TAASISI YA UMANGI.

KAZI ZAKE, UMUHIMU WAKE NA MABADILIKO YAKE.

– Kila kitu duniani kinachohusiana na watu au kuathiri maisha ya watu wa jamii kwa namna moja au nyingine huwa kinatoka kwenye asili ya binadamu. Mifumo ya kijamii kwa ujumla wake hutoka kwenye asili ya binadamu ikilenga kutatua changamoto fulani au kuboresha maisha ya watu wa jamii hiyo kwa namna mbalimbali japo mara nyingine sio rahisi kuonekana dhahiri kwa mtu asiyefikiri kwa kina.

– Uwepo wa mifumo ya kijamii ya utawala na uimara wake ni moja kati ya dalili zinazoonyesha kwamba jamii husika imepiga hatua kimaendeleo kwani mifumo bora na uimara wake ni moja kati ya zana muhimu sana katika kusukuma mbele maendeleo ya jamii husika. Huwa ni vigumu sana kwa jamii ya watu kusonga mbele bila kuwepo kwa mamlaka fulani inayoheshimika, kuaminika na kutegemewa ambayo ndio inaamrisha na kusukuma mbele agenda mbalimbali za kuifanya jamii husika kufanikisha mambo mbalimbali muhimu kwa jamii hiyo.

– Mamlaka hizi zinaweza kuwa ni za kidunia au za kiroho au mchanganyiko wa vyote viwili ambapo kwa kutumia mbinu mbalimbali hususan heshima na ukuu wa mamlaka hiyo huweza kuamrisha mambo mbalimbali kufanyika kwa faida ya watu wa jamii nzima. Kwa zile jamii zisizokuwa na mamlaka hizi huweza kuchelewa sana kupiga hatua au kuwa jamii zilizorudi nyuma na zisizo na mwelekeo unaoeleweka kwani binadamu walio wengi sio wazuri wa kujiamulia na kujiongoza wenyewe katika njia sahihi zaidi ya kutumbukia kwenye mambo yanayopelekea kuwaangamiza binafsi.

– Nchi ya wachagga(Chaggaland) ni moja kati ya jamii zilizoweza kufanikiwa sana katika eneo hili kutoka kwenye asili katika kutengeneza mamlaka zilizoweza kuwa na nguvu kubwa ya kusukuma mbele agenda nyingi zilizokuwa na maslahi kwa jamii yote licha ya changamoto mbalimbali zilizoambatana na mamlaka hizo na agenda hizo pia. Kwa nchi ya wachagga kitovu kikuu cha mamlaka hayo ni taasisi ya umangi.

– Taasisi ya umangi ilipata nguvu ya kuheshimika na kuaminiwa na watu kwa kuchanganya nguvu zote mbili za kimamlaka kuanzia ile ya kidunia mpaka ile ya kiroho. Mbinu za kidunia zilikuwa ni kama vile kutumia adhabu, vitisho, zawadi n.k., katika kujenga nidhamu kwa wachagga. Wakati mbinu za kiroho ni ule umuhimu wa taasisi ya umangi katika dini ya wachagga ambapo Mangi mwenyewe alikuwa ni kama Kuhani ndani ya dini hiyo hivyo kuwa na mamlaka ya kiroho yaliyompa kuheshimiwa zaidi, kusikilizwa, kuaminiwa na neno lake kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.

– Wachagga walikuwa na katiba imara sana kisiasa ambayo kituvo chake kilikuwa ni taasisi ya umangi. Uimara huo ulitokana na uzalendo mkubwa ambao wachagga wenyewe walikuwa wameuweka kwenye taasisi hiyo ya umangi. Mangi alikuwa ndiye mkuu wa taasisi hiyo na mtu mwenye mamlaka ya mwisho katika taasisi hiyo iliyokuwa na ushawishi mkubwa katika himaya zote za nchi ya wachagga.

– Lakini pamoja na ushawishi mkubwa sana aliokuwa na Mangi kwenye taasisi hii ya umangi iliyoheshimiwa sana na wachagga uchaggani kote bado yeye mwenyewe aliheshimu sana nafasi waliyokuwa nayo wachili wake(wazee wa nchi) au mawaziri na watu matajiri. Hivyo wachili na watu matajiri pia walikuwa na ushawishi mkubwa ambao hata Mangi mwenye nguvu kiasi gani hakuweza kupuuza au kubeza nafasi yao ndani ya nchi. Hii ni licha ya kwamba Mangi mwenyewe ndiye alichagua wachili wake kutoka kwenye koo kongwe na zilizojijengea heshima kubwa ndani ya nchi.

– Hata hivyo pamoja na nguvu kubwa ya ushawishi waliokuwa nayo wachili na watu matajiri bado haikuwa rahisi kufanya mapinduzi kupindua utawala wa Mangi kutokana na uimara wa taasisi yenyewe kama tulivyoeleza hapo juu na kosa la uhaini(kupindua serikali) lilipewa adhabu ya kifo moja kwa moja. Mangi alikuwa na mtandao wa askari na mashushushu ambao wengi walikuwa ni vijana majasiri na waliojenga uzalendo mkubwa sana kwake kwa maisha yao yote ambao walikuwa na kazi ya kumlinda dhidi ya maadui wote wa ndani na nje ya nchi.

– Tofauti na dhana inayoweza kuwa ndani ya akili za watu wengi, utawala wa umangi haukuwa wa kidikteta zaidi ulikuwa katika nafasi ya kulea na kuilinda jamii. Hili linaongezewa nguvu na ukweli kwamba nyumbani kwa Mangi kulikuwa wazi wakati wote kwa watu wote mpaka wale wa chini kabisa kuingia na kutoka kadiri walivyokuwa na agenda au matatizo waliyohitaji kutatuliwa au kuamuliwa na Mangi. Wachagga pia walienda mara kwa mara nyumbani kwa Mangi kwa ajili ya kusherehekea na shughuli nyingine zenye umuhimu mkubwa kijamii.

– Mangi alikuwa ndiye Hakimu mkuu wa nchi na Kuhani katika dini ya wachagga. Hivyo kesi mbalimbali zilizokuwa zinatokea miongoni mwa watu katika nchi ya wachagga zilikuwa zinafikishwa kwenye mahakama ya Mangi kwa ajili ya kutolewa hukumu na Mangi. Kesi nyingi zilizokuwa zinatokea ndani ya nchi ya wachagga zilihitaji uwezo mkubwa na busara ya hali ya juu katika kufanya maamuzi na kutoa hukumu iliyozingatia haki na usawa, uwezo ambao wachagga waliamini alikuwa nao Mangi ambaye waliamini katika maamuzi yake na hivyo kujenga ushawishi mkubwa kwao.

– Hivyo wachagga walipeleka kesi zao kwenye mahakama ya Mangi ambaye alikuwa na maamuzi ya mwisho juu ya kesi hizo na wachagga walimuona kama ni hazina ya haki na usawa. Mangi mwenyewe ndiye aliweza kutatua mgogoro wowote uliokuwa unaendelea kati ya watu au pande mbalimbali na alitoka hukumu na kila mtu aliheshimu maamuzi yake. Watu walipokuwa na mgogoro walijua kwamba Mangi atatumia mbinu nyingi kuhakikisha kwamba hukumu anayotoa imezingatia kila kitu na kuwa sahihi zaidi na inayostahili hivyo watu walijitahidi kujiridhisha sana kabla hawajapeleka kesi kwa Mangi.

– Wachagga walishangilia maamuzi ya Mangi katika kutoa hukumu mbalimbali kwa sababu waliamini kwamba maamuzi yake ndio msingi wa amani na utulivu katika nchi. Waliamini kwamba Mangi anaondoa mpasuko na kuiunganisha nchi na kuleta umoja na mshikamano katika nchi kupitia maamuzi yake ambayo waliamini ni ya haki.

– Mangi pia ndiye aliyekuwa kwenye mamlaka ya kutekeleza mambo yaliyokuwa yanaiathiri nchi nzima kidunia na hata kiroho. Kwa mfano kutoa sadaka kwa ajili ya kuiponya nchi nzima juu ya janga baya lililoikumba au kuondoa mnyama mkali anayepoteza maisha ya watu. Mangi alikuwa ndiye anatoa amri ya kutangaza jambo lolote la kiroho/kidini lililokuwa linapaswa kutekelezwa katika nchi, kwa mfano watu kutakiwa kutofanya kazi kutokana na tukio fulani la kiroho linalotakiwa kufanyika au sherehe fulani yenye umuhimu mkubwa kimila.

– Mtu yeyote mwenye changamoto kubwa au mwenye kuhitaji msaada na huruma ya Mangi alienda kwa Mangi na kushinikiza kutatuliwa changamoto yake ambapo Mangi mara nyingi alilazimika kufanya hivyo hata kwa kumuonea huruma kwani kupitia imani ya kichagga watu pia walikuwa na nguvu ya kumwachia laana Mangi ambayo itampata ikiwa atawapuuza wakiwa kwenye uhitaji wa kufa na kupona. Hivyo Mangi kutokana pia na kuogopa laana hiyo anayoweza kuachiwa na watu wake walioenda kumlilia itakayoweza kumletea shida mbeleni alijikuta analazimika kuwasikiliza na kuwajibika kwa matatizo yao.

– Wachagga waliamini kwamba ni jambo kubwa na la kujivunia na hatua kubwa kijamii kwa kuwa na mtawala kwani jamii kama ya Wandorobo ambao hawakuwa na taasisi ya utawala ilionekana kuwa ni jamii ya hovyo na isiyo na mwelekeo. Wandorobo walichekwa na kusanifiwa sana na wachagga kwani hata zile shughuli za kuimarisha na jamii na kuiboresha kama vile kujenga miundombinu ya barabara, mifumo ya umwagiliaji na shughuli nyingine muhimu za maendeleo kama zilivyokuwa zinafanyika uchaggani hazikuwa zinafanyika kwao. Kwa kifupi ni kwamba jamii isiyo na mamlaka inayoiongoza ilikuwa ni jamii isiyo na mwelekeo.

– Hivyo wachagga walijivunia kuwa na Mangi na walikuwa na nyimbo nyingi za kizalendo za kumsifu na kumtukuza Mangi kwa kazi kubwa aliyokuwa anaifanya kwa ajili ya nchi yake na nafasi yake katika kuilinda nchi.

– Hata hivyo kwa asili kitu chochote chenye faida au upande chanya hakikosa upande hasi hususan kitu chenye faida kubwa kama ya kuleta utulivu na amani wa eneo fulani huambatana na changamoto zake. Kwa sababu Mangi alikuwa ni mtu kama watu wengine pia tabia zake binafsi ziliweza kuathiri matendo yake yaliyosababisha mambo mema na mazuri kwa watu wake. Kama Mangi alikuwa ni mpole na mkarimu watu wake waliweza kunufaika na kama alikuwa ni jeuri na katili watu wake pia waliathirika. Kuna baadhi ya wamangi waliokuwa na nguvu sana lakini walisifika kwa kuwa na uungwana kama vile Mangi Horombo na Mangi Rindi Mandara na wengine kusifika kwa ukatili uliokithiri kama vile Mangi Ndesserua.

– Lakini kwa bahati mbaya sana kuna dhana nyingi potofu zimekuzwa sana na kuchochewa zaidi kwa upande wa hasi wa watawala hawa au taasisi hii ya umangi na kupuuza misingi yote imara iliyojengwa kupitia wao na kutuimarisha sana mpaka tulivyo sasa. Dhana hizi nyingi potofu zimechochewa zaidi na watu waliokuwa wanalenga kupaka matope taswira nzima ya jamii ya wachagga na kujaribu kusahaulisha kizazi cha sasa misingi yote imara iliyowajenga wachagga walivyo sasa na umuhimu wake. Hii ikiwa ni njia kuu ya kuwadhoofisha wachagga na kuhakikisha kwamba wanajidharau na kuamini kwamba wao wametokea kwenye ujinga na uovu na kwamba sio lolote wala chochote, kitu ambacho kinaathiri sana kujiamini kwao(self esteem) katika kutaka kufanya makubwa kwenye maisha.

– Lakini licha ya propaganda potofu nyingi zilizojengwa juu ya taasisi ya umangi zinazolenga kuwabomoa wachagga kwa ujumla na kuwapotezea kujiamini binafsi(self esteem) kwa kuweka msisitizo kwenye mambo hasi peke yake, ni muhimu kufahamu mambo mengi chanya yaliyotokana na taasisi hiyo muhimu iliyowafanya wachagga wafike hapo walipofika leo.

– Wamangi katika kipindi cha utawala wa serikali za wazungu walihimiza watu kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia ushawishi wao kwa watu uliopelekea wachagga kupata maendeleo makubwa ambayo hayajwahi kupatikana hapo kabla na hata baada. Jambo hili halikuwa rahisi kwa zile jamii ambazo hazikuwa hazikuwa na taasisi yenye mamlaka au kuwa na taasisi imara.

– Wamangi ndio waliwakaribisha viongozi wa dini, kuwapa ardhi na kuwahimiza kujenga taasisi za kimaendeleo ambazo zimeweza kuisaidia Kilimanjaro kupita hatua kwa namna nyingi sana.

– Wamangi walichangia kupunguza sana uhasama na mauaji katika nchi ya wachagga kwani vita baina ya koo zilikuwa ni kubwa sana na zilizopelekea mauaji makubwa sana. Mtu wa ukoo mmoja alipouawa ukoo mwingine ulilipa kisasi kwa kuua mtu wa ukoo huo kisha maujai yaliendleea hivyo moaka kuwa vita kubwa ya kupoteza kupoteza utulivu kwani ilishia kuwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu kulikuwa na mwingiliano mkuwa sana wa koo hizi. Lakini utawala wa Mangi uliamuru kwamba damu ya mtu haitalipwa kwa damu ya mtu mwingine bali kwa faini ya mali na hivyo kupelekea mauaji ya hovyo na holela kutoweka.

– Licha ya kuleta haki, amani na utulivu katika nchi ya wachagga taasisi ya umangi pia ilichochea maendeleo sana kwa kuhimiza ujenzi wa miundombinu ambayo ilikuwa na manufaa makubwa kwa wachagga ikiwemo kuondoa njaa katika nchi ya wachagga.

– Taasisi ya umangi ilikuwa inakusanya kodi kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kuiimarisha taasisi yenyewe na kuweza kuendesha shughuli nyingine nyingi za kijamii. Hata hivyo kuna dhana potofu iliyoenezwa kwamba taasisi hiyo ilikuwa inafanya dhulma kwa kukusanya kodi. Inawezekana kwamba kwa maoni yao kodi hiyo ilikuwa haitumiki vizuri kama jinsi ilivyo kwa kodi nyingi mpaka leo hii duniani kuaminika kwamba zinatumiwa hovyo na watawala lakini bado ile itabaki kuwa ni kodi na sio dhulma kama jinsi wale waliolenga kutaka kubomoa taswira ya Uchagga wanavyotaka kuwaaminisha watu.

– Lakini tuna mfano hao katika nchi ya wachagga miaka ya zamani sana, vile tulivyoona katika nchi ya Mshiri huko Marangu katika miaka ya 1600 wakati wa utawala wa Mangi Mtui. Mangi Mtui alikuwa mtawala wa nchi ya Mshiri huko Marangu baada ya utawala wa baba yake Mangi Kilaweso. Mangi Kilaweso alikuwa ndiye mtawala wa mwanzoni zaidi anayefahamika kutoka kodi kwa ajili ya kuilinda nchi na kuleta amani na utulivu. Lakini wakati wa utawala wa mtoto wake Mangi Mtui watu waligoma kulipa kodi na hivyo taasisi ile kudhoofika na kufa. Kilichofuata baad aya hapo ni fujo, vita na unyang’anyi mkubwa ulitokea katika nchi ya Mshiri na hapo watu walilazimika kumwomba Mangi Mtui arudi katika kiti cha utawala ili kurudisha hali ya utulivu na amani katika nchi.

– Na hapo ndipo watu walitakiwa kulipa kodi kubwa zaidi ya ile ya mwanzo ili kumshawishi Mangi Mtui kurudi katika kiti cha utawala na kurudisha hali ya amani na utulivu. Hivyo suala la kodi sio suala la kubeza au kuiita kodi ni dhulma kama jinsi wale wanaojaribu kuibomoa taswira ya utawala wa Uchagga wanavyojaribu kuwaaminisha watu. Bali kodi ni gharama ambayo mtu unalipa ili kukaa kwenye jamii yenye utulivu na amani. Kama kuna hoja yoyote juu ya kodi basi inapaswa ilenge kwenye matumizi yake lakini sio kuiita kodi ya Mangi kwa ni dhulma, hiyo ni dhana potofu iliyotengenezwa na watu wenye wivu na chuki waliolenga kubomoa taswira ya utawala wa uchagga kwa lengo la kuwabomoa kabisa wachagga.

– Lakini hata hivyo taasisi ya umangi haikuendelea kubaki vile vile ilivyokuwa miaka 500 iliyopita bali iliendelea kuja na mabadiliko mengi yaliyolenga kuiboresha zaidi. Kwenye historia tuliweza kuona kwamba kufikia karne ya 20 mambo mengi yalikuwa yamebadilika katika taasisi ya umangi, kwa mfano sheria zaidi ziliendelea kutungwa na hata kutengenezwa mfumo wa tofauti wa utawala wa umangi ulioongeza wawakilishi waliotokana na wananchi.

– Zilianzishwa taasisi za umangi mwitori ambazo zilikuwa na mamlaka ya juu zaidi ya Mangi wa maeneo na baadaye kuanzishwa kwa taasisi ya umangi Mkuu ambayo ilikuwa ndio taasisi ya juu yenye mamlaka makubwa kuliko zote. Nafasi za wawakilishi wa wananchi zisizotokana na Mangi kwa maeneo mengi zilianzishwa sambamba na uwakilishi katika tasisi ya umangi mwitori na umangi Mkuu. Pia mfumo wa mahakama zote kuanzia mahakama za maeneo, mahakama za waitori mpaka mahakama kuu ya wachagga ziliwekwa huru dhidi ya watwala na badala yake kuendeshwa na wanasheria badala ya watawala/wamangi. Yaani kufikia 1950’s mahakama kuu ya wachagga ilikuwa huru dhidi ya serikali ya Mangi Mkuu, hatua ambayo hata nchi ya Tanzania haijaweza kufikia mpaka leo.

Karibu kwa maoni, ushauri, maswali.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *