HADITHI ZA DINI YA ASILI YA WACHAGGA KABLA YA KUJA KWA WAMISIONARI WA KIKRISTO – 3

RUWA/IRUWA AINGAMIZA DUNIA.

Hapo zamani za kale watu waliendekeza uvivu na kutelekeza majukumu yao na kuwaagiza watu maskini na wanyonge kuwafanyia kazi zao. Kisha watu matajiri wakagoma kabisa kufanya kazi kwa namna yoyote ile. Walisubiri mpaka watu maskini na wenye uhitaji kuvuna mazao yao na mara baada ya kuvuna matajiri na wenye uwezo waliwapora kwa nguvu na kuyatumia.

Mambo haya yaliendelea kufanyika kila mwaka. Lakini mabinti za watu matajiri ndio walizidi kujivuna zaidi na kujiona fahari sana. Kazi yao kubwa kila siku ilikuwa ni kupiga ngoma na kucheza sana na kuwanyanyasa sana mabinti za watu maskini na wanyonge, sambamba na kuishi maisha ya kufanya uasherati na vijana wa matajiri wenzao.

Ruwa aliyaona haya na kukasirishwa sana. Alimtuma waziri wake aende kwa watu na kuwaambia: “Acheni njia zenu mbaya, fanyeni mema kama mlivyokuwa mnafanya mwanzo, au kama hamtafanya hivyo nitawaangamiza kabisa, nitawafuta kabisa kwenye uso wa dunia!” Lakini watu hawakusikiliza ushauri wala amri kutoka kwa mjumbe huyu aliyetumwa na Ruwa na badala yake walizidisha zaidi kufanya maovu.

Miaka hiyo alikuwepo binti mmoja mrembo aliyejaa ufahari mwingi. Binti huyu alijisemea kwamba hatamani kuchumbiwa na mwanaume yeyote wa nchi yao, bali atatafute mume wa kumuoa ambaye atakuwa ni mwenye nguvu kuzidi wanaume wote, na huyo ndiye atakayemuoa.

Hivyo binti huyu alijiwekea jukumu hili la kutafuta mwanaume atakayekuwa mume wake kama alivyojisemea mwenyewe. Alizunguka msituni, milimani, mtoni mpaka kwenye maziwani kujaribu kutafuta mwanaume huyu wa ndoto zake. Siku moja alifanikiwa kupata mwanaume imara sana anaishi katika ziwa. Lakini hakufanikiwa kuona mwili wake wote, aliishia kuona kichwa chake peke yake.Mwanaume huyo alimuuliza binti huyu, “unatafuta nini eneo hili?” Binti alimjibu, “namtafuta mume wangu atakayenichumbia na kuweza kunioa, lakini natamani huyo mume wangu awe ni mwenye nguvu kuzidi wanaume wote”. Mwanaume huyo wa ziwani akamwambia; “Kiukweli mimi ni mwenye nguvu kuzidi wanaume wote. Na nguvu zangu mtaziona, wewe na baba yako, na familia yako, sambamba na watu wote wa nchi yenu na kila kitu ndani ya nchi ya baba yako”.

Binti huyu aliposikia maneno hayo alifurahi sana kwamba amepata mume mwenye nguvu kuzidi wanaume wote. Hivyo walikubaliana na kupanga, na binti huyu alirudi nyumbani na kumweleza mama yake habari zote. Mama yake akamwambia; “ni vizuri lakini kwanza tumuone huyo mchumba wako ambaye atakuchumbia ambaye mmekubaliana.

“Hivyo binti alianza utaratibu wa kuwa anapika chakula na kumpelekea mchumba wake huyu ambaye wamekubaliana kwamba wataoana. Alipomfikishia chakula hicho alimpa na mchumba wake huyu alimeza chakula chote kwa pamoja sambamba na chungu chenyewe chenye chakula. Binti alistaajabu sana na kujisemea mwenyewe moyoni; “huyu ni mume wa namna gani anayemeza chakula chote kwa pamoja na chungu cha kupikia?”

Kisha binti huyu akamwambia mchumba wake; “Wazazi wangu wanatamani twende pamoja nyumbani kwetu ili wapate kukuona. Kisha watakupa ruhusu ya kunioa. Na hivi ndivyo walivyonituma kwako kukueleza.” Mchumba wake huyu wa ziwani alimjibu; “Ni sawa, lakini muda wangu wa kuja huko kwenye nchi yenu bado haujafika. Muda wangu wa kuja ukifika nitakuja huko kwenu kama jinsi unavyotamani.”

Binti alirudi nyumbani na kumweleza hayo mama yake. Mama yake akasema; “Ni sawa, lakini kwa hakika ni lazima tumuone.” Binti alipika chakula na kumpelekea na kumpelekea mchumba wake huyu wa ziwani siku zilizofuata. Mchumba wake alipokea chakula hicho na kukimeza kama alivyofanya mwanzo. Binti akamwambia: “Njoo sasa, twende nyumbani kwangu.” Mchumba wake alimjibu kwa wimbo huu.

“Hiya mangalawa lya Mchomba.

(Mimi ni Ngalawa ya kutokea pwani).

Ngakoya mndenyi ngiwemila.

(Nikifika nikamkuta baba yako nitammeza).

Ngakoya mmai ngiwemila.

(Nikimkuta mama yako, nitammeza).

Ngakoya msacha ngiwemila.

(Nikimkuta kaka yako nitammeza).

Hiya mangala lya Mchomba.

(Mimi ni ngalawa ya kutokea pwani).

Sasa binti huyu na mchumba wake walioongozana kwenda nyumbani kwa binti huku binti akitangulia mbele na mchumba wake akimfuata nyuma. Lo! Kumbe mchumba huyu alikuwa ni kiumbe kikubwa ajabu, alikuwa anaenea karibu nchi nzima. Wakati wakiendelea na safari yao ya kuelekea nyumbani mchumba wake huyu akamwambia binti, mimi kwa jina langu naitwa Rumu. Nimetumwa kwenu na kwa nchi nzima kuharibu kila kitu na kuangusha uumbaji wote.

Ruwa ameniagiza kuja kuangamiza binadamu wote na wanyama, kwa sababu watu wameziacha nchi zao njema za zamani na kuuendea uovu. Wanawakandamiza maskini, wameendekeza uvivu na wamekuwa ni watu wa majivuno kila siku. Hivyo kwanza nitaanza kukumeza wewe na wale wa nyumbani kwa baba yako, kisha nitameza watu wote wa dunia hii na wanyama wote.

Na siku hii ilikuwa ni siku ya kusherehekea kwa nyimbo na ngoma. Hivyo watu wote walikuwa wamekusanyika katika eneo la kusherehekea na kucheza sana ngoma. Walikusanyika watoto wa wakubwa wa kiume na wa kike. Waliendelea na safari binti akiwa ametangulia lakini tayari alikuwa amejaa hofu na kutetemeka sana kwa sababu ya maneno hayo ya Rumu. Walipokaribia nyumbani kwa kina binti huyo wazazi wake walikuwa sauti kubwa kama ya radi au tetemeko na hivyo walitoka nje kuangalia ni kitu gani hicho kinaitikisa dunia.

Ghafla moja Rumu akammeza binti huyo pamoja na watu wote wa familia yake. Hakubakia hata mtu mmoja katika kijiji cha baba yake. Alipomaliza Rumu aliwafuata wale waliokuwa wanasherehekea kwa ngoma na kumeza wote kwa pamoja kwa mara moja. Rumu hakubakiza mtu yeyote isipokuwa mwanamke mmoja ambaye alikuwa amejifungua mtoto siku hiyo. Mwanamke huyu alipoliona jitu hilo alikimbia kwenda kujificha kwenye zizi la ng’ombe yeye na mtoto wake mchanga.

Mtoto huyu mchanga alikuwa ni mtoto wa kiume. Mwanamke huyu aliweza kujiokoa yeye mwenyewe, binti yake mdogo pamoja na mtoto mchanga aliyekuwa amezaliwa. Rumu baada ya kumaliza kumeza watu waliokuwa wanacheza ngoma aliendelea maeneo mengine ya dunia nzima kumeza kila mtu. Aliendelea kumeza watoto kwa wakubwa, wanaume kwa wanawake na baada ya siku saba alikuwa ameshameza binadamu wote dunia nzima.

Hakubakia mtu yeyote duniani zaidi ya mwanamke yule mmoja na watoto wake wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike. Baadhi ya watu waliojaribu kujiokoa kwa kukimbilia msituni walishambulia na kulia na wanyama wakali hususan simba na chui. Wengine waliojaribu kupanda juu ya miti mirefu ili kujiokoa Ruwa alileta upepo mkali sana uliovunja vunja miti hiyo na kuwaangusha chini vibaya wakafariki. Wengine waliojaribu kukimbilia kwenye mapango ili kujiokoa Ruwa alipasua miamba iliyoko kwenye mapango kwa nguvu ambayo iliwaangukia wakafa.

Hivyo ndani ya siku saba binadamu wote duniani walitokomezwa kabisa. Rumu baada ya kuwatokomeza binadamu sasa akawarudia ng’ombe, mbuzi na kondoo. Rumu alimeza ng’ombe wote, mbuzi wote, kondoo wote pamoja na mbwa wote waliomilikiwa na watu.Lakini ndani ya nyumba ambayo mwanamke huyu maskini alikuwa amejificha pamoja na watoto wake kulikuwa na mifugo kadhaa Kulikuwa na ng’ombe watatu, majike wawili na dume moja, kisha mbuzi watatu pia majike wawili na beberu mmoja, na kondoo wawili moja dume(suwa) na moja jike pamoja na mbwa wadogo wawili moja dume na moja jike.

Rumu hakuingia kwenye nyumba hii aliyokuweko mwanamke huyu maskini na watoto wake kwani ilikuwa imefungwa vizuri na Ruwa aliilinda kwa sababu mwanamke huyu alikuwa maskini. Lakini wanyama wengine wote hawakuwa wa mwanamke huyu bali walikuwa ni mali za watu matajiri.Mali zake pekee zilikuwa ni mbwa hao wawili kwani mume wake alikuwa ni mwindaji wanyama wadogo wadogo kama vile digidigi kwa ajili ya kupata nyama.

Siku ya nane waziri wa Ruwa alikuja na kumwambia mwanamke huyu maskini: “Ondoka huko ulikojificha na utoke nje uweze kuitawala dunia wewe na mtoto wake mchanga kwani hakuna tena matajiri wala maskini wa kukunyanyasa na kukukandamiza. Na mtoto wako mdogo utamwita jina lake MKECHUWA.

Mkechuwa atakuwa mtu mkuu na atarekebisha mabaya yote yaliyofanywa na Rumu na Ruwa mwenyewe ataihurumia tena dunia. Na utafundishwa tena kuwinda kwa kutumia mishale kama jinsi alivyokuwa anafanya baba yako.

Waziri wa Ruwa alipoondoka na kurudi kwa Ruwa kumpelekea habari kuhusiana na Rumu na kazi aliyoifanya na mwanamke maskini aliyemkuta pamoja na mtoto wake aliyeitwa Mkechuwa, mwanamke huyu alitoka nje kuanza kuiangalia nchi yake. Alizunguka na kutafuta kila mahali lakini kulikuwa na ukimya mkuu. Hivyo aliishi yeye na watoto wake na wanyama wao katika ukimya mkubwa.

Alipoona hana kabisa marafiki wala kampani aliamua kujenga nyumba juu ya tawi la mti mmoja mkubwa na kuishi yeye na watoto wake. Kisha wanyama wake wakaishi katika nchi iliyojaa neema kubwa. Mwanamke huyu aliendelea kumhadithia mtoto wake Mkechuwa juu ya yale yote yaliyotokea katika nchi na juu ya Rumu pamoja na hasira ya Ruwa.

Mkechuwa alipokuwa mkubwa alikuwa mwindaji hodari sana wa aina zote za wanyama kuanzia ndege wa angani mpaka wanyama wenye miguu minne. Na kila alipowinda wanyama mbalimbali, wakubwa kwa wadogo alimuuliza mama yake, “Mama, huyo Rumu aliyetokomeza kila kitu na kuacha ukiwa, ndio huyu au sio?”. Mama anamjibu; “Sio huyo”, hii ni nyama yetu”. Kwa hiyo Mkechuwa aliendelea kuwinda kila siku.

Kisha Mkechuwa alioa mke aliyepewa na mama yake, na mke huyu alikuwa ni dada yake, ambaye alizaliwa wa kwanza kabla ya Mkechuwa. Kwa hiyo Mkechuwa alioa akapata watoto wengi wakike na wakiume. Mkechuwa aliwalea watoto wake kwa maadili na kuwapa mafunzo bora na malezi sahihi ili wasifanye uovu kama uliofanyika kabla ya dunia kuangamizwa ili Ruwa asije kuwa hasira na kuiangamiza dunia tena kwa mara nyingine.

Hivyo watu wakaongezeka tena duniani kwa mara nyingine. Mkechuwa aliishi miaka mingi sana mpaka akazeeka sana na kujaliwa kupata wajukuu wengi sana na vitukuu. Mwishowe Mkechuwa akaja kufariki. Kuanzia wakati huo Ruwa hakuwahi kutuma tena Rumu kwa ajili ya kuiangamiza dunia.

Hii ndio hadithi ya Mkechuwa iliyokuwa inafahamika kwa wachagga iliyoweza kuelezwa kwa waandishi mbalimbali mwishoni mwa karne ya 19 kutokwa kwa wazee wa kichagga.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na hadithi ya Ruwa kuiangamiza tena dunia kwa mara ya pili.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

2 Comments

  1. Kweli tupu tulinde urithi wetu kwa wivu mkubwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *