UKOO WA MUNISI/NKYA/NYARI.

– Baadhi ya watu hawajui kwamba Munisi, Nkya na Nyari ni ukoo mmoja licha ya kuonekana kama koo tofauti kwa watu wasiozijua. Hivyo licha ya zile sababu ambazo watu wanasema kuwa ndio chanzo cha utofauti wa ukoo huu uliogawanyika tutaujadili kama ukoo mmoja na wahusika wanaweza kutueleza sababu ya wao kuwa na majina matatu tofauti ya ukoo mmoja. Katika majina matatu tofauti ya ukoo huu, jina kongwe zaidi na pengine linalotumiwa na watu wengi zaidi wa ukoo huu ni Nkya ikifuatiwa na Munisi lakini wapo ambao wanatumia yote kwa pamoja.

– Kutoka kwenye historia ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari ni ukoo mkongwe sana pengine kuliko koo nyingine zote katika Machame ya mashariki na Machame ya magharibi. Hata hivyo kuna nadharia kuu mbili zinazoeleza chanzo cha ukoo huu mkongwe sana Machame na uchaggani kwa ujumla.

– Moja inaeleza kwamba ukoo wa Nkya umetokea kwenye kizazi cha Mashami ambaye alikuwa mtawala wa mwanzoni kabisa Machame na mkongwe zaidi katika historia ya wachagga kwa ujumla ambaye ndiye chanzo cha jina lenyewe Machame. Kwa sababu kama tulivyojifunza kutoka kwenye historia Machame na Mbokomu yalikuwa ndio maeneo ya mwanzoni na makongwe zaidi kukaliwa na wachagga asilia Kilimanjaro. Kwa maana hiyo huyo Mzee Nkya alikuwa ni mtoto wa kiume wa Mangi Mashami.

– Lakini nadharia nyingine kutoka kwa baadhi ya watu wa ukoo wa Nkya wenyewe katikati ya karne ya 19 walidai kwamba Nkya ni ukoo mkongwe kiasi kwamba Nkya ndio umezaa watu wote na sehemu kubwa ya jamii hayo. Nadharia hii inaeleza kwamba hata Mashami mwenyewe ambaye anasemekana kwamba kupitia yeye ndio koo karibu zote za upande wa magharibi na mashariki ya mti Kikafu zimetokea, anatajwa kuwa pia ni mtoto wa Nkya. Nadharia hii inaendelea kueleza kwamba hata sehemu kubwa ya wachagga wa Uru ni kizazi cha Mzee huyu aliyeitwa Nkya ambaye ni mkongwe sana.

– Nadharia hii inaongezewa uzito zaidi na lililokuwa eneo takatifu la kuabudia la wachagga wa ukoo huu wa Nkya lililokuwa linaitwa “Nkukun” katika ukanda wa chini zaidi wa Machame karibu na tambarare upande wa mashariki wa mto Kikafu. Eneo hili la kuabudia la wachagga wa ukoo Nkya lililokuwa ni eneo la Mzee wa ukoo wa Nkya, “Nkukun” ndio eneo lililokuwa na jiwe kubwa zaidi la kuabudia Kilimanjaro nzima likiwa linalingana ukubwa na jiwe la ukoo wa Maanga katika kijiji cha Korini, Mbokomu. Maeneo haya mawili ya kuabudia yaliyokuwa na mawe makubwa zaidi Kilimanjaro ya ukoo wa Nkya Machame na ukoo wa Maanga Mbokomu yalithibitisha pia ukongwe wa wachagga wa maeneo haya Kilimanjaro.

– Ukongwe wa ukoo huu wa Nkya unaosemekana kuzidi ukongwe hata wa Mashami mwenyewe unaendelea kuongezewa nguvu na ukweli kwamba watawala/wamangi wa Machame ambao wanatokea ukoo wa Mushi walikuwa wanafanya tambiko takatifu kila mwaka katika eneo hili la “Nkukun” ambalo lilikuwa ni eneo la kuabudia la ukoo wa Nkya. Hiyo ni kumaanisha kwamba licha ya nadharia niliyoitaja mwanzoni inayoeleza kuwa Mushi na Nkya wote baba yao ni Mashami lakini kitendo cha ukoo wa Mushi kufanya tambiko eneo hili linaweza kuwa ni uthibitisho kwamba Nkya ni kongwe kuliko Mashami mwenyewe na kweli kwamba ndio iliyomzaa Mashami mwenyewe na ndio maana Mushi wanafanya tambiko hapo kumaanisha kwamba hao ni babu zao.

– Ibada hii ya tambiko takatifu la watawala/wamangi wa Machame lilikuwa likiendelea kufanyika eneo hili la “Nkukun” la ukoo wa Nkya mpaka mwanzoni mwa karne ya 20 na liliweza kushuhudiwa hata na mmsionari wa kilutheri Dr. Bruno Guttman ambaye alilielezea kwenye kitabu chake cha “Poetry and Thinking of the Chagga” alichokiandika wakati akiishi Machame kati ya mwaka 1902 mpaka 1909. Eneo hili la “Nkukun” lililopo katika ukanda wa chini ya Machame linasemekana kwamba lilihamishwa kwenye miaka ya katikati ya karne ya 20 na kusogezwa pembeni kupisha ujenzi wa barabara kubwa inayopandisha Machame.

– Ukoo wa Munisi/Nkya/Nyari umekuwa ni ukoo mashuhuri sana na wenye mchango mkubwa sana Machame na wenye kuheshimiwa sana sambamba na ukoo wa Mushi wenyewe. Kwa Machame ukoo wa Nkya ulikuwa ndio ukoo maalum wa kufanya ibada yoyote takatifu ya maombi ya kuiombea nchi dhidi ya janga lolote linalotokea.

– Lakini pia eneo maalum la kufanyia mikutano la wachagga wa ukoo wa Nkya la “Kyalia” Machame Central ndiyo eneo takatifu lililokuwa linatumiwa na wachagga wa koo zote za magharibi na mashariki ya Machame kufanyia jando ya vijana wa kiume kuingia rika la utu uzima. Hii ilipelekea ukoo wa Nkya kuona wao ni sawa na ukoo wa watawala pia kutokana na ushawishi mkubwa na ukongwe waliokuwa nao Kilimanjaro.

-Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari ni ukoo mashuhuri na wenye watu wengi sana ulioenea zaidi mashariki na magharibi ya Machame na kwa kiasi nje ya Machame. Wakitokea katika eneo kongwe na Sienyi na kupandisha mpaka Uswaa na Shari ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari walielkea magharibi na mashariki ya Kikafu. Tawi mojawapo la ukoo wa Nkya walielekea magharibi kuvuka mto Marire na kuweka makazi ya kudumu katika kijiji cha Ngira, Masama huku wengine wakibaki Uswaa tawi kuu lilivuka mto Kikafu na kuweka makazi katika kijiji cha Foo, Machame kabla ya kuelekea magharibi zaidi na kuweka makazi mengine ya kudumu katika kijiji cha Nkuu, Machame.

– Ukoo wa Nkya unapatikana kwa kiasi huko katika himaya ya umangi Siha/Sanya juu.

– Uko wa Nkya unapatikana kwa kiasi huko Meru pia.

– Ukoo wa Nkya/Muni/Nyari unapatikana kwa kiasi huko Lukani, Masama magharibi.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Ngira na Sonu, Masama.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Roo, Mudio na Kibohehe, Masama.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Uswaa,Machame.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatikana kwa wingi pia katika kijiji cha Nronga, Machame.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari wanapatikana kwa wingi katika kijiji cha Foo, Machame na vitongoji vyake.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatika kwa wingi snaa katika kijiji cha Nkuu, Machame.

– Ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari unapatikana kwa wingi snaa pia Lyamungo, Machame.

Tunahitaji kupata taarifa zaidi juu ya ukoo huu mongwe sana Kilimanjaro, je nini kilipelekea wakaamua kuwa na majina tofauti tofauti ya ukoo mmoja?

Karibu kwa mchango wa mawazo.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Nkya/Munisi?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani? Wewe ni Nkya/Munisi/Nyari wa kutokea kijiji gani?

5. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

6. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari?

7. Wanawake wa ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari huitwaje?

8. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari?

9. Watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Nkya/Munisi/Nyari?

Karibu kwa Maoni na Maswali.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *