#THE JEWISH PHENOMENON# SEHEMU YA 11* #Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

#THE JEWISH PHENOMENON#

*SEHEMU YA 11*

#Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

#TAFUTA KITU CHA KUONYESHA WATU KWAMBA UNAWEZA(KITU AMBACHO KITAKUPA MSUKUMO WA KUWEKA BIDII NA JUHUDI KUBWA).#

-Wayahudi ni jamii ambayo imekumbana na changamoto nyingi sana katika historia, kuanzia kukataliwa, kutengwa, kufukuzwa, kubaguliwa, kukuawa na kila aina ya manyanyaso. Badala ya mambo hayo kuwakatisha tamaa badala yake yamekuwa ndio injini au msukumo wa wao kuweka bidii kubwa zaidi na kuonyesha watu kwamba wao ni watu muhimu sana katika jamii.

-Wayahudi wameendelea kujiona kwamba wanatakiwa kuwa bora kila siku na siku zote kuna jambo jipya la kuboresha zaidi bila kujali mambo yanaenda vizuri kiasi gani.

-Licha ya idadi yao ndogo, Wayahudi wamekuwa ni watu maarufu na mashuhuri kwa maelfu ya miaka kabla hata ya Kristo. Wameacha majina mengi makubwa duniani katika kila fani na nyanja ya maisha kuanzia fasihi, sayansi, falsafa mbalimbali, sanaa, muziki, fedha, biashara, udaktari n.k.,.

-Wayahudi wamepambana sana katika hii dunia katika nyakati zote na mara nyingi katika mazingira magumu, hujma na kila aina ya vikwazo kwao kusonga mbele lakini hawajachukulia hiyo kama sababu ya kusitisha mapambano na badala yake kutafuta njia mbadala kuendelea na mapambano bila kuchoka.

-Himaya nyingi zenye nguvu kama himaya ya Misri ya kale, himaya ya Babeli ya kale na himaya ya Uajemi ya kale ziliimarika kukua na kuwa na nguvu sana duniani na kupata umaarufu mkubwa na umashuhuri kwa miaka mingi takriban miaka 3,000 mpaka 4,000 kabla ya Kristo lakini mwisho zilianguka na kupotea kabisa. Wayahudi walikuwepo nyakati zote hizi wakizishuhudia himaya hizi na mara nyingi walikuwa wahanga wa siasa za himaya hizi lakini walisimama imara bila kuyumba wala kupotea.

-Zikaja nyakati za himaya ya Uyunani/Ugiriki ya kale ambayo ilikuwa ni himaya yenye nguvu na ambayo ilistaarabika na kuwa na wasomi wakubwa ambao walijenga misingi mingi ya falsafa na sayansi inayotumika mpaka leo hii karibu miaka 500 kabla ya Kristo, wakapata umaarufu na umashuhuri mkubwa duniani lakini mwisho Uyunani nayo ilisambaratika na kuangushwa, Wayahudi walikuwepo, waliishuhudia na waliendelea kusimama imara.

-Ikaja himaya yenye nguvu sana ya Rumi iliyotawala karibu dunia yote iliyokuwa na nguvu sana Ulaya yote, ikapata umaarufu na umashuhuri mkubwa duniani ikadumu miaka mingi sana lakini nayo ilikuja kuanguka na kupotea kabisa. Wayahudi walikuwepo walishuhudia yote haya, na walikuwa wahanga wakubwa wa siasa za himaya hii lakini wao wameendelea kuwa imara sana wakishikilia tamaduni zao na asili yao na utambulisho wao bila kutetereka.

-Zikaja himaya mbalimbali za Ulaya na maeneo mengine, ambazo zimekuwa na nguvu, umaarufu, umashuhuri na ushawishi mkubwa sana duniani lakini zinasimama na kudhoofika mara kwa mara lakini Wayahudi wameendelea kuwepo wakiwa wenye nguvu na ari ya mapambano mpaka leo bila kuchoka kama kawaida yao. Vitu vingi na himaya nyingi zimeanza na kuanguka lakini Wayahudi wameendelea kuwepo, nini siri ya mafanikio yao?

Mwanasaikolojia mashuhuri wa Marekani David McClelland ambaye alifanya utafiti mwingi juu ya msukumo au hitaji anasema msukumo wa aina hii wa mtu unatoka kwenye tamaduni, mila na desturi za jamii yake. David McClelland aliiainisha misukumo hii kama hitaji la mtu kuwa na mafanikio, hitaji la kuwa sehemu muhimu ya jamii na hitaji la kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi na ushawishi katika jamii yake.

-Wayahudi wana msukumo mkubwa wa kuendelea kuwa bora kila siku bila kujali mambo ni mazuri au mabaya kiasi gani.

-Wazazi wa kiyahudi wameweka matarajio makubwa sana kwa watoto wao na wanawapa changamoto mbalimbali kuwajenga na hivyo watoto wanakuwa kama na deni la kumlipa mzazi kwa kumdhihirishia kwamba ana uwezo wa kufikia lengo ambalo mzazi wake anatarajia mtoto afikie au hata zaidi. Wazazi wa kiyahudi huwa na shauku na hamu kubwa ya kumuona mtoto akipata elimu bora na kisha kuwa na mafanikio makubwa katika Ulimwengu wa kazi na biashara.

-Wayahudi wengi huona ubora na umuhimu wao uko kwenye mafanikio yao katika ulimwengu wa kazi na biashara, hivyo huweka bidii kubwa upande huo.

-Katika taasisi na mashirika mengi kumeendelea kuwa na namna kadhaa za kuwahujumu wayahudi kupanda katika nafasi za juu za vyeo, hilo limekuwa msukumo mkubwa kwa wayahudi kuendelea kuweka nguvu na juhudi kubwa zaidi kusonga mbele.

-Katika fani na kazi ambazo zina hatari kubwa na zinazohitaji mabadiliko mengi ya haraka zimevutia zaidi wayahudi kuingia na kufikia viwango vya juu vya mafanikio huku watu wengi wakiziogopa.

-Kwa sababu hizi hizi wayahudi wameweza kubuni na kuboresha vitu vingi sana ambavyo vimewakuza na kuwaongezea ubora, umaarufu na utajiiri.

MAMBO AMBAYO WACHAGGA TUNAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA KWA WAYAHUDI.

-Sisi kama wachagga tunatakiwa kupenda na kukumbatia asili na utambulisho wetu pamoja na tamaduni mila na desturi zetu, kuziboresha na kuzitunza na kuzienzi ambazo kimsingi ndizo zilizoweza kutujenga na kutufikisha hapa na kutufanya tuwe hivi tulivyo, hatupaswi kudanganywa na mtu mwingine vinginevyo.

-Kuna wachagga wengi wamefanya na wanaendelea kufanya mambo mengi makubwa kwenye nchi hii na kwingineko duniani, hayo yakiwa ni matunda ya tamaduni, mila na desturi zilizotulea na kutukuza ambazo hatutakiwi kuthubutu kuziacha zikapotea.

Tunapaswa kukumbatia tamaduni na asili yetu pamoja na utambulisho wetu na kujivunia ili kutusukuma kuelekea kufanikisha mambo mazito na makubwa zaidi. Pia tuna jukumu la kuwajengea mtazamo sahihi watoto wetu kwa kutumia mafanikio ya nyuma ya watu wa jamii yetu pamoja na mapambano mazito yanayoendelea miongoni mwetu iwe chachu ya maendeleo na msukumo kwa wao kufanya vizuri zaidi pamoja na kutunza na kuenzi tamaduni hizi bora zilizotufikisha katika mafanikio zaidi.

-Tuna mifano ya wachagga waliofanya mambo makubwa na wengi wakijitahidi katika mapambano zaidi kuelekea kufanya makubwa sana, ambao tunaweza kuwaangalia kama wenzetu wakatupa msukumo na ari ya kuweka malengo makubwa na kuyafikia. Kuna shirika la ndege kama la Precision Air ambalo ni shirika binafsi la usafiri wa angani linalofanya vizuri sana licha ya ushindani mkubwa uliopo na serikali ambalo limeanzishwa na linamilikiwa mtu binafsi ambaye ni mchagga kama sisi. Hii ni hatua kubwa ya kimaendeleo kufanywa na mtu binafsi kwa nchi kama hii. Kuna mabenki makubwa kama Akiba na mengineyo, ambayo yameanzishwa au kuendelezwa na watu binafsi wachagga, samabamba na makampuni mengine mengi makubwa mbalimbali na yanayofanya vizuri sana katika soko. Yote haya ni matunda ya tamaduni na desturi zilizotulea ambazo tunapaswa kuziboresha na kuziendeleza.

-Ukisoma kitabu cha Dr. Reginald Mengi, “I can, I must and I will”, ameeleza vizuri na utaweza kuona ni jinsi gani misingi iliyojengwa na wazee wetu waliotutangulia sambamba na tamaduni zilizomlea na kumkuza zimeweza kumsaidia kufanikisha kufikia mafanikio makubwa sana aliyofikia. Kuanza kutokea chini kabisa kimaisha na kufikia kiwango cha ubilionea katika nchi kama hii ni hatua kubwa sana kimaisha inayostahili pongezi kubwa.

-Weka malengo ya muda mrefu. Fikiria kuhusu maisha yako na kile unachotaka kufanikisha. Kwanza andika vitu vitatu unavyovipenda au kuvithamini sana. Kisha andika malengo yako ya miezi sita, mwaka mmoja, miaka mitano na miaka kumi huku ukifikiria vile vitu unavyothamini sana. Malengo unayojiwekea yanatakiwa kuwa makubwa kwa mfano kulima heka 100 za mazao fulani, kuandika kitabu kitakachoauza sana, kujenga jengo refu la ghorofa eneo fulani la mjini n.k.,. Kisha andika mambo matatu unayotakiwa kufanya ili kufanikisha hili. Kama unaona huwezi usiogope andika chini lengo lako kisha tafuta mtu ambaye ameshafanikiwa sana katika hilo unalolenga na umwombe awe mshauri wako kuelekea huko unakotaka kufika, ukipata watu 10 ukawaomba hutakosa mmoja au zaidi atakayekubali kuwa mshauri wako.

-Weka bidii na malengo kwenye kazi za kutumia akili zaidi, ukumbuke kwamba utajiri ni zao la akili na sio mikono. Kuweza kufanikisha mambo mengi na makubwa unatakiwa kutumia akili sana na itakuchukua miaka kadhaa, sio chini ya miaka 7 mpaka 10 au zaidi kama ukiweka bidii sana, usijidanganye kabisa kwamba unaweza kufanikisha jambo lolote lile la maana ndani ya miaka miwili, mitatu au hata mitano, hiyo ni miaka michache sana.

Utalazimika pia kufanya kazi na watu kwa hiyo ni lazima uboreshe sana mahusiano yako na watu wengine. Fundisha wengine, kuwa mtu wa mipango, mtu wa mbinu, kuwa kiongozi. Okoa nguvu na muda wako kwa kufanya vitu muhimu na vingine fanya zaidi na watu huku wewe ukiwa kiongozi.

-Usiogope kuchukua hatari zenye manufaa(risks), hata hivyo fanya kwa uangalifu lakini usiwe mwoga, uoga ni kitu cha hovyo sana, tutajifunza faida za ujasiri kupitia historia za wachagga. Jifunze mambo mengi sana, jifunze kila siku, hakikisha kila siku unasoma angalau kurasa tano za kitabu, kila siku bila kukosa.

-Jitahidi kufanya kitu kitakachokupa mafanikio ya kiuchumi na ushawishi kwenye jamii, ambacho unakipenda sana pia, ukifanya kazi kwa ajili ya fedha peke yake ni rahisi kuchoka na kupoteza ari baada ya kupata mafanikio kidogo.

-Chukua hatamu ya maisha yako na ona kwamba una jukumu la kufanya kitu na kulifanikisha wewe peke yako.

-Kuwa na ma-role models unaowaangalia wanakuongezea ari na shauku ya kujituma zaidi, soma hadithi za mafanikio za watu waliofanya makubwa katika maisha na wenye mafanikio sana. Vizuri zaidi ukisoma hadithi za mafanikio za watu wa nyumbani ambao tumetokea eneo moja, zinakuwa na nguvu na kukuongezea ujasiri zaidi kuliko watu wa mbali. Uzuri ni kwamba wachagga tuna hadithi nyingi sana za mafanikio za watu wa maeneo tunayotokea, unapaswa kupanga kufanya vizuri zaidi kuwazidi wote unaowafahamu.

-Weka imani katika mipango yako na malengo yako, fanya vitu vya tofauti, jichanganye na watu tofauti hasa zaidi watu wenye mafanikio. Fanya kuomba ushauri kwa watu wenye mafanikio, usiogope kukutana na watu mbalimbali waliopiga hatua kwa ajili ya ushauri na hata urafiki pia, hao kuna mambo mengi usiyojua ambayo wao wanafahamu ila hawana muda wa kukwambia. Puuza imani za kishirikina, pamoja na mambo mabaya unayosikia kuhusu watu wenye mafanikio, nyingi ni uongo wa kutunga unaosambazwa na watu wenye wivu tu, usitilie maanani sana.

-Mwisho na muhimu zaidi tunahimiza sana kurudi kwenye tamaduni na njia zetu za maisha tulizorithi kutoka kwa wazee wetu kwa sababu licha ya kwamba hakuna msisitizo mkubwa uliyowekwa lakini ile asili imetusaidia kuonekana wa tofauti kidogo angalau katika mazingira ya nchi hii. Hiyo inamaana kwamba tuna uwezo mkubwa wa kufanikiwa hata mara kumi au zaidi kama tukiweka msisitizo na kuhimizana sana.

Mwanafalsafa wa karne ya 19 wa Marekani ambaye pia anatambulika kama baba wa falsafa ya Marekani(father of American Phisolophy), Ralph Waldo Emerson aliwahi kusema “Wewe ni gari iliyoendeshwa na mababu zako wote waliopita”, akimaanisha kwamba wewe ulivyo ni mwendelezo wa wazee wako, na hili kibaiolojia halipingiki lakini hata kisaikolojia ni hivyo hivyo, asije mtu mwingine akakuaminisha vinginevyo.

Ukisoma vitabu vingi sana alivyoandika mwanafalsafa, mwanahistoria na mmsionari kutoka Ujerumani Dr. Bruno Guttman kuhusu asili na mambo yote ya kijamii kuhusu wachagga utaweza kuelewa kwa usahihi sana kauli hii ya mwanafalsafa Ralph Waldo Emerson.

Ahsanteni

Tumefika Mwisho wa Uchambuzi Huu wa Kitabu Cha “THE JEWISH PHENOMENON”. Ya Kujifunza, Tujifunze na Tufanyie Kazi.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *