HADITHI YA WACHAGGA INAYOTOA MAONYO JUU YA MTU KUKOSA SHUKRAN KWA MATENDO MEMA ALIYOFANYIWA NA WENGINE.

Wachagga wa miaka ya zamani za kale walifahamu kwamba mtu anapofariki huenda kwenye dunia ya rohoni. Kisha mtu hubaki kwenye dunia hii ya roho mpaka pale anapofikia kuwa roho kweli. Lakini hukaa tena kwenye dunia hii ya rohoni mpaka anazeeka kisha anakwenda kwenye dunia nyingine ya ngazi ya pili ya roho ya watu waliofariki miaka ya zamani zaidi na ambao ni maskini zaidi.

Kisha baada ya kuishi kwenye dunia ya ngazi ya pili ya rohoni kwa muda mrefu zaidi mpaka kuzee huenda tena kwenye dunia ya tatu ya rohoni. Dunia hii ya ngazi ya tatu ya rohoni ni maskini zaidi na ina watu waliofariki miaka ya zamani sana ambao wanakaribia kupotea kabisa. Baada ya hapa mtu huweza kupotea kabisa na sio rahisi kurudi tena. Hivyo ndivyo wachagga wa zamani za kale walikuwa wakiamini.

Lakini wakati mwingine kuna baadhi ya hali zilizoweza kupelekea Ruwa/Iruwa kuamuru kwamba mtu arudi kuwa hai tena duniani. Hivyo kuna baadhi ya matukio ambayo yaliaminiwa na wachagga na kuaminiwa kwamba yalikuwa ni maamuzi ya Ruwa.

Hapo zamani za kale katika nchi ya wachagga kulikuwa na Bwana mmoja aliyekuwa na ndege nyumbani anayejua kucheza dansi kwa umaridadi kama mtu. Jina la ndege huyu aliitwa Kitowole. Huyu Bwana alikuwa anamtunza ndege huyu ndani ya chungu, na kila alipotamani kupata burudani ya ndege huyu kucheza dansi akimuangalia, basi alimtoa kwenye chungu atoe burudani kisha alimrudisha tena katika chungu alipomaliza.

Bwana huyu alikuwa tajiri sana, pia alikuwa na watoto wawili wa kike. Binti mmoja alikuwa ni mtoto wake wa kumzaa na huyo binti mwingine alikuwa ni binti anayemlea lakini sio wa kumzaa. Siku moja asubuhi binti yake huyu wa kumzaa alimtoa ndege Kitowole katika chungu kile na kuanza kucheza naye. Ghafla moja yule ndege Kitowole alipeperuka na kukimbia. Huyu binti mwingine asiye wa kumzaa aliongea kwa sauti akimlaumu mwenzake kwamba amempoteza Kitowole.

Baba yao aliposikia hayo alikasirika sana. Alitoka nje na sime kwa hasira na kumkatakata binti yake vipande vitatu na mtoto wake kufariki hapo hapo. Mama yake na binti alihuzunika na kuomboleza sana, kwa sababu ndiye alikuwa mtoto wake wa pekee. Mama yake alimlilia Ruwa kwa kupoteza mtoto wake ambaye aliuawa na baba yake mwenyewe.

Usiku wake mama yake na binti huyu alimuona mtu mweupe katika ndoto. Mtu huyu aliyemuona katika ndoto alimwambia; “Tulia, tulia mtoto wake atarudi tena. Lakini atakaporudi atatakiwa kukaa ndani ya nyumba kila siku; atakapotoka nje ya nyumba atafariki tena.” Siku iliyofuata Ruwa alimtuma kunguru mkubwa ambaye alikusanya vile vipande vitatu vya mwili wa mtoto yule na kuondoka navyo mpaka kwenye pango. Kisha alichukua unyoya wake mkubwa alioutumia kushoneshea vile vipande vitatu vya mwili wa yule binti pamoja. Kisha yule mtoto alirudi upya na kuwa hai na moja kwa moja alianza kuongea kama alivyokuwa mwanzo.

Sasa ilikuwa ni kazi ya yule kunguru mkubwa kila siku kwenda kutafuta chakula kwa ajili ya mtoto huyu aliyekuwa ndani ya pango alikompeleka, kwa sababu kunguru alimchukulia yule mtoto sasa kama ni binti yake. Siku moja wakati mama wa yule binti ameenda shambani kukata majani ya ng’ombe alimuona yule kunguru mara kwa mara akipeleka chakula kwenye pango. Aliendelea kumwangalia na zoezi hili lilikuwa likijirudia.

Basi mama wa yule binti akiwa shambani alisubiri mpaka yule kunguru alipoondoka kisha aliingia ndani ya lile pango. Alishangaa kumuona binti yake akiwa hai tena ndani ya pango lile. Mama yule alimchukua yule mtoto wake kwenye lile pango na kumpeleka kwa mume wake na kumweleza kila kitu, akamweleza mpaka kuhusu ile ndoto aliyoota usiku.

Mama yake alimweka binti yake ndani ya nyumba na kumpa maelekezo yote ya kuhusu yeye kutotoka kabisa nje ya nyumba akimwambia; Mwanangu, unapaswa kubaki hapa kila siku. Usijaribu kwenda nje wakati wowote ule. Siku utakayotoka nje utakufa.”Yule kunguru alivyorudi na chakula kwenye lile pango hakumkuta yule mtoto. Alikasirika sana na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa mama yake na yule binti. Kunguru yule alikaa juu ya mti uliokuwepo pale nje ya nyumba yao na kulia kwa sauti kubwa sana, akihitaji kurudishiwa mtoto wake, au kama sio hivyo basi alipwe fidia ya kazi aliyofanya ya kumrudishia uhai na kumtunza mtoto huyo.

Baba na mama wa binti yule hawakukubaliana na jambo hilo na hivyo wakaamua kumpuuza kunguru yule. Lakini kunguru yule hakuondoka kabisa pale aliendelea kukaa juu ya mti ule na kuendelea kulia na kudai mtoto wake au fidia. Kunguru yule alipohisi njaa aliondoka kwenda kutafuta chakula kisha alirudi juu ya mti ule pale nje ya nyumba yao. Alienda kufanya hivyo kila siku, miaka kwa miaka. Lakini binti yule hakuwahi kutoa nje kabisa kwani alizingatia amri aliyopewa na mama yake.

Siku moja baba na mama yake binti yule walienda porini kule kwenye tambarare. Kisha siku hiyo mvua kubwa sana ilinyesha wakati wako mbali na nyumbani huko shambani porini. Sasa binti yule aliyekuwa ndani ya nyumba, alipoona kwamba mvua kubwa iliyokuwa inanyesha inaharibu nafaka za baba yake kama ulezi, mtama na mahindi vilivyokuwa vimeanikwa nje alisikitika sana, kwa sababu hakukuwa na mtu mwingine yeyote nyumbani wa kuvianua na kurudisha ndani.

Hivyo binti yule alishindwa kuvumilia akajifunika vizuri mwili wake na kutoka nje ili kukusanya na kurudisha ndani. Yule binti alipoanza tu kutoka nje, yule kunguru pale juu ya mti alishuka chini mara moja alipokuwa yule binti, kisha akalikamata lile nyoya alilokuwa amelitumia kushonoshea mwili wa yule binti ili kuurudishia pamoja, na kulichomoa kutoka kwenye mwili wa yule binti na kuondoka zake.

Hapo hapo yule binti alianguka chini kisha akagawanyika katika vipande vitatu kama mwanzoni na kufariki. Mvua na upepo vikasukuma vipande vile vya mwili wa yule binti mpaka shambani mgombani. Wazazi wake waliporudi walikuta vipande vile vya mwili wa binti yao katikati ya migomba, na mtoto wao akiwa amefariki. Na kunguru yule aliyekuwa juu ya mti pale nje ya nyumba yao, akiwa ameondoka zake na nyoya lake. Baba na mama wa binti yule walilia sana na kuomboleza sana.

Tangu siku hiyo katika nchi ya wachagga watu wamekuwa wakisema; “Kumbuka kurudisha shukran kwa mtu yeyote aliyekufanyia mambo mema.”

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *