UKOO WA MTUI.

– Ukoo wa Mtui ni ukoo mkongwe sana na uliokuwa mashuhuri sana zamani Uchaggani. Huu ni ukoo mkubwa na maarufu sana katika vijiji vingi vya upande Kaskazini wa himaya ya umangi Marangu. Wachagga wa ukoo wa Mtui walifahamika kwa uwezo mkubwa kiakili, kiuongozi na hata kivita tangu karne nyigi zilizopita huko Uchaggani, Kilimanjaro.

– Makazi ya asili na ya mwanzoni kabisa ya ukoo wa Mtui ni katika kijiji cha Mshiri, Marangu japo hata hivyo baadaye walisambaa zaidi na kuenea zaidi katika vijiji vya upande wa Kaskazini magharibi ya Marangu. Hivyo hata sasa licha ya chimbuko lao kuwa katika kijiji cha Mshiri, Marangu lakini ukoo huu wa Mtui unapatikana kwa wingi pia katika vijiji vingine.

– Kutoka kwenye historia ukoo wa Mtui walikuwa ndio watawala wa eneo la Mshiri, Marangu na walikuwa na nguvu kubwa sana kiuchumi na hata kijeshi. Ukoo huu wa Mtui ndio ukoo unaotambuliwa na historia kuwa ndio wachagga wa mwanzoni zaidi kuanzisha utawala na serikali inayotoza kodi ili kuimarisha ulinzi sambamba na huduma nyingine za kijamii.

– Mtawala wa mwanzoni zaidi anayefahamika na historia kutoka kwenye ukoo huu wa Mtui aliyeishi pengine zaidi ya miaka 400 iliyopita mpaka sasa aliitwa “Kilaweso”. Huyu ndiye mtawala wa mwanzoni zaidi kuanzisha mfumo wa kutoza kodi ili kuimarisha ulinzi katika eneo hilo na wachagga wote wa eneo hilo kukaa chini ya utawala wake.

– Ndani ya ukoo wa Mtui ndipo kulikuwa na hadithi maarufu ya kichagga ya zamani(Chagga legendary story) ya konokono aliyekuwa ana uwezo wa kufufua watu ambapo inasemekana alikuwa anarudisha kuwa hai wanajeshi wa ukoo wa Mtui waliokuwa wanafia vitani na hivyo kupelekea Mshiri kuwa ngome imara sana isiyoweza kutikishwa na yeyote. Wakati wa utawala wa Mmori aliyekuja baadaye baada ya utawala Kilaweso wachagga wa ukoo wa Lyimo walijaribu kuitikisa Mshiri lakini waliishia kushindwa vibaya kiasi hata cha kunyang’anywa eneo la Lyamrakana walilokuwa wameliteka kutoka kwa wakina Mboro na kuondolewa kabisa hapo Lyamrakana ambayo ilichukuliwa na ukoo wa Mtui na wao kufukuzwa kabisa na kukimbilia upande wa magharibi wa mto Moonjo.

– Hata hivyo wakati wa utawala wa Mawache Mshiri wachagga wa ukoo wa Lyimo waliweza kutumia mbinu za ujanja na udanganyifu wakafanikiwa kuwaangusha na kuwaadhoofisha wachagga wa ukoo wa Mtui na hata kufanikiwa kurudisha eneo la Lyamrakana mikononi mwao. Wachagga wa ukoo wa Mtui licha ya kuwa na uwezo mkubwa kiakili na muonekana murua waliendelea kudhibitiwa na hivyo kutoweza kurudi katika umahiri wao wa mwanzoni.

– Mchagga mwingine mashuhuri ambaye alikuwa na uwezo wa tofauti kutoka kwenye ukoo wa Mtui aliitwa Ndemasiungi katika kipindi cha utawala wa Mangi Ndegoruo Marealle. Lakini pia mwanahistoria msomi wa kwanza katika historia ya wachagga, Kilimanjaro alitokea kwenye ukoo huu wa Mtui katika kijiji cha Mshiri na aliitwa Nathaniel. Nathanieli Mtui ni mchagga mbobezi wa historia aliyetusaidia kutafuta na kuhifadhi sehemu kubwa sana ya historia za zamani sana za wachagga Kilimanjaro.

– Nathanieli Mtui ambaye alikuwa na uwezo mkubwa sana kiakili akiwa ni mmoja kati ya watu wa mwanzoni sana kufundisha katika chuo cha ualimu Marangu alifanya utafiti mkubwa na wa kina Uchaggani kuanzia magharibi Siha/Sanya Juu mpaka mashariki Usseri, Rombo na tafiti zake zimesaidia waandishi wengi sana. Nathanieli mwenyewe ambaye alizaliwa mwaka 1892 kwa sababu pengine za kisiasa aliuawa mwaka 1927 kijijini mwake huko Mshiri, Marangu.

– Sambamba na uwezo mkubwa kiakili wachagga wa ukoo wa Mtui wanasemekana kwamba walikuwa ni wenye muonekana maridadi na wenye kung’aa sana.

– Ukoo wa Mtui umeendelea kutoa watu wengine wengi mashuhuri katika historia na hata mpaka sasa ambao wanafanya vizuri sana maeneo mbalimbali. Hata hivyo tunahitaji kupata taarifa zaidi na mengi ya kuongezea katika tafiti kuhusiana na ukoo huu mkongwe na uliokuwa na nguvu kubwa sana na umashuhuri mkubwa wa Mtui.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Mshiri, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa wingi sana pia katika kijiji cha Mmbahe, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa wingi katika kijiji cha Ashira, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa wingi katika kijiji cha Komela, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa wingi katika kijiji Lyasongoro, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa kiasi pia katika kijiji cha Arisi, Marangu.

– Ukoo wa Mtui wanapatikana kwa uchache pia kwenye baadhi ya vijiji vya Mamba.

Karibu kwa mchango zaidi wa mawazo kuhusiana na ukoo mashuhuri wa Mtui.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mtui?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Mtui?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mtui?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Mtui una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani? Wewe ni Mtui wa kutokea kijiji gani?

5. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Mtui kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

6. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mtui?

7. Wanawake wa ukoo wa Mtui huitwaje?

8. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Mtui?

9. Watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Mtui?

Karibu kwa Maoni na Maswali.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *