KUKUA NA KUANGUKA KWA HIMAYA ZA UCHAGGANI, KILIMANJARO KATIKA HISTORIA.

Kuna nyakati ambapo Uchaggani, Kilimanjaro kulikuwa na vihimaya vidogo vidogo sana, yaani kuna nyakati ambapo vijiji vya uchaggani vya leo hii zilikuwa ni nchi au himaya mpaka kwenye miaka ya 1600. Kwa mfano sehemu kama Kibosho vijiji vya Singa na Sungu zilikuwa ni himaya zinajitegemea, kijiji cha Mweka kilikuwa ni himaya inayojitegemea. Kijiji cha Tella, Mowo, Tsudunyi na Kidia, Old Moshi ni himaya zilizokuwa zinajitegemea zenye mtawala wake na sheria zao. Kijiji cha Mrumeni Kirua Vunjo ni himaya iliyokuwa inajitegemea bila kuingilia na utawala wa Kirua Vunjo. Kijiji cha Mshiri, Mmbahe, Samanga, Kyala na Sembeti, Marangu ni himaya zilizokuwa zinajitegemea zenye tawala tofauti.

Himaya hizi ndogo ndogo kadiri muda ulivyoendelea mbele ziliendelea kuungana kupitia njia mbalimbali na kutengeneza himaya kubwa zaidi ambazo ziliendelea kuungana mpaka kutengeneza himaya za umangi zilizopo sasa. Njia zilizotumika zilikuwa mara nyingi ni vita ambapo himaya iliyoshindwa iliichukuliwa na ile iliyoshinda na kuunganishwa kuwa himaya moja na kutawaliwa. Njia nyingine iliyotumika ni ya kidiplomasia au vitisho kuweza kuishawishi au kuilazimisha himaya moja kuwa chini ya nyingine kimamlaka ikiwa ni pamoja na ushawishi kwa kutumia mali au utajiri.

Himaya nyingi ndogo zilikuwa kubwa zaidi na zilikuwa zinaendelea kukua zaidi. Upande wa magharibi ya Kilimanjaro hususan Machame na Kibosho himaya zake zilikuwa ni kubwa zaidi huku upande wa mashariki kukiwa na himaya ndogo zaidi ukilinganisha na magharibi. Eneo la Rombo ndio lilikuwa na himaya kubwa chache na himaya nyingi sana ndogo ndogo sana mpaka kufikia mwishoni mwa karne ya 19 au miaka ya 1800. Himaya ndogo ndogo za Rombo zilizokuwepo mpaka karne ya 20 au miaka ya 1900 nyingine kwa sasa ni kati na nyingine ni vijiji ndani ya kati.

Kisha baadaye katika miaka ya 1700 ndipo zilianza kunyanyuka himaya kubwa zenye nguvu kubwa zaidi zilizotawala maeneo makubwa ya Kilimanjaro, yaani himaya zilizotawala himaya nyingine kubwa kufikia kutawala robo ya Kilimanjaro, nusu ya Kilimanjaro mpaka Kilimanjaro nzima.Himaya ya mwanzoni zaidi kujiimarisha kijeshi na kutawala eneo kubwa la Kilimanjaro inayojulikana ni himaya ya umangi Mamba. Himaya ya Mamba iliyopo upande wa mashariki wa Marangu tangu katikati ya miaka ya 1700 ilikuwa imeshajijenga kiasi cha kukaliwa himaya nyingi Kilimanjaro. Kuanzia kipindi cha utawala wa Mangi Marawite wa Mamba, himaya ya Mamba ilitawala kuanzia Marangu kuelekea upande mashariki mpaka maeneo ya Shimbi, Mkuu, Rombo. Baada ya Mangi Marawite kiti cha umangi wa Mamba kilikaliwa na mtoto wake aliyeitwa Mangi Mapfuluke ambaye alitawala kuanzia Kilema kuelekea upande wa mashariki wa Vunjo yote na nusu nzima ya Rombo. Mangi Mapfuluke pia alikuwa akiingilia pia kutawala upande wa magharibi wa Kilimanjaro katika himaya za Uru na Kibosho.

Baada ya Mangi Mapfuluke utawala ulipita kwa mtoto wake Mangi Ngawondo kisha akaja Mangi Mashina aliyekuwa mke wa Mangi Mapfuluke aliyetawala katika kipindi ambacho Mangi Rongoma na Kilema na Mangi Horombo wa Keni walikuwa wanajiimarisha kijeshi. Mangi Horombo wa Keni alijaribu kupambana na majeshi ya Mamba ili kuondoa ushawishi wao katika eneo la Rombo na vita hiyo ilikuwa ngumu mpaka walilazimika kuingia makubaliano ya amani na kuchanjia undugu wa damu. Hapo Mangi Horombo akabaki na eneo la Rombo huku Mangi Mashina akibakia Vunjo.

Ni wakati huu ambapo Mangi Rongoma wa Kilema alijaribu naye kupambana na Mangi Mashina wa Mamba bila mafanikio na mwisho akatumia mbinu za kumteka Mashina na hivyo kufanikiwa kuiangusha Mamba na kuitawala Vunjo yote. Mangi Horombo alikuja na majeshi yake kupambana na majeshi ya Mangi Rongoma ili kumwokoa mshirika wake Mangi Mashina lakini vita ilipigwa sana bila kupatikana mshindi na hivyo kuamua kuingia kwenye mkataba wa amani na hivi Mangi Rongoma akatawala eneo lote la Vunjo na Mangi Horombo kutawala eneo la Rombo katika miaka ya mwishoni ya 1700 au mwanzoni mwa 1800.

Haikuchukua muda mrefu na Mangi Rongoma alifariki na hapo ndipo Mangi Horombo aliivamia Vunjo yote akaiangusha na kuiweka chini ya utawala wake. Mangi Horombo akatawala nusu ya Kilimanjaro katika eneo la Rombo na Vunjo katika ya miaka ya mwanzoni ya 1800. Mangi Horombo alifanikiwa kufanya mambo makubwa sana akitawala kuanzia Kirua Vunjo mpaka Usseri, Rombo na kujenga ngome kubwa na imara sana katika maeneo ya Keni, Rombo na Mkuu, Rombo.

Wakati huo katika miaka ya mwanzoni ya 1800 upande wa magharibi wa Kilimanjaro Mangi Rengua wa Machame alikuwa amezishambulia himaya zilizokuwepo upande wa mashariki na kuziweka chini ya utawala wake. Mangi Rengua alitawala kuanzia magharibi Siha/Sanya mpaka mto Nanga huku upande wa pili kuanzia mto Nanga kuelekea mashariki mpaka Usseri, Rombo kukiwa chini ya utawala wa Mangi Horombo.

Baada ya Mangi Rengua wa Machame kiti cha utawala wa umangi wa Machame kilikaliwa na Mtoto wake aliyeitwa Mamkinga. Mangi Mamkinga alitawala eneo kubwa zaidi la Kilimanjaro mpaka maeneo ya Vunjo mpaka miaka ya katikati ya 1800. Baada ya utawala wa Mangi Mamkinga kiti cha umagi kilikaliwa na mtoto wake aliyeitwa Ndesserua ambaye alikuwa bado ana nguvu sana.Kisha katika miaka ya katikati ya karne ya 19 Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi akaanza kukua na kujiimarisha. Baada ya nguvu za Mamkinga wa Machame, Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi alijiimarisha na kutawala eneo lote la Vunjo na Rombo mpaka upande wake wa magharibi Mbokomu, Uru na Kibosho wakati wa utawala wa Mangi Lokila. Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi pia alifanya ushirika na upande wa magharibi katika himaya ya umangi Machame wakati wa utawala wa Mangi Ndesserua ambapo waliunganisha majeshi yote ya Kilimanjaro na kwenda kuvamia maeneo mengi ya nje ya Kilimanjaro kuanzia Upare, Usambara, Taveta na Ukamba upande wa nchi ya Kenya mpaka Serengeti na Loita katika maeneo ya nchi ya Kenya. Hivyo maeneo mengi ya Tanga na Taita upande wa Kenya yote yalishambuliwa na kudhibitiwa kutokea Kilimanjaro na majeshi ya washirika ya Mangi Rindi Mandara.

Baadaye Mangi Sina wa Kibosho aliimarika na kunyanyuka akafanikiwa kuiangusha na kuitawala Machame baada ya utawala wa Mangi Ndesserua na kisha kutawala upande wa magharibi mpaka Siha/Sanya Juu. Utawala wa Mangi Ndesserua uliidhoofisha Machame iliyokuwa na nguvu sana na hivyo kutoa mwanya wa Machame kuangushwa na kutawaliwa na Kibosho baada ya Mangi Ndesserua tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo Kibosho ilikuwa inaitawala Machame. Kuelekea mwishoni mwa karne ya 19 kulikuwa na ugomvi na vita kubwa kati ya majeshi washirika ya Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi na majeshi ya Mangi Sina wa Kibosho kugombea ukuu wa Kilimanjaro baada ya Mangi Sina kufanikiwa kuiangusha Machame na kuitawala.

Mwishoni mwa karne ya 19 wajerumani waliingia Kilimanjaro na kuiangusha Kibosho baada ya mapambano makubwa kati yao na majeshi ya Mangi Sina mwaka 1891. Mangi Sina alisalimu amri na kukubali kukaa chini ya utawala wa wajerumani. Huku Old Moshi Mangi Meli Mandara alikuwa ameingia madarakani baad aya baba yake Mangi Rindi Mandara kufariki na moja kwa moja alijikuta naye akiingia katika uhasama na mgogoro na wajerumani ambao aliona kama wanambana na aliwachukia sana.

Hivyo mwaka uliofuatia wa 1892 Mangi Meli Mandara naye alipigana vita na wajerumani ambapo mara ya kwanza alifanikiwa kuwashinda na kuwaondoa kabisa Kilimanjaro. Hivyo Mangi Meli Mandara akajitangaza kuwa ndiye Mangi Mkuu wa Kilimanjaro na kuwafukuza wajerumani wengine wamisionari waliokuwepo Kilimanjaro na hivyo kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi. Mwaka uliofuatia wa 1893 wajerumani walirudi tena kupambana na majeshi ya Mangi Meli Mandara Old Moshi na kumshinda vita na kumlazimisha kujasalimisha na kuwa chini ya utawala wa wajerumani kwa nguvu. Aliendelea na mivutano na mwisho alinyongwa mwaka 1900.

Kisha kuanzia mwaka 1893 Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu alifanikiwa kufanya ushirika na wajerumani hivyo akapata nguvu za kutosha kuidhibiti Vunjo na Rombo yote na baadaye wajerumani wakamtegemea kuwa mtoa maamuzi wa mambo yote ya utawala Kilimanjaro. Mangi Ndegoruo Marealle aliweza kutajirika sana hususan kupitia mali nyingi alizozipata eneo la Rombo na kidogo Vunjo na kujenga ushawishi mkubwa wa kisiasa. Lakini mwanzoni kabisa mwa karne ya 20 Mangi Ndegoruo Marealle aliingia katika mgogoro tena na wajerumani akituhumiwa kutaka kuwapindua na hivyo kupoteza ushawishi wake wote Kilimanjaro ambapo wajerumani hawakuwapenda watawala wenye nguvu.

Kuanzia miaka ya 1920’s waingereza waliingia kwenye utawala kuchukua nafasi ya wajerumani na katika Kilimanjaro walifanya ushirika na Mangi Abdiel Shangali wa Machame ambaye naye alipata nguvu kubwa na ushawishi mkubwa Kilimanjaro. Lakini mwishoni wachagga waliweza kuchagua Mangi Mkuu wa Kilimanjaro kwa njia za kidemokrasia na Thomas Marealle wa Marangu alishinda nafasi hiyo na hivyo nguvu kubwa zaidi ya ushawishi Kilimanjaro ikawa imehamia tena kwake.

Baada ya hapo ndipo ilikuwa mwisho wa nguvu za kisiasa Kilimanjaro kutoka kwa wenyeji baada ya kuanza kuletewa watawala kutoka maeneo mengine ya nje ya Kilimanjaro kupitia mfumo wa kisiasa uliokuja na serikali mpya. Kwenye historia kuna uchambuzi wa kina wa himaya zote 15 za umangi ndogo na kubwa na watawala wote waliokuwa mashuhuri na waliokuwa wa kawaida.

Karibu kwa maoni.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *