KWA NINI VIKUNDI VINGI VYA KIJAMII AU TAASISI ZA KIJAMII ZINAZOANZISHWA HAZIFIKII MALENGO YA KIUCHUMI?

Wachagga wamekuwa wakianzisha vikundi mbalimbali vya kijamii vyenye malengo tofauti tofauti tangu zamani sana japo mara nyingi lengo kuu huwa ni kujiwekeza kiuchumi na kuvuna faida kwa manufaa ya wanachama wa kikundi au taasisi husika.

– Lakini kwa bahati mbaya vikundi vingi au taasisi hizi za kijamii huwa hazifikii malengo na nyingi hufa ndani ya kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake. Mimi binafsi nikiwa nimewahi kuwa mwanachama katika vikundi hivi na hata kuanzisha pia moja kati ya vikundi hivi kuna mambo mengi nimejifunza kwa uzoefu na hata kutoka kwenye uzoefu wa vikundi vingine. Hii ni sambamba na kujifunza pia kanuni mbalimbali za kijamii na kiuchumi hivyo kuelewa pia kinadharia juu ya maanguko haya ya kitaasisi kwa viwango vya mashirika makubwa na taasisi kubwa.

– Hapa nitajaribu kujadili kwa nini vikundi hivi havifikii malengo kwa upande wa malengo ya kiuchumi ambayo vingi ndio hulenga ikiwa pia ndio eneo lenye changamoto kubwa. Kwa upande wa malengo ya kijamii changamoto zake sio kubwa sana lakini pia hujikuta yakiathiriwa na kushindwa kufikiwa kwa malengo ya kiuchumi.

– Kwanza kabisa faida ya vikundi hivi vya kijamii ambayo pia ndio hupelekea msukumo mkubwa wa uanzishwaji wake ipo kwenye eneo la mtaji. Kwa watu kuwa katika kikundi ni rahisi kukusanya mtaji mkubwa na kwa haraka ukilinganisha na mtu akiwa mmoja peke yake na hivyo inakuwa rahisi kuanzisha lile jambo ambalo linalengwa kwa haraka.

– Sasa sababu ya kwanza na kubwa inayopelekea kushindwa kufikiwa kwa malengo ya vikundi hivi ni kukosekana kwa uongozi makini unaoelewa kwa usahihi na kwa uzoefu ni wapi watu hao wanaelekea. Eneo hili la uongozi ni muhimu kwa sababu ndilo linalotoa matumaini kwa wanachama na kuleta uhai wa kundi lakini pia ndilo eneo ambalo maamuzi mengi ya mwisho ya kundi hufanyikia. Uongozi au kiongozi anapaswa kuwa na maono makubwa ya kule taasisi inapoelekea, uwezo binafsi kiuongozi na uzoefu wa kujua ni kipi sahihi cha kufanya katika safari nzima ya kufanikisha malengo yaliyoazimiwa. Sasa kupata kiongozi wa namna hii ambaye pia amejitoa kikamilifu kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa sio jambo rahisi.

– Kupata kiongozi sahihi sio jambo rahisi kwa sababu mbili kubwa, kwanza watu wenye uwezo huo mkubwa ni wachache sana hivyo ni nadra kupatikana kwa urahisi. Pili ni kwamba hata hao wachache sana wanaopatikana ni vigumu kuwa tayari kujitolea kwa jambo la kijamii badala yake utamkuta tayari yuko kwenye jambo lingine la kubwa analofanya aidha kwa kuajiriwa au kwa biashara zake binafsi. Hii ni kwa sababu taasisi inayoanza huwa haina uhakika wala mtaji wa kutosha kumshawishi mtu mwenye uwezo mkubwa kutumia muda wake na rasilimali zake kuhangaika kukuza taasisi hiyo vinginevyo awe na mapenzi makubwa kupitiliza katika jambo hilo.

– Sababu ya pili ni kukosekana kwa uelewa mpana miongoni mwa wanachama juu ya ugumu wa safari iliyopo mbele yao ya kufikia malengo hayo. Mara nyingi watu na hasa vijana hususan waliopo kwenye miaka ya 20’s na hata mpaka 30’s, saa nyingine hata mpaka 40’s hawana uelewa mkubwa wa changamoto nzito sana zilizopo katika kufikia malengo yoyote makubwa kwenye maisha. Ahadi rahisi zinazotolewa na uongozi wa taasisi huaminiwa kirahisi na watu na hasa wa kundi hili la umri huo bila kujua safari nzito sana na yenye kila aina ya changamoto iliyopo kati ya hapo walipo na kufikia malengo wanayoweka. Hii hupelekea watu kuwa na matumaini makubwa mwanzoni na baada ya muda kupita bila kuona matokeo waliyotarajia huishia kukata tamaa na kupelekea morali yote kupotea na hivyo kikundi au taasisi husika kuishia kufa bila kufikia malengo waliyojiwekea.

– Sababu ya tatu na ambayo imekuwa na ushahidi mkubwa sana na wa wazi kutoka kwenye historia ni suala zima la kitu cha wengi kukosa mtu mwenye uchungu nacho wa kukisimamia. Hii ni kwa sababu ya sifa mbili kubwa walizonazo binadamu kiasili ambazo ni uvivu na ubinafsi. Pale ambapo tunajua kwamba kuna wengine ambao watafanya jambo huwa tuna kawaida ya kutegeana tofauti na pale mtu anapojua kwamba jambo fulani linamhusu yeye peke yake. Lakini pia jambo linapokuwa lina manufaa kwa wengi na sio kwa mtu mmoja peke yake moja kwa moja mtu anaona kama kujitoa sana kunaenda kunufaisha wengine wengi pia zaidi kwa hiyo haweki nguvu kubwa kama ambavyo angeweka kwenye jambo binafsi linalomnufaisha yeye peke yake moja kwa moja. Hisia hizi kwa sababu zipo ndani yetu sio rahisi sana kuzikabili bila kuwepo kwa nguvu ya ziada.

– Jambo hili unaweza kuliona zaidi kupitia taasisi na mashirika ya kiserikali ambapo uzembe na kutojali ni utamadani wa kawaida kabisa kwa mashirika hayo. Mashirika mengi ya serikali huendeshwa kwa hasara lakini hakuna mtu anayejali sana juu ya hilo kwa sababu hasara hiyo haimuathiri Rais, mkurugenzi na watendaji wengine moja kwa moja, sana sana wanaweza kutengeneza takwimu feki kuonyesha kwamba shirika linapata faida na shirika likaweza kuendelea kupewa fedha za kujiendesha kutoka kwenye kodi za wananchi ambazo zinapatikana bure kabisa. Hii ni kwa sababu hakuna mtu mwenye uchungu wa moja kwa moja kuhakikisha kwamba shirika hilo linafanya vizuri na hakuna mtu anayeathirika zaidi ya kuwa tu mzigo kwa wananchi walipa kodi.

– Hata serikali ambazo kiuhalisia hazina mwenyewe mhusika zaidi ya kusemekana ni mali ya umma isipokuwa wanasiasa ambao wengi wao wapo kwa ajili ya maslahi yao binafsi, zisingeweza kujiendesha kama sio kutoza kodi kwa wananchi. Licha ya serikali kuwa na biashara kadhaa lakini biashara hizo kwa kuwa ni za umma maana yake watu waliopo kwenye nafasi za uongozi ni wapitaji tu na wala hawana malengo ya muda mrefu basi hakuna anayejali sana, hivyo biashara nyingi zina hasara kwa sababu hakuna anayejali faida wala hasara. Serikali zipo na zinaendelea kuwepo kwa sababu zinatoza kodi ambazo ni jasho la wananchi na hivyo haziishiwi fedha, lakini kwa namna zinavyoendeshwa ingekuwa zinapaswa kutafuta faida zenyewe ili zijiendeshe bila kutegemea kutoza wananchi kodi basi zingeshaanguka zamani sana.

– Hii ndio sababu kuu kwamba itikadi ya ujamaa katika uchumi ilishindwa kabisa. Itikadi ya ujamaa ilikuwa na sera kwamba njia zote za uzalishaji kumilikiwa na serikali, ikimaanisha kwamba hakuna mtu binasi aliyeruhusiwa kuendesha biashara zaidi ya serikali. Hii ni kumaanisha kwamba wananchi wataishia kuwa waajiriwa wa serikali. Kitu muhimu kilichosahaulika hapa ni kwamba serikali sio ya mtu na hivyo hakuna mtu mwenye uchungu nayo, hata huyo Rais ambaye ni mwanasiasa kiasili hana uchungu na serikali kwa sababu sio mali yake binafsi, bali yeye ni mpitaji tu. Hivyo ujamaa ulishia kuanguka vibaya dunia nzima na hakuna nchi yoyote duniani iliyoweza kufanikiwa kuwa na uchumi imara kupitia mfumo wa ujamaa kiuchumi licha ya propaganda nyingi za kisiasa zinazoendelea na kuaminiwa na watu wasiofuatilia mambo ili kufahamu undani wake. Mfumo wa kijamaa hauwezi kufanikiwa kamwe kwa sababu katika uhalisia unaenda kinyume na asili ya binadamu. Hii ndio maana serikali zilizoua sekta binafsi na kutaifisha mali za watu ili kuendesha biashara hizo yenyewe zilishia kuanguka vibaya dunia nzima na kusababisha umaskini mkubwa kwa watu na matatizo makubwa kiuchumi na hata kijamii.

– Ujamaa ulijengwa kwenye misingi inayokaribia kufanana na namna vikundi hivi vya kijamii vinaendeshwa na ndio maana hata vikundi hivi vinaishia kudhoofika na kufa. Hii ni tofauti na biashara zinazoendeshwa na wahusika ambao wana uchungu nazo kwani wanaweka nguvu zao zote, kufanya kazi kwa bidii sana bila kuchoka na kudhibiti kila aina ya ubadhirifu na uharibifu unaotokea kwenye biashara hizo na hivyo kusonga mbele.

– Sababu ya nne ni vikundi hivi kuanzisha biashara mpya ambazo hawana uzoefu nazo na hivyo kuishia kufa kutokana wahusika kukosa uwezo na uzoefu wa kuziendesha. Hili linapelekea watu kupoteza mtaji mkubwa waliouchanga kwa shida na hivyo kukata tamaa kuendelea na biashara kuangamia kabisa. Kiuhalisia kuanzisha biashara ikasimama sio jambo rahisi. Mtu anapaswa kujitoa kweli kweli kuweka kazi kubwa na muda mrefu sana mpaka kusimamisha biashara hiyo, nidhamu ambayo sio rahisi kwa watu wengi.

– Takwimu zinaonyesha kwamba asilimia 80% ya biashara hufa ndani ya kipindi cha miaka mitano baada ya kuanzishwa. Hii ni kwa sababu nguvu kazi, mtaji na muda ambao mtu anapaswa kuweka kwenye biashara huku akiwa na maarifa sahihi ya namna ya kuendesha biashara hiyo huwa sio jambo rahisi sana kwa wengi. Sasa ukichangia na ukweli kwamba pia biashara hizi ni za jumuia basi utakuta watu hawajitoi sana na biashara husika kufa. Biashara kusimama sio jambo la mzaha mzaha hivyo kabla ya kuwekeza kwenye biaashara yoyote watu wanapaswa kujua kwa uhalisia juu ya ni nini wanachofanya.- Sababu ya tano inaweza kuwa ni ubadhirifu wa fedha na mali za taasisi kwa sababu ya tabia mbaya za kukosa uaminifu miongoni mwa walioaminiwa na kupewa dhamana ya uongozi inayoweza kuchangiwa pia na kukosekana kwa mfumo imara wa taasisi husika katika kukabiliana na changamoto kama hizo.

– Sababu ya sita inayotaka kufanana na hiyo ni kuwepo kwa nia ovu miongoni mwa waanzilishi. Wakati mwingine watu wanaweza kuanzisha kikundi au taasisi ya kijamii wakijnadi kwamba wanataka kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya wanajamii husika, kumbe huku nyuma ya pazia wakiwa na mipango yao mingine ovu ya kufanya utapeli na kukimbia, hii nayo ni changamoto iliyopo.

JE SASA NDIO KUSEMA HAKUNA MATUMAINI KABISA KWENYE KUWEKEZA KATIKA TAASISI ZA KIJAMII IKIWA TUNAHITAJI KUJILETEA MAENDELEO.

– Kimsingi matumaini yapo makubwa sana kwa sababu njia mbadala zipo lakini jambo la muhimu sana la kwanza ni kuishi katika ukweli na uhalisia wa mambo. Kuishi katika ukweli na uhalisia ndio itasaidia kuleta mafanikio katika hizi taasisi binafsi. Kuishi katika uhalisia ni kujua kwamba suala la kuanzisha biashara kwa mafanikio halijawahi kuwa rahisi na halitakuwa kuja kuwa rahisi. Kwa wale waliowahi kufanya biashara na hasa wale wenye mafanikio katika biashara wanatambua hili kwa usahihi sana. Lakini pia kuendesha kikundi au taasisi ya kijamii sio suala rahisi sana pia ikiwa hakuna uongozi wenye kujitambua ni nini wanachofanya na wapi wanakotaka kuelekea.

– Hivyo sasa kwa kujua kwamba kuanzisha biashara na kuisimamisha kwa watu waliopo kwenye vikundi ni kazi ngumu sana, ni vyema kuwekeza fedha hizo kwenye biashara nyingine ambayo tayari ilishaimarika na inayoendeshwa na watu wenye uwezo na uzoefu kwa makubaliano maalumu na biashara husika. Hii linaweza kufanyika kwa kuwekeza pia kwenye masoko ya mitaji au masoko ya hisa kama DSE, na hilo hasa ndio lengo halisi la masoko haya ya mitaji na kisha kusubiri gawio. Au kuwekeza kwenye mifuko ya pamoja kama vile UTT-Amis na mingine ya namna hiyo.

– Mbadala mwingine ni kuwekeza kwenye mali zisizohamishika kama vile ardhi na majengo. Mali hizi hupanda thamani kadiri muda unavyokwenda na baadaye kujikuta mmekusanya utajiri mkubwa. Hata hivyo njia hizi mbili zinahitaji uvumilivu mkubwa sana kwani inachukua miaka mingi kuweza kuyaona mafanikio yanayotarajiwa tofauti na ambavyo wengi hufikiri na kutegemea mafanikio ya haraka haraka. Jambo muhimu kufahamu ni kujua kwamba mafanikio ya haraka sana kama inavyotegemewa na wengi huwa hayapo na pia hata kama utasema ufanye biashara mwenyewe ili kufanikiwa haraka utahitaji kuweka kazi kubwa sana kufikia mafanikio lakini hata hivyo bado haitachukua muda mfupi kama wengi wanavyotegemea, inaweza kukuchukua hata miaka mitano au zaidi ya kuhangaika sana kabla ya kuanza kuyaona mafanikio unayoyatarajia.

– Hata hivyo katika vikundi hivi vya kijamii kuna kitu kimoja muhimu sana kinachoweza kuwasaidia watu kuwa na mafanikio ya uhakika na ya kudumu kwa vizazi na vizazi ikiwa utamaduni huo utapewa kipaumbele.

– Utamaduni huu unajengwa na jamii yetu kwamba wale ambao tayari wameshafanikiwa wanawashika mkono na kuwafundisha njia za mafanikio kupitia uzoefu wao na kufanya nao kazi watu wa ndani ya koo na familia na jamii kwa ujumla wale ambao hawajafanikiwa. Njia hii sio rahisi sana kwani inahitaji upendo wa hali ya juu sana na kuvumiliana baina ya wanaukoo na wanafamilia au wanajamii kwa ujumla lakini ni njia yenye nguvu sana katika kuisaidia jamii ya watu husika kupiga hatua kubwa kimaendeleo na kudhibiti kabisa umaskini.

– Kukiwepo kuhamashishana na kuwekeana malengo kijamii, kiukoo na kifamilia basi inaweza kusaidia kujenga utamaduni bora sana ambao utakuja kujivuniwa sana miaka ya baadaye. Changamoto za njia hii zinachangiwa sana na asili ya binadamu ya kuwa na wivu na ubinafsi miongoni mwa wanajamii na tabia ya kupenda mashindano na ukuu ambayo ipo katika kila jamii duniani. Lakini kwa baadhi ya jamii zinazoweza kukabiliana na hali hiyo huweza kupiga hatua kubwa sana.

– Jambo la msingi la kufahamu ni kwamba mtu kuwa na fedha ni kwa sababu kuna siri anazozijua na mara nyingi ni tabia zilizojengeka ndani yake anazoziishi ambazo ndio msingi wa mafanikio yake. Hivyo mtu huyo mwenye mafanikio anapomchukua mtu na kuishi naye kwa muda akamfundisha hayo kwa kuona na kuiga na yeye akaondoka kwenda kuanzisha biashara yake atapiga hatua kubwa pia. Ukifuatilia hata matajiri wengi wa sasa utakuta kuna namna walipata hamasa kutoka kwa wengine waliowaona au kufanya kazi kwao na kisha kuondoka na kwenda kupambana kama walivyokuwa wakiona bosi wake au mtu mwingine waliomfahamu akipambana na kuiga baadhi ya mambo yale na kupiga hatua. Japo sio kila mtu anaweza kuwa na morali au ari ya maendeleo lakini hii bado itasaidia wengi sana waliolala.

– Utamaduni huu wa kushikana mikono unakwenda mpaka kwenye maeneo mengine yenye fursa muhimu kama vile ajira na vipaji vingine. Hivyo kunakuwa na utamaduni wa kumchukua mtu kijijini au mahali pengine na kumpambania naye aweze kupiga hatua kisha naye anapewa deni la kumchukua mwingine na kumpania mpaka apige hatua. Kwa namna hii jamii huweza kufika mbali sana kimaendeleo kwa kusimama kwenye msimamo huu wa upendo baina ya wanafamilia, wanajamii na wanaukoo kwa ujumla. Muhimu kukumbuka ni kwamba kila mtu anaweza kufanikiwa zaidi kadiri anavyowasaidia watu wengi zaidi kufanikiwa. Fursa huwa hazina kikomo.

Una maoni gani?

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *