UTAFITI NA UFAHAMU ZAIDI JUU YA KOO ZA KICHAGGA.

– Kazi ya kufanya utafiti na kufahamu zaidi kuhusu koo mbalimbali za kichagga ni kazi kubwa sana na inahusisha mambo mengi sana kwa sababu ya uwingi na upana wa koo zenyewe. Kazi hii pia ina changamoto ya uhaba wa taarifa hususan inapokuwa sio jumuishi kwa kila mwenye uelewa fulani.

– Lakini habari njema ni kwamba kwa kujaribu kuifanya kuwa jumuishi kwa kutumia majukwaa ya mtandaoni yenye wafuasi wengi imesaidia kuona wazi kwamba kuna uwezekano wa kupata taarifa nyingi na zinazoweza kuchangia katika kurahisisha zoezi zima la utafiti huu. Vipo vitabu mbalimbali tulivyosoma vimezungumzia kuhusu koo mbalimbali lakini hazijaweza kufikia hata nusu yake na pia kuna mambo mengi muhimu juu ya koo hizi ambayo hayajazungumziwa kwa sababu kitabu hakiwezi kuandika kila kitu.

– Lakini hapa tuna uhuru wa kujadili kila kitu kwa mapana kadiri itakavyowezekana bila kuhofia ufinyu wa kurasa na kisha kujumuisha taarifa hizi na utafiti unaoendelea kisha kuzihifadhi kwenye tovuti yetu ya www.wachagga.com kwa manufaa mbalimbali. Hivyo sasa kila siku tutakuwa tunajadili ukoo mmojawapo ambapo tutahitaji mchango wa kila mtu kuzungumzia kile anachofahamu kuhusu ukoo husika hususan wahusika wenyewe. Taarifa hizo zitachanganywa na taarifa nyingine za utafiti unaoendelea kiha kuchuja na kupata taarifa sahihi zaidi kuhusu ukoo husika au familia husika.

– Tutakuwa tunaweka ukoo mmoja hapa na kutoa maelezo mafupi kuhusiana na ukoo husika na kisha watu wataendelea kuzungumza zaidi kile wanachofahamu kuhusu ukoo huo. Utasema kama ukoo husika unapatikana kwenye kijiji chako na unafahamu nini kuhusu ukoo huo, ni watu wa aina gani na wana ushirikiano kiasi gani.

– Tunafahamu kwamba koo za kichagga zina matawi mengi maeneo mengine ya uchaggani hivyo pia kwa wale wenye kufahamu ni lini tawi husika lilihama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine na sababu iliyopelekea hilo. Kwa wenye kufahamu pia anaweza kusaidia kujua ni mzee gani wa zamani zaidi wa ukoo husika anayekumbukwa na yuko wapi au alifariki mwaka gani. Ikiwa kuna chanzo chochote cha taarifa juu ya ukoo husika unaweza kushirikisha hapa au kusoma mwenyewe na kuandika hapa kile ulichoweza kufahamu.

– Tafadhali usiwe tu mlaji bali jitahidi nawe kushirikisha uzoefu wako wowote unaoufahamu kuhusu ukoo husika. Na kwa wale wenye ukoo ni fursa nzuri ya kufahamu mengi juu ya ukoo wako lakini pia ni fursa ya wewe kutoa taarifa sahihi na muhimu juu ya ukoo wako ili kulinda taswira yake dhidi ya taarifa nyingine hasi.

Karibuni sana.

Leo Tutaanza na;

UKOO WA KILEO.

– Ukoo wa Kileo ni moja ya koo kubwa na zinazojulikana sana za Wachagga. Huu ni ukoo ambao uko kwa wingi zaidi huko Siha/Sanya Juu kuliko eneo lingine lolote la Uchaggani. Ni ukoo mkongwe sana na mashuhuri ambao umefanikisha mambo mengi katika historia ya Wachagga.

– Kutoka katika historia inasemekana kwamba wachagga wa ukoo wa Kileo wa huko Siha/Sanya Juu walikuwa ni wataalamu mainjinia(wahandisi) wa kutengeneza mifereji maarufu kwa kiingereza kama (furrow surveyors).

– Kutoka kwenye historia pia inafahamika kwamba mtawala wa mwanzoni zaidi wa eneo la Siha/Sanya Juu aliyeitwa Mangi Mndusio alitokea kwenye ukoo wa Kileo na aliishi katika kijiji ambacho leo hii ni kijiji cha Samaki Maini. Japo baadaye alikuja kuuawa na watu wa ukoo wa Orio/Urio lakini mwishoni mwa karne ya kiti cha umangi wa Siha Sanya Juu kilirudi tena kwenye ukoo wa Kileo kupitia Mangi Sinare ambaye aliungwa mkono na baba mkwe wake aliyeitwa Kirema kutokea kwenye ukoo wa Orio/Urio.

– Utawala wa Siha uliendelea kwa Mangi Jacobus Sinare mtoto wa Mangi Sinare kutoka kwenye ukoo wa Kileo kabla utawala wa himaya ya umangi Siha haijachukuliwa na kutawaliwa na ukoo wa Mushi kutoka Machame mpaka mwisho wa umangi.

– Hata hivyo Mangi wa karne ya 21 wa Siha/Sanya Mangi Godfriend Kileo mtoto wa Mangi Jacobus Kileo ambaye yupo mpaka sasa alirudisha tena kiti cha umangi kwenye ukoo wa Kileo mwezi Desemba 2021.

– Mbali na Siha/Sanya Juu ukoo wa Kileo unapatikana pia maeneo mengi ya Uchaggani pia ikiwemo mbalimbali ya Machame, ukoo wa Kileo unapatikana pia Kibosho hasa katika kijiji cha Kirima Kati Masoka, ukoo wa Kileo unapatikana pia Uru maeneo ya Shimbwe n.k., Inasemekana kwamba ukoo wa Kileo unapatikana pia Mbokomu.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Kileo?

2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Kileo?

3. Kama wewe ni wa ukoo wa Kileo una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

4. Bado mna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Kileo?

Karibuni sana kwa Mchango zaidi au Maswali.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *