UMEWAHI KUOGOPA KUJITAMBULISHA KUWA WEWE NI MCHAGGA?

– Wakati mwingine kuwa Mchagga sio habari njema sana kwa baadhi ya watu ambao wana mitazamo mbalimbali kuhusu wachagga. Hii ni kwa sababu Wachagga wamekuwa wakitazamwa kwa namna ya tofauti na baadhi ya watu wa jamii nyingine kadiri ya namna watu hao walivyoaminishwa kuhusu wachagga.

– Kilichonisukuma kuandika hii makala ni rafiki yangu mmoja wa kike aliyeniambia kwamba yeye hakuwahi kujitambulisha popote kwamba yeye ni mchagga. Anasema kwamba alijaribu sana kukwepa kujitambulisha kuwa ni mchagga kutokana na sifa nyingi mbaya zilizokuwa zinasemwa kuhusu wachagga kwa ujumla. Yeye anasema amekuwa akiogopa kujitambulisha yeye ni mchagga kwa kuona aibu juu ya yale yanayosemwa kuhusu wachagga.

– Ukweli hata mimi nilipokutana naye mwanzoni japo nilijuwa kwamba yeye ni mchagga na hata kumwambia kabisa yeye ni mchagga wa sehemu gani lakini alinisisitiza kwamba yeye ni mmasai japo kweli ana asili ya uchagga pia. Mwisho alishindwa kunidanganya kwa kushindwa kujibu maswali mengi niliyomuuliza na hivyo kukiri kwamba yeye ni mchagga lakini huwa hapendi kujitambulisha hivyo. Badala yake hupenda kukwepa kujulikana ni mchagga japo mara nyingine watu humshitukia kuwa yeye ni mchagga.

– Hali hii naamini imeshawakuta watu wengi na pengine hata kwa makabila mengine lakini kwa Tanzania wachagga wamekuwa wahanga zaidi kuliko watu wengine tangu miaka mingi. Na hii sio tu kujitambulisha kama mchagga lakini hata kutaja jina la ukoo kama vile Swai, Tarimo, Massawe, Urio, Kimaro, Lyimo n.k., imekuwa ni jambo linalokwepwa na baadhi ya watu hususan kwenye baadhi ya mazingira. Baadhi ya watu wamekuwa wakiogopa kwa kusikia tu au kuhisi kwamba mchagga anaweza kubaguliwa lakini wapo baadhi wengine wamewahi kubaguliwa kweli kwa sababu ni wachagga.

– Lakini pia wengine ni kwa sababu wamekuwa wakijisikia aibu kujulikana ni wachagga kwa kuamini kwamba wachagga wanaaminika kuwa watu wabaya hivyo akijulikana ni mchagga itakuwa ni aibu mbele za watu hao. Watu wengine wamekuwa wakitamani hata kuomba msamaha kwa kuwa wao ni wachagga, yaani wasamehewa kwa ubaya ambao unasemekana juu yao.

– Ni kweli kwamba wachagga wamekuwa wakihusishwa na tabia zisizovutia na hasa kwenye majukwaa ya kisiasa yenye lengo na manufaa ya kisisiasa. Kauli kama wachagga ni wezi, ni wajanja wajanja, wana tamaa ya pesa zimeanza kuzungumzwa tangu awamu ya kwanza na zimekuwa hata ni agenda zinazosukumwa mbele na wanasiasa kwa malengo ya kisiasa na hata kwa sababu nyingine pia.

– Kuna mzee mmoja mwenyeji wa Dar es Salaam siku moja alikuwa ananisumulia kwamba hata kabla ya uhuru wa Tanganyika jinsi wachagga walivyokuwa wanapigwa vita Dar es Salaam na serikali ya waingereza. Yule Mzee alikuwa anaitwa Mzee Maskini aliniambia serikali ya Waingereza iliwaambia kwamba watakapomwona mchagga yeyote Dar es Salaam wamripoti mara moja kwani wachagga ni watu hatari na wabaya sana hivyo wakimwacha atawamaliza. Kwa maana hivyo wachagga wengi waliokuwa wanaingia Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli zao binafsi walikuwa wanapakiwa kwenye treni na kurudishwa Moshi.

– Hili likaendelea kwenye awamu ya kwanza ambapo wachagga walipewa majina mengi yasiyofaa kama vile wezi na watu wenye tamaa ya fedha na wabinafsi au wana ukabila. Hili halikufanywa siri bali lilizunguzwa na wanasiasa kwenye majukwaa na kufanya wachagga kuonekana ni watu hatari na wa tofuati. Tuliweza kuona hata kwenye awamu ya tano jinsi wachagga walivyochukuliwa kwa mtazamo wa tofauti kabisa na hata mwanasiasa kusimama jukwaani na kutamka wazi kwamba watu hao sio watu wa kuwaamini na kuwapa dhamana ya kushika fedha baada ya malalamiko kwamba kuna mwanamke wa kichagga amepewa nafasi ya kuwa mweka hazina wa kikundi fulani na kupotea na fedha za watu.

– Tunafahamu kwamba hata katika awamu ya kwanza ya uongozi watu walibaguliwa kwenye fursa za elimu kwa sababu tu wao ni wachagga, japo iliambatana na hoja nyingi zisizo na mashiko. Pengine ubaguzi wa namna hii ulichangia kuwafanya wachagga kuendeleza hofu hii ya kujitambulisha kuwa ni wachagga.

– Hata propaganda nyingine za kisiasa zimekuwa zikivihusisha baadhi ya vyama vya siasa kwamba ni vya wachagga na viko kwa ajili ya kupigania maslahi ya wachagga kwa lengo la kuvipunguzia ushawishi kutokana na watu wengi kuamini kwamba wachagga ni wabinafsi na wakabila. Propaganda hizo zikiwa na lengo la kuvifanya vionekane havifai kwa sababu kumbe viko kwa maslahi ya wachagga ambao ni wakabila, wabinafsi na wajanja wajanja sana.

– Mitazamo hii imewafanya wachagga wengi kujihisi hawako sahihi na wanapaswa hata kuomba msamaha kwa hayo yanayosemwa juu yao. Lakini wengine wamekuwa tu wakiogopa kukosa au kupoteza fursa fulani ikiwa watajulikana kwamba wao ni wachagga. Hata mimi binafsi hofu hii imewahi kunitokea siku za nyuma lakini baadaye nikaona sio kitu kizuri wala sihitaji kujificha sana isipokuwa tu kama kuna hatari kubwa sana. Hata hivyo bado niliweza kubainika na kujulikana na hakukuniacha salama pia kwa wenye imani hiyo.

– Ukweli ni kwamba wachagga hawana shida yoyote na hawapaswi kuogopa wala kujali chochote juu ya wao kuwa wachagga kwani kinachosemwa kuhusu wao ni mitazamo ya watu iliyochangiwa na propaganda zenye malengo mbalimbali. Kama suala ni tabia kila jamii ina tabia zake tofauti tofauti ambazo ni nzuri na mbaya kadiri ya maadili ya jamii husika yanavyoweza kuzihukumu. Kama watu wanaamini wachagga ni tatizo hilo sio tatizo la wachagga bali ni mitazamo yao. Na kama kuna mchagga amefanya jambo baya basi haipaswi kuhusisha jamii nzima kwani hakuna sehemu duniani kusikofanyika mambo hayo.

– Hata hivyo wewe kama mchagga hupaswi kuwa mnyonge kwa kutengenezewa hatia feki kwani kwa kufanya hivyo unaipa nguvu na kuihalalisha licha ya kutokuwa na uhalali na hivyo unakuwa unajihujumu mwenyewe. Unapaswa kujiamini na kupuuza ili kudhihirisha kwamba ni uzushi na haina nguvu yoyote ili isiweze kutumika dhidi ya wachagga.

– Hii ni kwa sababu mambo yatakapoharibika au kama ambavyo yaliwahi kuharibika kwa kiasi usifikiri wewe kama mchagga utapona kiurahisi. Ikitokea wachagga wanaadhibiwa kwa sababu tu ni wachagga kama ilivyowahi kuonekana wewe kama mchagga haijalishi ni mnyonge au mpole kiasi gani au utajitetea kiasi gani ujue hakuna namna utapona kwani utakuwa umekidhi vigezo vya kuadhibiwa kwa sababu ni mchagga. Hivyo ni jukumu la kila mchagga kusimama imara dhidi ya propaganda za kuhalalisha kwamba wachagga ni watu wabaya na waovu kwa sababu athari zake hazitakuacha salama.

– Lakini pia hakuna haja ya kuogopa sana na kukwepa kujitambulisha kwamba wewe ni mchagga kwa sababu wapo watu pia ambao wanawapenda wachagga kwa sababu ni wachagga. Kuna watu pia wanamheshimu mtu na hata kupenda kufanya naye kazi kwa sababu ni mchagga hivyo kuna upande chanya pia. Japo ni kweli kwamba kuna watu wameapa kwenye maisha yao kwamba hawataoa au kuolewa na mchagga lakini pia kuna watu wameazimia kwenye maisha yao kwamba hawataoa au kuolewa na mtu asiyekuwa mchagga pia.

– Kwa maana hiyo hakuna haja ya kuogopa sana kujitambulisha kuwa mchagga kwani licha ya kuwa na upande hasi lakini kuna upande chanya pia, na bado pia kuna upande wa katikati “neutral” ambao ndio una watu wengi zaidi wasiojali kama wewe ni mchagga au sio mchagga wao kama una vigezo watafanya kazi na wewe. Hivyo hakuna haja ya kuogopa kukosa fursa au kukosa mke au mume kwani kwa kujitambulisha kuwa mchagga utakuta wakati mwingine ndio unakaribisha fursa pia.

– Kiuhalisia mambo haya yakiendelezwa na kukuzwa sana kwa kutumia propaganda hasa za kisiasa huwezi kuwaumiza sana wahusika. Na mara nyingi ni mambo yanayosababishwa na wivu na chuki kwa watu husika ambazo huendelea kupandikizwa kwa watu na kutumiwa kwa malengo ya kisiasa au malengo mengine bila kujali madhara yake.

– Je, umewahi kusita kujitambulisha kuwa ni mchagga eneo fulani kwa kuhofia kukosa fursa fulani au kubaguliwa?

– Je, unaamini kwamba wachagga kweli ni wabaya na wanapaswa kuomba radhi kwa watu wengine kwa ubaya wao huo?

– Je, unaamini kwamba wachagga wanapaswa kubaguliwa na kunyanyaswa kwa sababu wanasababisha uharibifu kwenye jamii?

Karibu kwa Maoni au Maswali.

Ahsanteni sana.

Whatsapp +255 754 584 270

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *