“THE JEWISH PHENOMENON” “SEHEMU YA 5” Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Utajiri Mkubwa na Unaodumu.

“THE JEWISH PHENOMENON”

“SEHEMU YA 5”

Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Utajiri Mkubwa na Unaodumu.

1. UTAJIRI UNABEBEKA, NI MAARIFA, NI ELIMU.

Mwandishi anasema uwekezaji bora zaidi mtu anaoweza kuufanya kwa ajili ya baadaye ni elimu na maarifa.

Hata kama elimu hiyo itakugharimu sana au kukuacha na madeni bado hakuna mtu anaweza kuiondoa elimu hiyo kichwani kwako au kukunyang’anya, ukishaipata imekuwa yako na itakusaidia haijalishi umeipata kwa gharama kiasi gani.

Mwandishi anasema wayahudi wamekuwa wakiipa elimu kipaumbele cha kwanza kabla ya kitu chochote na wamekuwa wakihamasishwa juu ya kupata elimu bora tangu wakiwa wadogo kabisa.

Anasema ikitokea mtoto mdogo wa kiyahudi amelilia kitu ambacho ni cha gharama kuliko uwezo wa mzazi wake basi mzazi wake anaanza kumjengea mtazamo kwamba aweke bidii katika elimu na kujifunza na atakuja kuwa na uwezo wa kununua midoli mizuri au vigari vizuri au baiskeli za gharama sana za kutumia.

Mwandishi anasema mtoto wa kiyahudi anavyoendelea kukua mzazi wake alianza kumuonyesha uhalisia wa gharama za maisha zilivyo kubwa na kwamba atahitaji kuwa kwenye nafasi ya kuingiza kipato kikubwa sana ili kuweza kuishi maisha bora yasiyokuwa na misukosuko ya kifedha, hivyo anapaswa kupata elimu bora itakayomhakikishia kipato kizuri kitakachotosha kumudu gharama za maisha bora, kwa hiyo anapaswa kuweka nguvu kubwa sana katika kupata maarifa bora kwa manufaa ya baadaye.

Mwandishi anasema hii ilipelekea kufikia miaka ya 1990 idadi ya wayahudi waliokuwa na elimu ya juu Marekani kuwa mara mbili zaidi ya idadi ya wazungu.

Mwandishi anasema swali wayahudi halijawahi kuwa endapo atasoma elimu ya juu bali swali lilikuwa ni wapi ataisomea hiyo elimu ya juu.

Mwandishi Steven Silbiger anasema wayahudi walifukuzwa na kuondolewa kwenye ardhi yao na mara kwa mara wamekuwa wakifukuzwa au kupigwa marufuku katika nchi mbalimbali, hilo lilipelekea wayahudi kutegemea zaidi maarifa bora ili kuendelea kwani mara nyingi walijikuta hawana ardhi wala mali kutokana na kukosa utulivu katika vipindi mbalimbali katika historia.

Kwa mujibu wa mwandishi wayahudi waliwahi kufukuzwa Ujerumani mwaka 1,182, walipigwa marufuku Uingereza kati ya miaka ya 1,290 mpaka 1,650, walifukuzwa Ufaransa mwaka 1,306 na mwaka 1,394, walizushiwa kuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko na hivyo kunyanyasika sana Ulaya mwaka 1,348, walifukuzwa Austria mwaka 1,421, walifukuzwa Hispania mwaka 1,492, Poland mwaka 1,648, Vienna mwaka 1,670, Prague mwaka 1,744, na Ulaya mashariki chini ya Urusi mwaka 1,880.

Hivyo wamejikuta wakitegemea akili na maarifa kuweza kumudu maisha katika hali hizi za kutokuwa na uhakika wa utulivu. Wayahudi wamekuwa wakijulikana kama “watu wa kitabu”, Watoto wa kiyahudi wamekuwa wakifanyiwa sherehe kubwa na kupongezwa sana pamoja na kupewa zawadi nyingi siku ya kwanza wanapokwenda kuanza shule. Lengo lake ni ili kumjengea mtoto mtazamo kwamba elimu ni kitu cha thamani na ambacho wazazi wameweka matumaini makubwa kwamba watafanya vizuri na kufika mbali.

Wayahudi pia wamekuwa wakijifunza elimu ya dini na wamekuwa wakisoma na kuhoji sana maandiko ya kidini kutoka kwenye Biblia, ambayo ni kama historia yao, pia kutoka kwenye Torah, Talmud na Mishna ambavyo ni vitabu vya dini ya kiyahudi.

Tofauti na wakristo ambao huwa wanakuwa na hofu ya kuhoji chochote kilichoandikwa kwenye biblia na badala yake kukubaliana nacho kama kilivyo kwa kuamini kwamba vyote vilivyoandikwa ni vitakatifu sana, wayahudi wao huwa wanaihoji biblia na hata kuikosoa katika mijadala mbalimbali bila hofu ya kuamini kwamba wanakosoa kitabu kitakatifu.

Wayahudi wamefundishwa kujifunza kuishi na kila aina ya ugumu unaotokea kwenye maisha na kujifunza mbinu za kukabiliana na changamoto hizi kwa haraka badala tu ya kuamini kwamba zinaweza kutoweka kwa miujiza.

Kutokana na wayahudi kuwekewa vikwazo vingi katika kujiunga na elimu ya juu ya nchini Marekani mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, wayahudi walijenga taasisi zao wenyewe za elimu ya juu kwa wingi ili wasiachwe nyuma katika kupata maarifa bora ya elimu ya juu na kufikia miaka ya 1930’s walikuwa wamepiga hatua kubwa katika zile taaluma zenye kipato kikubwa. Ambapo katika jiji la New York asilimia 55% ya madaktari walikuwa ni wayahudi, asilimia 64% ya madaktari wa meno(dentists) na asilimia 65% ya wanasheria walikuwa ni wayahudi.

Mwandishi anasema kwamba wayahudi pia wana role models wengi wa kiyahudi ambao wamefanya makubwa wanaoweza kujifunza kutoka kwao katika kila nyanja ya maisha ya kiuchumi na na kitaaluma.

#MWANDISHI ANASHAURI YAFUATAYO KAMA UNATAKA JAMII AU KIZAZI CHAKO KUWA KWENYE NAFASI YA KUPATA MAFANIKIO MAKUBWA NA YA KUDUMU.#

1. Mjengee mtoto kujiamini katika kitu anachoweza kufanya kwa ubora, mfanye ajisikie ni kati ya watu wateule bila kujali historia ya nyuma.

Wafundishe Watoto historia ya kwenu na ya mababu zenu pamoja na mambo makuu na makubwa yaliyofanywa na mababu zenu. Hii husaidia watoto kuwa na kitu cha kujivunia na misingi ya kuisimamia hivyo kutengeneza focus zaidi kwenye maisha tofauti na mtoto kubaki akiwa hajui historia yoyote ya nyuma ya kizazi chake.

2. Wajengee watoto uwezo wa kuahirisha starehe na anasa za dunia na kuweka nguvu kwenye maarifa, nidhamu hiyo itasaidia kumjengea msingi wa tabia sahihi ambayo itamuimarisha sana katika maeneo muhimu ya maisha.

Hili linawezekana zaidi kupitia kumpongeza mtoto pale anapofanya vizuri darasani sambamba na kumnunulia zawadi mbalimbali ili kumjengea tamaa na hamu ya kuendelea kufanya vizuri.

3. Mpatie mtoto elimu bora zaidi inayoweza kupatikana.

Mwandishi anasisitiza kwamba sio tu elimu bali elimu bora na ya viwango vya juu. Wayahudi wengi huingia katika vyuo vinavyojulikana Marekani kama “Ivy League Schools”, ambavyo ndio vyuo bora kabisa kama Havard University, MIT, Stanford University, Columbia University n.k.,.

Mtoto anatakiwa kujengwa tangu mdogo apambane kutambua mbinu mbalimbali za kumwezesha kusoma vyuo bora kwani mara nyingi huko ndiko uwezekano pia wa kukutana na watu watakaoweza kuwa na msaada mkubwa mbeleni katika kufanya vizuri kwenye maisha kwa sababu mbalimbali.

4. Mfundishe mtoto na kumwingizia kichwani kwake mambo mbalimbali yatakayopelekea kujenga hamu na shauku ya kujifunza zaidi. Mfundishe hadithi na mafanikio ya mashujaa mbalimbali waliopita hasa kutoka kwenye jamii yenu na onyesha kuwakubali sana ili mtoto ajenge hamu ya kujua zaidi na kutaka naye kufanya vizuri kwenye maisha.

5. Mwonyeshe mtoto kwamba unategemea makubwa sana katika safari yake ya elimu, kwamba unategemea atafika mbali na fungua kabisa akaunti ya kuweka fedha kwa ajili ya elimu yake ya juu naye afahamu kabisa kwamba tayari kuna fedha inawekezwa kwa ajili ya elimu yake ya juu.

Wayahudi wao swali huwa sio kama mtu atafika elimu ya juu bali swali ni kwamba ataisomea wapi hiyo elimu ya juu. Hiyo inamjengea mtazamo wa kwamba hana njia nyingine zaidi ya kuweka bidii kubwa sana katika elimu yake kwani tayari wazazi wanatarajia atafika mbali.

6. Unapokuwa mtu mzima au kumaliza elimu ya kawaida unatakiwa kuendelea kujielimisha sana kwa ujuzi na maarifa mbalimbali hasa kusoma vitabu katika nyanja mbalimbali, ambavyo kwa dunia ya sasa ni vingi na vina maarifa bora sana.

Ahsanteni

Kwenye makala inayofuatia Tutaendelea na Siri Ya Pili.

N. Moshi

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *