WACHAGGA TUNA HAZINA KUBWA SANA INAYOENDELEA KUPOTEA, TUNAPASWA KUJIONGEZA.

– Moja kati ya vitu ambavyo watu wengi sana wanahofia na pamoja ni kupotea kwa urithi wetu muhimu sana ambao umerithishwa kutoka kwenye vizazi vilivyopita unaofikia mpaka maelfu ya miaka. Urithi huu ni mila, desturi na tamaduni kwa ujumla na hasa vitu muhimu kama lugha ambayo inahifadhi historia na fasihi nzima ya jamii iliyobeba tafsiri ya vitu vingi sana muhimu ndani yake.

– Lugha ni msingi mkuu kwa sababu kuna vitu vingi ambavyo haviwezi kuelezewa kwa lugha nyingine yoyote duniani vikaeleweka kwa usahihi na kuleta maana sahihi iliyokusudiwa isipokuwa kwa lugha ile yenyewe husika ya jamii hiyo. Baadhi ya mashirika makubwa ya kimataifa yanayohusika na masuala ya tamaduni na mambo ya asili yamekuwa yakipigania sana na kutetea utunzaji wa mila na tamaduni asili za maeneo kwani mambo hayo huenda sambamba sana na utunzaji wa mazingira pia.

– Hata hivyo pamoja na yote hayo bado kuna watu wengi wamepoteza matumaini kabisa kwamba baadhi ya mambo muhimu ya zamani yanaweza kutunzwa katika dunia ya leo inayokwenda kasi sana huku mambo mengi yakimezwa na mengine kupuuzwa kabisa. Hakuna juhudi zozote zenye nguvu zinazofanyika katika kulinda au kutunza tamaduni hususan lugha katika mazingira ya sasa ambapo hata imani na mitazamo iliyojengwa juu ya mambo hayo ni potofu na hasi sana.

– Kuna msemo maarufu wenye ukweli ndani yake unasema hakuna changamoto isiyokuwa na suluhisho, kwa kiingereza wanasema, “Every problem has a solution”. Yaani hata katika eneo ambalo watu wamepoteza matumaini ni kwamba suluhisho lipo lakini ni aidha watu hawaoni haja ya kujihangaisha kufanyia kazi changamoto hiyo au bado hawajafikiria kwa kina na kwa usahihi wa kutosha kuja na suluhisho sahihi kwa tatizo husika. Hivyo hata hilo la kupotea kwa lugha ambayo ni moja ya utambulisho muhimu wa jamii yetu kuna suluhisho, tena kuna masuluhisho mengi ya njia tofauti tofauti.

– Moja kati ya njia nzuri za kutunza lugha na hata tamaduni nyingine ni kupitia burudani mbalimbali kwa kutumia lugha hiyo na hasa kupitia nyimbo za aina mbalimbali. Nyimbo zimekuwa ni sehemu muhimu sana za maendeleo na kuimarika kwa jamii ya wachagga katika nyanja mbalimbali zikitumika kuhamasisha mambo mengi muhimu ya kijamii na zikiwa na mafanikio makubwa. Kuna nyimbo nyingi sana za zamani ambazo bado zinajulikana na wazee japo nyingine nyingi zikiwa zimepotea.

– Kupitia maandiko mbalimbali yanayozungumzia historia ya wachagga zamani tunaweza kuona maeneo mengi sana ambayo nyimbo pia zikitumika kuelezea mambo mbalimbali na kuhifadhi taarifa muhimu. Kimsingi nyimbo zimetumika katika kuhamasisha shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kila nyanja. Kwa mfano kwenye kitabu kilichoandikwa na Prof. R. Sambuli Mosha cha “The Heartbeat of Indigenous Africa, the Study of Chagga Education System”, Prof. Mosha ameelezea jinsi Mangi Rindi Mandara alikuwa akitumia nyimbo alizokuwa anatunga pamoja na ngoma katika kuhamasisha vita ambapo nyimbo zilitumiwa kuleta hamasa na kuwezesha ushindi katika vita mbalimbali.

– Tumeona pia kwenye kitabu cha Mary Kathleen Stahl, “History of the Chagga People of Kilimanjaro” kwamba vita kati ya Machame na Kibosho iliyoacha simanzi kubwa iliacha pia urithi wa nyimbo zinazoielezea kwa pande zote mbili. Kupitia Mary Kathleen Stahl tuliweza kuelewa ukuu wa Mangi Horombo kupitia wimbo uliodumu karibu miaka 150 ukielezea ukuu na umashuhuri wake huku ukiwa umehifadhi lugha halisi iliyotumika wakati huo. Pia tuliweza kuona shairi lililotungwa na Mangi Rindi Mandara na kuelezea ujumbe wake wa mwisho wa watu wake lililotafsiriwa na kuandikwa na Dr, Bruno Guttman.

– Kupitia pia wasifu wa kijana Sameni ole Kivasisi au Justin Lemenye tuliweza kufahamu mtazamo wa wachagga na namna walivyochukulia ushindi wao dhidi ya wajerumani baada ya vita ambayo majeshi ya Mangi Meli Mandara yaliposhinda vita ya kwanza dhidi ya wajerumani kupitia wimbo ulioimbwa, “Ngoti ilelemba Mandumbo”. Mpaka sasa bado ziko nyimbo nyingi mbalimbali za matukio ya zamani ambazo baadhi ya wazee wanazifahamu angalau kwa kuzirithi kutoka kila eneo la Uchagga, Kilimanjaro ambazo ni hazina kubwa kwetu ambayo bado tunayo ukiachana na baadhi ambazo zimeshapotea na hatuwezi kuzipata tena.

– Nyimbo hizi jambo la kwanza zimebeba jumbe muhimu zinazoongeza taarifa na maudhui mengi katika historia na tamaduni za wachagga lakini pia zinabeba lugha ambayo inaweza kudumu kwa miaka mingi sana kama tutazitengenezea utaratibu sahihi. Nyimbo hizi kwa kutengenezewa utaratibu sahihi zinaweza kuhakikisha lugha ya kichagga inadumu kwa muda mrefu huku ikiwa na umuhimu mkubwa pia.

MAPENDEKEZO YANGU.

– Tuna wasanii wengi wanaopenda kutunga na kuimba nyimbo mbalimbali za kichagga na baadhi ni waimbaji wazuri sana. Waimbaji hawa wanajitahidi kutunga nyimbo zao wenyewe zenye jumbe mbalimbali za kisasa na ni nyimbo nzuri sana japo hazipewi sana nafasi katika vyombo vya habari na maeneo mengine kwa sababu pengine ya mitazamo potofu kwenye jamii, ukisasa uliokithiri pamoja na uzembe na kutojali.

– Sasa tunaweza kuweka utaratibu wa kuchanga fedha na kuzitumia kumlipa msanii ambaye atakuwa tayari kutengeneza wimbo kwa viwango bora sana na kuuimba pamoja na kuutangaza katika maeneo mbalimbali. Uzito mkubwa tunaweza kuuweka kwenye kutafuta nyimbo za zamani kupitia wazee ambao bado wana kumbukumbu ya nyimbo nyingi vichwani mwao kisha kuboreshwa na kuimbwa na wasanii wa leo wa kichagga kwa lugha husika. Wimbo unaweza kuboreshwa zaidi lakini usipoteze ule ujumbe muhimu uliokuwa unakusudiwa. Kwa mfano hata wimbo tu uliokuwa wimbo wa taifa la wachagga wakati wa utawala wa Mangi Mkuu, haujulikani kabisa lakini upo na una ujumbe muhimu unaoweza kutuhamasisha wengi katika mambo mbalimbali ikiwa utaimbwa kwa namna ya kuvutia na kuelimisha.

– Lakini pia ikiwa msanii anaweza kuja na wimbo wake binafsi wenye maudhui na ubora unaoridhisha anaweza pia kupatiwa fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuutangaza pia. Jambo la muhimu ni kuhakikisha kwamba tuna nyimbo nyingi na wasanii wengi ambao wana kazi moja ya kuhakikisha kwamba mila, desturi na tamaduni za wachagga ikiwemo lugha vinajenga ushawishi mkubwa kwa wachagga na hata watu wa jamii nyingine. Kwa namna hii tuna uhakika wa kutunza na kuhamasisha mshikamano katika kufanikisha agenda nyingine muhimu kwetu ikiwa taratibu muhimu ambazo zinaenda zikipotea. Nyimbo zikiwateka watu zitahamasisha pia watu kujifunza kichagga, japo hata hivyo wimbo ukiwa mzuri unaweza kuwa burudani bila kujalisha lugha yake.

– Wako wasanii wengi wazuri wa kichagga wenye uwezo wa kutusaidia sana katika hili kwa kuweka kazi na ubunifu mkubwa katika eneo lao ambalo wanalipenda sana lakini wengi wamekata tamaa kutokana na kukosa kuungwa mkono kwa kazi zao na hata kukosa fedha kutokana na kazi zao nzuri. Ikiwa tutakuwa tayari kununua miradi yao hiyo ya nyimbo basi tutaweza kujikuta tumeleta shamrashamra kubwa sana katika eneo hili na kuongeza hamasa na shauku ya kuendelea kuboresha maeneo mengine.

– Kuna wasanii tunaowafahamu kutoka Machame, Kibosho, Old Moshi, Kilema, Marangu, Mwika, Rombo na wengine katika maeneo mengine ambao hatuwasikii sana lakini wanaweza kuwa na utayari mkubwa ikiwa tutaonyesha utayari wa kuwalipa katika miradi yao hiyo.

Karibu kwa Maoni, Ushauri au Maswali.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *