RAI YA MWAKA MPYA.

Tujenge Utamaduni wa Kusoma, Tukuze Uwezo wa Kusoma.

– Kiasili kila kiumbe ameendeleza uimara katika eneo fulani la mwili wake au maeneo fulani ya mwili wake yanayomwezesha kukabiliana na mazingira anayoishi na hivyo kuishi kwa ubora zaidi. Kwa mfano baadhi ya wanyama wana nguvu, mbio, meno na makucha yanayowawezesha kuwinda wanyama wengine kwa mafanikio na kuweza kuishi. Hivyo kila mmoja kukabiliana na mazingira yake kwa namna hiyo.

Kwa upande wa binadamu eneo la mwili aliloendeleza linalompa manufaa makubwa zaidi na kuweza kukabiliana na mazingira yake kwa mafanikio makubwa zaidi ni ubongo wake ambao ndio chanzo cha akili yake. Akili ya binadamu ndio iliyomwezesha kufanikiwa kupiga hatua kubwa kutoka kuishi kwenye mapango na kwa uhasama mkubwa baina ya kundi moja na jingine mpaka kufikia kuishi kwenye mazingira bora sana na kwa utulivu na maelewano ya hali ya juu. Haya yameenda sambamba na maendeleo makubwa ya kiteknolojia ambayo yamefanya maisha kuwa rahisi sana. Yote haya yamewezeshwa na uwezo mkubwa wa akili ya binadamu.

– Hivyo akili ya binadamu ni baraka kubwa kwa binadamu mwenyewe na dunia kwa ujumla kwani ukilinganisha na viumbe wengine walioendeleza viungo vingine vya miili yao, binadamu ambaye ameendeleza ubongo na kuinoa akili ameweza kufanya makubwa kuwazidi mbili na hata kuitawala dunia ikiwemo na viumbe wengine wote. Sasa akili hiyo iliyofanya mambo yote makubwa kiasi hicho ili iweze kutuletea manufaa zaidi kila siku inapaswa kunolewa kila siku ili kuwezeshwa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kwa viwango bora zaidi.

– Kama ilivyo kwamba kufanya mazoezi kunaimarisha misuli ya mwili ndivyo hivyo ilivyo kwamba kusoma mambo mbalimbali hususan vitu vinavyohusisha tafakuri za kina kunasaidia kuimarisha akili na kuifanya kufikiri kwa kina na kwa undani sana.

– Tunafahamu kwamba mifumo yote ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, mifumo ya ufanyaji kazi n.k. imeweza kuwa bora na yenye ufanisi kutokana matokeo ya falsafa bora zilizoendelezwa na kuandikwa na watu waliokaa wakasoma, kujadili na kufikiri kwa kina sana mpaka kufikia hapo. Usomaji huu wa falsafa ni kati ya usomaji unaohitaji utulivu mkubwa wa akili kuweza kupata uelewa huo mkubwa unaolenga kuboresha maisha ya kijamii tunayoishi yawe na manufaa makubwa kwetu.

– Sio rahisi kutengeneza mawazo bora au kujenga hoja zenye ubora mkubwa kama akili yako haijatanuka sana kwa kupitia kazi ya kusoma na kuelewa mambo mengi. Ufikiri wa mtu huweza kutoka kwenye ufikiri wa kawaida na wa moja kwa moja kwenda kwenye ufikiri wa kina na tata (complex thinking) kupitia kusoma na kujaribu kuelewa mambo au dhana zinazoonekana kuwa ni ngumu kwa kwa undani na kwa kina sana.

– Hata hivyo kwenye jamii na hasa wale waliotengeneza mifumo ya kinyonyaji ya kijamii na kisiasa wanafurahia watu wengi kubaki na uwezo duni wa kufikiri kwani ni kwa namna hiyo wanafanikiwa na kuendelea kunufaika kupitia uduni wao wa kufikiri. Kuna watu wengi kwenye jamii ambao kutokana na uwezo duni wa watu kufikiri wanaaminiwa kuwa ni mashujaa na wakombozi wao kumbe ni matapeli, wanyonyaji na waharibifu wa jamii. Lakini kwa sababu ya watu wengi kutotaka kukuza uwezo wao wa kufikiri kupitia kusoma kwa kina mambo muhimu mbalimbali na kuelewa undani yale yanayoendelea kwenye jamii.

– Chanzo cha uduni wa maisha na uduni wa maeneo mengine mengi ya kimaisha unaosababishwa na ubovu wa mifumo iliyowekwa kwa makusudi na watu wenye nia ovu unaendelea kuiumiza sana jamii kwa sababu sehemu kubwa ya watu wanaopaswa kufanya mabadiliko hayo wanakosa uwezo wa kufanya ufikiri wa kina kuelewa chanzo cha matatizo yao.

– Moja kati ya waanzilishi wa taifa la Marekani ambaye pia ni mwanasayansi mgunduzi mashuhuri ambaye pia ni mkuu wa kwanza wa shirika la Posta la Marekani ambaye picha yake ndio ipo kwenye noti ya dola 100 za kimarekani Benjamin Franklin alipata kusema uwekezaji kwenye maarifa siku zote unalipa faida zenye ubora wa hali ya juu. “Investment in knowledge always pays the best dividends”.

– Hata hivyo, kwa bahati mbaya zaidi kwa sehemu kubwa jamii ina mtazamo hasi zaidi kuhusu kusoma na kujenga uwezo imara wa kufikiri kwa sababu huwa hakuna matokeo ya haraka na ya moja kwa moja ya mtu anayesoma au wakati mwingine hakuna matokeo kabisa. Jamii inaamini kwamba jambo muhimu ni kuwa na pesa na kusoma baada ya kumaliza shule ni kuichosha akili na kupoteza muda.

– Mtazamo huu umepelekea kuwa na jamii iliyodumaa sana kuanzia kijamii, kiuchumi na hata kisiasa kwani inaishi kwa mitazamo iliyopitwa na wakati na isiyo sahihi katika dunia inayokuwa kwa kasi sana kiuchumi na kiteknolojia. Japo ni kweli kwamba kupata mafanikio ya kawaida ambayo kwenye jamii zetu yanaonekana kama ni mafanikio makubwa haihitaji uwezo mkubwa kutafakari bali bidii, nidhamu na uvumilivu katika kazi, lakini kupata mafanikio makubwa kiuhalisia au kuendesha taasisi kubwa au mashirika makubwa uwezo mkubwa wa kiakili na kufikiri kwa kina sambamba na kusoma sana.

– Takwimu zinaonyesha kwamba kwa wastani wakurugenzi wa mashirika au makumpuni makubwa anasoma angalau vitabu 50 kwa mwaka. Huu ni wastani tu lakini kuna wengi wanasoma mara mbili mpaka mara tatu yake. Kwa mfano kama umesoma kitabu cha Dr. Reginald Mengi, “I can, I must, I will” utagundua kwamba Mengi mweyewe alikuwa na mkurugenzi anayesoma sana vitabu na mambo mbalimbali na ndio maana aliweza kuwa moja kati ya waafrika wachache sana kufikia mafanikio makubwa sana kiuchumi. Moja kati ya wawekezaji wakubwa sana dunia ambaye mara nyingi huwa hakosekana kwenye orodha ya matajiri watano wakubwa duniani anayejulikana kwa jina la Warren Buffet mwenye umri wa miaka karibu 93 kwa sasa anasema yeye anaamini ili mtu anapaswa kusoma angalau vitabu viwili kwa siku yaani wastani wa kurasa 500 za kitabu kila siku.

– Bilionea Warren Buffet mwenyewe ambaye ni tajiri namba 5 duniani mwenye umri wa miaka 92 ambaye ni mwenyekiti wa makampuni ya Berkshire Hathaway kwa sasa na rafiki yake Bilionea Charlie Munger mwenye umri wa miaka 99 kwa sasa ambaye ni makamu mwenyekiti wa makampuni ya Berkshire Hathaway ni watu wanaosoma sana. Bilionea Charlie Munger anasema watoto wake walimtungia jina la utani kwa kumwita ni maktaba inayotembea. Mitazamo mipya na nguvu mawazo wanayojenga kila siku imeweza kuwasaidia kuwa na mawazo ya ujana hata uzeeni na kupelekea wao kuendelea kufanya kazi hata katika umri wa miaka ya 90 kuelekea miaka 100.

– Faida nyingine kubwa sana ya jamii kuwa na utamaduni wa kusoma sana na hususan kusoma vitabu ni kuishi kwenye jamii iliyostaarabika. Ukweli ni kwamba karibu wanasiasa wote wa dunia hii hupenda kufanya utapeli pale wanapopata nafasi hiyo kwani huwarahisishia kazi na kuwapa uhakika, lakini katika zile nchi ambazo utapeli wa kisiasa uko kwa viwango vya chini na ukomavu wa demokrasia ni wa viwango vya juu zaidi utakuta kuna sehemu kubwa ya raia wake ambao ni “idealists” kwa maana ya wenye uelewa mpana wa dhana mbalimbali kutokana na kusoma na kuelewa namna mifumo mbalimbali inavyofanya kazi.

– Lakini katika zile jamii au nchi ambazo raia wake hawajihangaishi kujiimarisha kiakili na kifikra kupitia kusoma na kutafakari mambo mbalimbali “idealists” hata kama wamejaliwa uwezo mkubwa wa akili kiasili bado utakuta kuna utapeli mkubwa sana wa kisiasa unaoendelea katika nchi hizo. Watu wa jamii hizi huweza kukubaliana na propaganda za wanasiasa zinazolenga kuwahadaa ili kuendelea kuwaweka gizani kwa manufaa ya wenye madaraka. Utakuta wale watu waovu na waharibifu wakitukuzwa na kuonekana ni mashujaa na watakatifu kwa sababu tu uwezo wa raia kuielewa mifumo, falsafa na dhana mbalimbali zinavyowaathiri katika kila nyanja ya maisha ni mdogo sana. Lakini kutukuza huko waovu ni sehemu ya kukumbatia na kuenzi uharibifu waliofanya bila kujua, yaani ni sawa na kujihujumu wenyewe bila kujua.

– Jamii au nchi zilizoendelea zinaonekana kuwa na ustaarabu wa viwango vya juu na mara zote kuwa na mawazo bora, mazingira bora, tamaduni nyingi bora na hata utajiri na uchumi mkubwa kwa sababu ni “idealist” wana utajiri mkubwa wa mawazo yanayotokana na kuelewa mambo mengi mbalimbali na kuwa na akili zilizochangamka. Hata busara na matendo mema yanayokuwa faida kwa jamii nzima badala ya mtu mmoja au wachache kujinufaisha kwa gharama ya kuibia wananchi husababishwa na raia walio wengi kuwa na mawazo bora na mitazamo sahihi inayotokana na kusoma na kuelewa mambo mengi kwa usahihi zaidi.

– Hata hivyo ni ukweli ulio wazi kwamba kazi ya kusoma hasa kusoma vitu vigumu sio rahisi, ni kazi ngumu sana lakini wote tunajua kwamba hakuna kitu chenye manufaa makubwa kinachopatikana kiurahisi. Hii ni kanuni ya dhahabu kwamba chochote kizuri hakijawahi kuwa rahisi na hakuna njia ya mkato ya kufanikisha mambo yenye thamani kubwa. Hivyo ugumu wake ndipo ilipo thamani yake na wale wanaojitoa kuweka bidii na kuvumilia ndio watakaopata manufaa makubwa na kuwa na majuto kidogo katika maisha yao.

– Hatua ya kwanza muhimu katika kujenga utamaduni wa kusoma ni kuanza kwa kutengeneza mazingira yanayojenga na kuhimiza usomaji. Kwa mfano kutengeneza shelf la vitabu nyumbani au kuwa na chumba kabisa cha kujisomea, “study room” kilichojaa vitabu, majarida na zana nyingine zinazohamasisha usomaji. Pia kutenga muda hata kama ni lisaa limoja au mawili kwa siku sambamba na nidhamu kali ya kusoma kila siku katika muda husika. Baada ya muda utakuta utamaduni na mazoea hayo yanaimarika na hata uwezo wa kusoma kwa haraka na kuelewa(comprehension) unaongezeka sana. Huhitaji kusema unabanwa na kazi kwa sababu ratiba yake unapaswa kuipanga nje ya ratiba ya kazi, na kama kweli unahitaji utaahirisha mengine yasiyokuwa na umuhimu mkubwa na kuweka kipaumbele kwa yale muhimu zaidi kwako.

– Manufaa ya mtu kuendeleza uwezo wa kusoma, kujenga utamaduni na nidhamu ya kusoma kila siku unaweza kuanza kuyaona kuanzia miaka mitatu mpaka mitano ya kusoma mfululizo mambo mbalimbali kwa muda wa angalau lisaa limoja kwa siku. Hapa unaweka bidii katika kujaribu kuelewa dhana mbalimbali katika yale maeneo uliyochagua iwe ni sayansi, falsafa, saikolojia, siasa, historia, dini, biashara, uchumi au muunganiko wa fani mbalimbali kwa pamoja.

– Uzuri wa kujenga utamaduni huu ni kwamba utaweza kuuuambukiza kwa watoto wako au wengine wanaokuzunguka ambao kwa kufanya hivyo nao watakuwa na maisha yenye utulivu, yaliyo bora na yenye mafanikio kwa namna waliyoamua kuitafsiri wenyewe. Kwa hili sina namna kusisitiza zaidi umuhimu wake na pia sitatumia nguvu zaidi kupingana na wale wenye mtazamo hasi juu yake kwani matokeo yake yako dhahiri kila mahali.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *