“NDEKOCHA” BINTI WA KICHAGGA ALIYEUAWA KIKATILI KUPEWA MTAA HUKO BREMEN, UJERUMANI.

– Kupitia historia tunafahamu kwamba utawala wa wajerumani hasa katika miaka ya mwanzoni ulikuwa ni wa kikatili sana na mwasisi wa ukatili huu uliokithiri alikuwa ni mtu maarufu tuliyemsoma kwenye historia Karl Peters. Karl Peters watu wanahistoria wengi wa karne ya 21 wanamchukulia kama alikuwa ni nusu mwendawazimu kwa jinsi alivyotekeleza vitendo vingi vya ukatili uliokithiri. Huko Ujerumani anaitwa “mnyongaji Peters” au “nusu mwendawazimu”.

– Kuna watu wengine wanamchukulia Karl Peters kama mtu aliyekuwa na ile roho mbaya sana ya kufurahia mateso na udhalilishaji wa wengine, “sadist”. Hili linatokana na jinsi alivyochukulia ni jambo la kawaida kuua, kubaka na kufanya vitendo vya kikatili sana kwa binadamu wenzake. Hivyo baada ya mambo mengi aliyofanya mwishoni mwa karne ya 19 Afrika mashariki na hususan Kilimanjaro anachukuliwa ni kati ya watu wa hovyo kuwahi kutokea.

– Kati ya vitendo vya kikatili alivyofanya Karl Peters ni pamoja na kumyonga binti wa kichagga aliyeitwa Ndekocha ambaye alikuwa amemchukua kama hawara wake. Ndekocha alikuwa ni binti mrembo sana kutoka Marangu ambaye alikuwa kwenye mipango ya kuolewa na Mangi Malamya wa Mamba. Lakini baadaye huenda pia kwa msaada wa Mangi Ndegoruo Ndekocha alichukuliwa na Karl Peters aliyekuwa amehamisha makao makuu ya Wajerumani Kilimanjaro kutokea Old Moshi kwenda Marangu akiwa kama hawara wake. Lakini kutokana na vitendo vingi viovu sana na maisha ya wasiwasi kwa Karl Peters Ndekocha hakupenda kuishi na Karl Peters.

– Ndekocha alifanikiwa kutoroka Marangu na kukimbilia Mamba kwa Mangi Malamya ambapo alipokelewa kama mke wa Mangi Malamya wakati huo Mangi Malamya akiwa hafahamu kama kuna uhusiano wowote kati ya Ndekocha na Karl Peters. Karl Peters alipokuja kugundua alipokimbilia Ndekocha aliivamia ngome ya Mangi wa Mamba na kwa hasira alimpindua madarakani Mangi Malamya mtoto wa Mangi Mlawi na kumtawalisha kwenye kiti cha umangi ndugu yake aliyeitwa Kuimbere.

– Baada ya hapo Karl Peters aliondoka na Ndekocha kurudi Marangu lakini naye kwa hasira aliishi kumnyonga mpaka kufa kwenye mti uliokuwa kwenye kingo za mto Una karibu na mji mdogo wa Marangu Mtoni ya leo. Tukio hili la kusikitisha sana lakini lililopata umaarufu lilikuwa ni moja kati ya matukio mengi ya kikatili sana yaliyofanywa na Karl Peters Kilimanjaro.

– Kwa sasa huko Ujerumani na Ulaya kwa ujumla kuna harakati nyingi zinazoendelea kuondoa heshima feki waliyopewa wasiostahili na kuwapa watu waliokuwa wahanga wa maovu ya hao mashujaa feki. Sasa huko katika mji wa Bremen, Ujerumani kuna mtaa ambao ulikuwa na jina la Karl Peters ambaye kwa sasa ni moja kati ya watu waliopoteza kabisa heshima waliokuwa nayo na wanaodharaulika sana. Mtaa huo unatakiwa kubadilishwa jina la Karl Peters na kupewa jina lingine.

– Hivyo sasa kutokana na hadithi ya binti mrembo sana wa Kichagga Ndekocha aliyenyongwa kikatili na Karl Peters pale Marangu Mtoni kupata umaarufu mkubwa huko Ujerumani, kikundi kimoja cha wanaharakati katika jiji la Bremen, Kaskazini ya Ujerumani wanaolaani vikali vitendo hivyo vya Karl Peters wamependekeza mtaa huo unaobadilishwa jina kupewa jina “Ndekocha”. Mmoja kati ya wanaharakati hao wa mrengo huo wa siasa za Ujerumani amenitafuta kutaka kupata uhakika wa usahihi wa jina na usahihi wa hadithi husika ili kuweza kuliongezea uzito wa kuwa jina la heshima la mtaa huo.

– Kama jina la “Ndekocha” litapita basi binti huyu wa kichagga aliyenyongwa kikatili mpaka kufa na Karl Peters mwaka 1892 pembezoni mwa kingo za mto Una, Marangu atakuwa amepewa heshima ya kipekee dhidi ya udhalilishaji mbaya aliofanyia.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270

You may also like...

Popular Posts

1 Comment

  1. Alexander joachim nyalu says:

    NIMEFARIJIKA SANA.NAPENDA KUJUWA KUHUSU UKOO WA NYALU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *