakaapishwe wasitoe kamwe siri zinazohusu Mangi na nchi nzima. Vijana hawa watakuwa kazi yao ni kuaminiwa na kuwa wasiri wa Mangi na nchi. Iwapo nchi imepigwa vita, Mangi akalazimishwa kuondoka nchini mwake, baadhi ya vijana hawa watafuatana naye popote aendapo, na wengine watabaki nchini wakaaminiwa kuficha mali ya Mangi salama bila ya kumwonyesha mtu yeyote, mpaka hapo Mangi atakapoweza kurudi nchini mwake. Wao ndio wanaoanza kuarifiwa ikiwa Mangi anataka kuipelekea nchi jirani vita; pia wao ndio wapenzi wa Mangi wanaotumwa naye kwa ujumbe wa siri wowote.
ITAENDELEA ….,
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255754 584 270.