BIBI MAKIMARO KALANGA.

– Mimi na rafiki yangu pamoja na rafiki zetu siku ya mwaka mpya 2023 tulifanikiwa kutembelea huko mitaa ya Kibosho katika kijiji cha Kirima kati, Kida Chini na kukutana na bibi mmoja mcheshi, mchangamfu na mwenye akili sana. Bibi huyu mjasiriamali na mpambanaji sana anayeitwa Makimaro Kalanga ana wastani wa umri wa miaka kati ya 115 mpaka 120 akiwa na nguvu zote, akili sana na kumbukumbu zake zote tangu akiwa binti mdogo kabisa.

– Bibi huyu ambaye anakumbuka karibu kila kitu tangu utoto wake alitueleza kwamba alikuwa binti mdogo wakati Mangi Malamia Mushi, mtoto wa Mangi Sianga alipokuwa mtawala wa Kibosho. Mangi Malamia Mushi alitawala Kibosho baada ya utawala wa baba yake Mangi Sianga tangu mwaka 1911 mpaka mwaka 1917 alipoondolewa madarakani kwa tuhuma za uhaini dhidi ya serikali ya Uingereza. Hivyo kwa makadirio wakati wa utawala wa Mangi Malamia bibi huyu alikuwa tayari ana umri wa wastani wa miaka 10.

– Bibi Makimaro Kalanga ambaye nyumbani kwao alikotokea ni katika kitongoji cha Ngirini, katika kijiji cha Kirima Kati, Kibosho anatokea kwenye ukoo wa Kimaro. Bibi huyu alitueleza kwamba yeye mwenyewe alijaribu kuchumbiwa ili kuolewa na Mangi Ngilisho Sina Mushi wa Kibosho ambaye aliingia madarakani mwaka 1917 baada ya kuondolewa kwa ndugu yake Mangi Malamia. Bibi Makimaro anasema kwamba alikataa kuolewa na Mangi Ngilisho ambaye alikuwa katika miaka ya mwanzoni ya utawala wake kwani alikuwa anaolewa kama mke wa 7 kitu ambacho hakukitaka na hivyo kuamua kuolewa kwenye ukoo wa Kalanga wa Kidachini, Kirima Kati, Kibosho.

– Licha ya umri mkubwa sana wa miaka takriban 120 alionao bibi Makimaro ana kumbukumbu nyingi za tangu miaka ya 1910’s na kuendelea mpaka sasa. Hii ni kusema kwamba Bibi Makimaro alikuwepo wakati vita ya kwanza ya dunia inaanza. Zaidi ya hapo bibi huyu anaongea vizuri sana kiswahili na kichagga na ana nguvu zote pia. Ni mcheshi, mchangamfu, mwenye akili sana na mwenye mambo mengi kichwani kwake ya kueleza na kusimulia tangu miaka ya zamani kabisa ya utoto wake.

Tulikuwa na mazungumzo mazuri sana na Bibi Makimaro na alifurahia sana uwepo wetu pia.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *