UCHUMBA MPAKA NDOA KWA WACHAGGA.

2. NDOA.

SEHEMU YA 1.

Baada ya taratibu zote za mambo ya uchumba na ndugu wote wa bibi harusi wanaopaswa kupewa kile wanachostahili kumalizika sasa umefika wakati wa bwana harusi wa kichagga kumdai ili kukabidhiwa bibi harusi wake. Tangazo la ndoa hupelekwa kwa wazazi wa bibi harusi kupitia Mkara(mdhamini) kwenda kwa baba wa binti akiambatana na debe mbili za mbege, mbuzi mmoja na kondoo, ambapo mbuzi huyo huitwa, “Mburu ya wamae o mana na ya makumbi” ikimamaanisha mbuzi ya mama wa mtoto na ya majembe. Kondoo huyo anatakiwa kuwa kondoo mzuri na msafi ambaye hajawahi kuzaa. Kuzunguka kwenye shingo ya kondoo huyo hufungwa majani ya mti ya masale ikiwa ni kama alama ya neem ana baraka. Bibi zake na bibi harusi kama wako hai hutakiwa kupewa kila mmoja kondoo.

– Siku ya harusi ndugu, jamaa na marafiki za bibi harusi hukusanyika pamoja. Kisha inapofika mchana, “Mkara” akiwa ameongozana na bwana harusi na ndugu zake bwana harusi huenda kuwafuata. Baba wa bibi harusi anakutana nao na kuwauliza, “Mnatafuta nini?” nao humjibu “Tunatafuta ng’ombe jike kijana”. Naye huwauliza, “Wa namna gani?”, nao humjibu “Anayeelekea kufanana kama mtoto”, naye huwauliza, “Kwani yuko kwangu?” na wao humjibu, “Tunafahamu kwamba yuko kwako”. Baada ya kujibiwa hivyo baba wa bibi harusi anawageukia ndugu zake na kuwaeleza hayo. Kisha wanakubaliana na ndugu zake na zoezi linalofuata ni la kuhesabiana mahari yanayolipwa na yale yatakayokuja kulipwa baadaye.

– Kisha “Mkara” hutengeneza mafungu matatu ya vijiti ambavyo ndivyo vinavyowakilisha makundi matatu ya mahari. Fungu la kwanza la vijiti linawakilisha zawadi za pombe ambazo zimeshatumika ambavyo anavikabidhi kwa mikono yake mwenyewe, fungu la pili linawakilisha mahari ya mbege na vyakula ambayo bado haijatolewa na fungu la tatu la vijiti linawakilisha mahari ya mifugo ambayo itakuja kutolewa baadaye. Fungu la kwanza la vijiti hukabidhiwa kwa baba wa bibi harusi ambaye huchukua na kuwaonyesha ndugu zake na kuwaambia, “Tazama, vijiti hivi ni ushuhuda wa mahari ya kula na kunywa ambayo imeshatolewa na kutumika”. Kisha Mkara anachukua fungu la vijiti linalowakilisha kile ambacho anapaswa kupewa bwana harusi ambacho kiko ndani ya nyumba.

– Hapo ndipo bibi harusi anaitwa kutoka kwenye nyumba aliyomo, kisha mbele za watu wote waliohudhuria harusi hiyo Mkara anawapa maelekezo wote wawili juu ya wajibu wao na majukumu ya kila mmoja kwa mwenzake. Kisha kwa maelekezo kutoka kwa baba wa bibi harusi, mtoto wa kiume wa kaka yake husema maneno ya mwisho ya baba wa bibi harusi kwa binti yake huyo ambaye ndio anaondoka zake kuelekea kwa mume.

– Baada ya hapo Mkara wa kike anamrushia bibi harusi nguo mpya, ambaye anaacha nguo zake za zamani kwa mama yake kama “salamu za mwisho” na kisha Mkara wa kike anambeba bibi harusi mgongoni kumpeleka nyumbani kwa mume wake. Ndugu na marafiki wa bibi harusi wanaonekana kuomboleza huku wakijifanya kuzuia njia bibi harusi asiondoke na hivyo Mkara wa kiume anawagawia zawadi njiani pamoja na vijiti vinavyowakilisha zawadi watakazopewa baadaye ili wapishe njia ya bibi harusi kupelekwa kwa mume wake. Wakati mwingine bibi harusi naye alijifanya kulia wakati amebebwa kupelekwa kwa mume wake akiashiria kama vile alikuwa hataki bali analazimishwa kuondoka kwao ili akaolewe kama ishara ya kuonyesha upendo na kujali ndugu zake.

– Inasemekana kwamba katika karne zilizopita huko nyuma zaidi kuna wakati katika baadhi ya maeneo ya Uchagga bibi harusi alitekwa kabisa na watu wa kwao kutaka kumrudisha nyumbani na hata kupelekea mapigano makali baina ya ndugu wa pande zote mbili kiasi cha kupelekea askari wa Mangi kuja kuingilia na kuhakikisha mambo yanakwenda kama yalivyopagwa. Bibi harusi alifikishwa kwenye nyumba ya kijana anayemuoa na mara nyingi nyumba ya mama ya kijana au tuseme nyumba ya mama mkwe wake, binti alipokelewa na mama mkwe ambaye alimpaka mafuta na kuanza kuwa mwangalizi wake kuanzia siku hiyo.

– Siku chache baadaye baba wa bwana harusi alitisha madebe mawili makubwa ya mbege ili kuwaalika ndugu zake, wanaukoo na marafiki. Hapo ndipo harusi ilitangazwa rasmi na walialikwa ili kusaidia katika kuandaa sherehe ambayo ilikuwa kama ni sherehe ya harusi ya pili. Ndugu wote walioalikwa walichangia kiasi cha ulezi kwa ajili ya kutengeneza mbege nyingi sana itakayotumika kwenye harusi ya upande wa bwana harusi. Pombe hii iliitwa kwa jina la, “Wari wo shanye”, ikimaanisha “pombe shirikishi”. Pombe hii ilinywewa na ndugu na marafiki huku madebe manne yakitumwa kwa baba wa bibi harusi ili kumwomba baraka, kisha debe la tano lilitumwa kwa mama wa bibi harusi.

ITAENDELEA.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *