UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 11.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

USAWI (UCHAWI) KWA WACHAGGA.

-Katika nchi ya Uchagga tuliogopa sana “usawi” (uchawi) toka zamani sana. Huu uchawi ulitisha watu wote, wakubwa kwa wadogo, waume kwa wake, watoto mpaka Wamangi. Ulitisha kuliko magonjwa ya kifua kikuu na ndui. Kwani mtu mzima aliweza kula na mgonjwa wa kifua kikuu lakini haikuwa jambo rahisi kwa Mchagga kula na mtu aliyetuhumiwa kuwa ni mchawi.

Tulitishwa hivi kwa miaka mingi na hata watoto walirithi uoga ule na mpaka sasa; kutokana na kuugopa sana uchawi ulipata nguvu na kutawala sana roho zilizouamini. Wazee walisimulia habari za uchawi kwamba hakuna anayejua uchawi ulivyo isipokuwa mchawi mwenyewe, na haujulikani kwa watu wote kwa kuwa mambo yenyewe ni siri ya wachawi wenyewe.

Hata hivyo tulikuwa tukisikia kutoka kwenye jamii na mataifa mengine kuhusu mambo makubwa sana yanayofanywa na wachawi wa mataifa hayo ambayo huku kwetu hayakuwepo wala kuwezekana kama miujiza mikubwa.

-Kwa hakika uchawi ulitisha sana katika nchi ya Uchagga, na mpaka sasa hofu ile bado iko, lakini tukifikiri na kuangalia jinsi uchawi wa namna mbalimbali unavyofanyika bila shaka tunaona hakuna uchawi wa kweli. Hadithi nyingi huzungumzwa juu ya uchawi lakini ukiuliza ni mtu gani aliye mchawi ili uambiwe siri ya uchawi wake hutampata.

Watu waliotuhumiwa kuwa ni wachawi walihukumiwa kwa kupewa dawa inayolevya sana iitwayo “kimanganu” maana yake, kitu kinachomaliza ubishi wa mtu mkaidi. Dawa hii iliwafanya waongee kila kitu kuelezea namna wanafanya uchawi lakini walishindwa kusema na mwisho waliishia kusingizia wamefanya jambo fulani baada ya maumivu makali ili waachiliwe tu lakini sio kweli.

-Mimi nathubutu kusema kuwa Wachagga huzungumza siku hizi habari za uchawi wa namna hizi kwa kusikia tu lakini hawajui; Na hata wale waliokuwa wakiuamini sana na kutafuta waganga wawasaidie zamani, walikuja kuudharau na kutoa habari za maisha yao walipokuwa wakiogopa uchawi. Hofu imeendelea kuwapo kwa sababu tulizaliwa katika woga, na mpaka sasa bado kuna Wachagga wanaogopa uchawi licha ya kwamba hawaujui.

Tumeweza kuona kwamba Wachagga walishaudharau uchawi zamani baada ya kudadisi na kukutana na uzushi mwingi na kuogopeshana ndio maana huwezi kupata Mchagga mganga wa kienyeji wa zama hizi kwani shida hizo za uchawi ambazo zinawafanya watu kwenda kwa waganga kwa Wachagga zilitoweka zamani hivyo waganga hawakuwa wanahitajika tena.

Lakini hata hivyo bado utakuta watoto wanaozaliwa siku hizi na kukutana na watu wa jamii nyingine ambao bado wako nyuma kwa maswala haya na bado wanahofia mambo ya uchawi wanawaogopesha upya na wanaendelea kuamini na kuogopa uchawi kiasi cha kufikiria kutafuta waganga wa kienyeji kuwasaidia.

ITAENDELEA ….. !!!

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *