ASILI/CHANZO CHA HALI YA UZALENDO KWA JAMII/TAIFA/KABILA/KUNDI LA KIJAMII AMBALO MTU ANATOKEA NA LINALOMPA UTAMBULISHO FULANI.

– Tabia nyingi za asili tulizonazo binadamu haziko kwa bahati mbaya kwani nyingi zina chanzo chake na sababu muhimu sana katika maisha yetu, lakini ni mara chache sana watu huelewa chanzo na sababu hizo kwa mambo husika.

– Kupitia mabadiliko ya binadamu kihistoria tangu zama za zamani kabisa (prehistoric times) katika kipindi kinachofikia mpaka mamia elfu ya miaka na zaidi, binadamu ameendeleza tabia fulani ambazo zimemsaidia na zinaendelea kumsaidia katika kukabiliana na mazingira yake ili kuweza kuishi kwa usahihi na kwa usalama kadiri ya kanuni zenyewe za asili. Dhana hii inajulikana kwa lugha ya kiingereza kama (evolutionary psychology).

– Sasa kuna hali ya mtu ambayo iko kiasili ya mtu kuipenda sana jamii yake/kabila lake na kuwa na uzalendo mkubwa sana kwa jamii hiyo na kujivunia sana hilo hususan kama jamii hiyo ni jamii ya watu bora na wanaofanya mambo makubwa na ta kifahari katika maisha. Hali hii au hisia hizi ziko ndani kabisa ya watu japo wakati mwingine watu huwa hawako huru kuzionyesha hisia hizi na badala yake wanazificha ndani kwa nguvu lakini moyoni wanazihisi kabisa.

– Hisia hizi ziko kwa asili na ziko kwa binadamu walio wengi, karibu binadamu wote lakini kwa viwango tofauti tofauti kwa kila mtu na haijalishi mtu huyo yuko katika ngazi gani kijamii, changamoto ni kwamba tu watu kwa sababu mbalimbali huwa hawaonyeshi moja kwa moja. Tunaweza kuona kwamba hata mwanafalsafa nguli na moja kati ya watu au mtu aliyewahi kuwa na akili sana duniani wa Ugiriki ya kale aliyejulikana kwa jina la Aristotle alikuwa na hisia kali sana za kizalendo kwa Ugiriki ya kale au Uyunani ya kale.

– Wakati huo wagiriki wakiwa ni wasomi sana na watu waliopiga hatua kubwa sana kimaendeleo na wenye nguvu sana Aristotle alionekana kujivunia na kufurahia sana hilo. Alijitahidi kumshawishi Alexander the Great awekeze katika kuwaendeleza sana Wayunani ambao waliendelea mpaka kuiangusha dola ya Uajemi wakati wa utawala wa Darius III na baadaye kuiangusha na Misri na kuzitawala. Hapa ndio utajua kwamba asili hii ya uzalendo ina nguvu sana kama iliweza kuwa sifa ya mwanafalsafa msomi na mashuhuri ambaye mpaka leo ni vigumu kumpata mtu wa uwezo ule duniani.

– Sasa chanzo cha asili hii inayotokana na (evolutionary psychology) ni asili ya binadamu kuhakikisha yuko salama muda wote. Kwa miaka ya zamani sana (prehistoric time) mtu alikuwa hawezi kuwa salama kwa kukaa peke yake bali ilikuwa ni lazima uwe kwenye kundi/jamii/kabila ili inapotokea hatari iwezekane kujilinda kwa pamoja. Ukikaa peke yake utaishia kuuawa na watu wa jamii nyingine au hata wanyama wakali ambao walikuwa wanaishi kwenye mazingira ya pamoja na binadamu. Hivyo kuwa salama ilikuwa ni lazima uwe kwenye kundi/jamii ambayo ina majeshi makubwa ambayo yako kwa ajili ya kujilinda dhidi ya hatari yoyote ambayo ingeweza kuwaangamiza.

– Hivyo kwa sababu ili mtu uwe salama na kufanikiwa kuishi ni lazima uwe ndani ya jamii basi watu wakajikuta wanazipenda sana jamii zao kwa sababu ndio salama yao pekee na pia kuendeleza uzalendo wa hali ya juu ili kuzipigania jamii hizo dhidi ya kundi/kabila lingine lolote hatari ambalo linaweza kuwavamia na kuwaangamiza kabisa. Na kweli kuna makabila mengi yalipotea kabisa ambayo yaliangamizwa kabisa na makabila mengine yenye nguvu. Hata kuna aina nyingine ya binadamu inayojulikana kama neanderthals ambayo iliangamia na inayosemekana kwamba iliangamizwa na binadamu wa spishi ya sapiens.

– Sasa ilikuwa mtu anaweza kupata furaha na kujivunia pale anapokuwa kwenye jamii yenye nguvu na hivyo kuvaa roho ya uzalendo na kuipigania sana jamii yake kwani kwa kufanya hivyo ndipo anaweza kuwa salama na kuwa na kuendeleza kizazi hicho. Hivyo ndivyo saikolojia ya binadamu ya kuwa mzalendo sana kwa jamii yake dhidi ya jamii nyingine ilikotokea na kuendelea mpaka sasa ambapo tabia hizi zitaendelea kuwepo angalau hata kwa miaka elfu hamsini ijayo au zaidi kwani imetokea mbali sana pia.

– Kwa wale wanaofikiri kwamba binadamu watafika mahali na kuacha kujivunia wao kutokea kwenye jamii fulani au kusikia ufahari kuhusishwa na jamii bora na iliyopiga hatua wanajidanganya. Hali hii ya watu wa jamii na mataifa mbalimbali kujivunia jamii yao au kundi sio jambo lililopitwa na wakati wala sio jambo la kuisha leo wala kesho kwani liko ndani kabisa ya tabia za binadamu wa sasa, yaana ni asili iliyoshoneshewa ndani ya saikolojia ya binadamu hivyo sio jambo unaloweza kumtenganisha nalo mtu kiurahisi. Ushahidi wa haya uko kila mahali duniani.

– Hii ndio sababu pia hata vitu vyenye itikadi kama vile timu za mipira japo hazina umuhimu mkubwa sambamba na aina nyingine za ushabiki kama siasa au dini vina nguvu sana kwa wafuasi wake. Sababu kubwa ni kwa vile nazo zimekaa kwa mfumo wa makundi/makabila ndio maana mtu akishakuwa kwenye kundi mojawapo anakuwa na uzalendo nalo zaidi na muda mwingine anafikiria namna litafanikiwa na pale linapofanikiwa anakuwa na furaha sana au linapopoteza anaumia sana. Hiyo ni asili ya mambo haya inavyofanya kazi. Sasa vitu vyenye utambulisho rasmi na vyenye historia kubwa kama jamii/kabila vinakuwa na nguvu kubwa zaidi sana ukilinganisha na hivyo vingine.

SWALI LINAKUJA, JE KWA DUNIA YA SASA TABIA HIZI ZA ASILI ZINA UMUHIMU WOWOTE?JIBU NI NDIO ZINA UMUHIMU WAKE.

– Jambo la kwanza tunapaswa kuzingatia kwamba tabia hizi ni za asili hivyo uwe unazipenda au huzipendi huwezi kuzibadilisha kwa namna yoyote ile wala kuziondoa kwa watu, hivyo ni muhimu sana kuangalia namna ya kuzitumia kwa mafanikio.

– Lakini muhimu zaidi ni kufahamu kwamba kuna vitu kisaikolojia vinajenga kujiamini na kujithamini sana(self esteem) ikiwa ni pamoja na mtu kuwa sehemu ya jamii ambayo ni bora na yenye ufahari. Mtu anayetokea kwenye jamii bora na iliyofanikiwa ana nafasi kubwa sana ya kufanikiwa ukilinganisha na mtu anayetokea kwenye jamii dunia na inayodharaulika. Hebu chukua mfano wa kati ya mtu anayetokea kwenye jamii ya wajerumani na mtu anayetokea kwenye jamii ya wamalawi yupo ambaye ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri pale wanapopewa nafasi. Unaweza kuona ile tu hali ya kujiamini kwa Mjerumani tayari ni faida kubwa kabisa kwake.

– Lakini pia utofauti na ushindani wa kimafanikio baina ya jamii na jamii unajaribu kufanana na ule wa mtu na mtu kwani unaleta changamoto ya watu kufanya vizuri zaidi. Pale tunapotamani kuwa sawa au kufanana na kila mtu kwanza tunaenda kinyume na kanuni ya asili lakini pia tunaua ile asili ya mapambano ya kupeleke maendeleo mbele. Saikolojia hii ya ushindani imewasaidia sana Wachina na Wakorea katika kupiga hatua kuweza kuelekea kuwafikia Wajapan na imekuwa na nguvu sana kwa sababu asili yake ina nguvu sana.

– Sasa kwa kuwa ile hali ya kuwa kwenye jamii yenye maendeleo na iliyojaa ufahari kwa sababu ya juhudi zao kubwa katika maisha inamfanya mtu ajivunie na kujisikia ufahari wa kuwa katika jamii hiyo itakuwa ni chachu ya kuongezeka bidii katika maisha ili kuhakikisha jamii hiyo inakuwa bora na yenye maendeleo siku zote ili iendeleee kuwa yenye kujivunia. Hii ni kwa sababu jamii inapoporomoka na kuwa ya hovyo hudharauliwa kiasi kwamba watu wake huchukia hata kujitambulisha kwamba wanatokana na jamii hiyo.

– Kwa hiyo ili tuendelee kujivunia kwamba tunatoka kwenye jamii yenye ufahari tutaongeza bidii kubwa na hivyo kuzidi kuwa na mafanikio zaidi kwenye maisha. Wewe chukulia jamii au mataifa mengi ambayo yalikuwa yanafanya vizuri karne kadhaa zilizopita utakuta mpaka leo ndio yanayoongoza uchumi wa dunia. Hiyo ni kwa sababu wanazidi kuweka bidii kubwa katika kila eneo ili waendelee kujivunia ufahari walionao tofauti na zile jamii/mataifa duni jinsi zinavyojivuta kwa sababu hata hali ya kujiamini ni ya kususasua.

– Kwa maana hiyo hata sasa bado kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuipigania jamii yetu ambayo ndio utambulisho wetu wa asili wa kwanza, kwa sababu mafanikio yake ni furaha yetu na ufahari wetu sote unaotupa kuheshimiwa sana na kukubalika na watu. Hili ni jambo linalotupa furaha na ufahari badala ya kujichukia na kujidharau kama jamii ambazo ni duni. Hii maana yake ni kwamba japo zamani asili hii ilikuwa ina kazi tofauti lakini hata sasa bado ina umuhimu wake mkubwa. Hii ni kwa sababu inaleta tafsiri ya haraka ya vile ambavyo unatambulika.

Karibu kwa Maoni.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *