UKOO WA URIO/ORIO.

– Ukoo wa Urio/Orio ni kati ya koo kubwa, kongwe na maarufu sana miongoni mwa wachagga. Kwa uchaggani ukoo wa Urio/Orio unaaminika kwamba ulianzia Sanya Juu na uliweza kutoa watu mashuhuri katika historia kama Mzee Msanya ambaye anasemekana alihamia Meru kwa muda na kisha kurudi Sanya Juu na baadaye vizazi vyake kusambaa maeneo mengine ya Uchaggani. Baadhi ya waandishi wanaamini kwamba hata mto Sanya umeitwa kwa jina la Msanya au mtoto wake Yansanya kutoka katika ukoo huu wa Urio/Orio.

– Katika eneo la Sanya juu ukoo wa Urio/Orio waliposhuka kutokea maeneo ya ukanda wa juu sana waliweka makazi yao katika kijiji cha Samake ya zamani maarufu kwa sasa kama kijiji cha Samaki Maini. Kwa nyakati tofauti waliweza kutoa watawala wa eneo hili na walionekana kuwa ni watu wenye uwezo mkubwa kiutawala na waliokuwa matajiri wakubwa pia. Mwishoni walikuja kuwa ni watawala wa eneo la kijiji cha Samaki Maini pekee wakati wa utawala wa Mangi Lilio na mwishowe mtoto wa Lilio aliyeitwa Mangi Maimbe.

– Wachagga wa ukoo wa Urio/Orio walisambaa maeneo mengine mengi ya Uchagga na kila walipokwenda waliweza kuwa mashuhuri na kuendelea kuwa matajiri na wakati mwingine kufanikiwa kukalia kiti cha utawala. Matawi ya ukoo wa Urio/Orio yaliweza kusambaa kuanzia Kibosho walikojenga ushawishi mkubwa sana pia, Mbokomu ambako walikuwa pia na ushawishi, Mwika ambako walifanikiwa kukalia kiti cha utawala na Keni, Rombo ambapo waliendelea kuwa mashuhuri sana.

– Ukoo wa Urio/Orio pia wanapatikana kwa wingi Uru, Old Moshi, Kirua Vunjo, Marangu pamoja na Mashati, Rombo. Ukoo wa Urio/Orio wanapatikana kwa wingi sana Meru ambapo inaaminika ni tawi hilo hilo lililoanzia maeneo ya Sanya Juu.

Karibu kwa mchango wa mawazo zaidi juu ya ukoo huu mashuhuri wa Urio/Orio. Tunawashukuru sana wote waliotoa mchango wa mawazo jana kuhusiana na ukoo wa Kileo hususan ndugu wahusika wa ukoo wenyewe. Tumeweza kufahamu mambo muhimu na ya ndani sana juu ya ukoo wa Kileo, tutajumuisha taarifa hizo muhimu kwenye tafiti juu ya ukoo wa Kileo. Hivyo sasa leo tunaomba mchango wowote wa mawazo na maoni juu ya ukoo huu wa Urio/Orio.

Changia chochote juu ya ukoo huu, hata kama tu kijijini kwako kuna familia ya ukoo wa Urio/Orio unaweza tu kukitaja hapa kijiji hicho, kwa Mfano kwa kusema tu hata kijiji cha Uswaa, Machame kuna ukoo wa Urio/Orio inatosha. Au unaweza kutoa maelezo zaidi pia ni sawa. Tunatamani hata kufahamu tu maeneo au vijiji ambavyo kuna familia za ukoo huu wa Urio/Orio.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Urio/Orio?

2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Urio/Orio?

3. Kama wewe ni wa ukoo wa Urio/Orio una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

4. Bado mna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Urio/Orio?

Karibuni sana kwa Mchango zaidi au Maswali.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

You may also like...

Popular Posts

1 Comment

  1. patrick ernest says:

    Mimi ni Urio ya Meru lakini Babu alihamia kutoka Masama Mula na kitongoji anapoishi kimepatiwa jina la Mula kutokana na kuwa maarufu sana na hakutaka kupoteza asili yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *