KURUDISHA NA KUDUMISHA UKUU NA UIMARA WA WACHAGGA KUPITIA KOO.

Tunapozungumzia Uimara wa Wachagga Watu Wengi Wana Mtazamo wa Uimara wa Kiuchumi Zaidi au Vitu Vinavyoonekana na Kushikika. Lakini Katika Uhalisia Uimara Wetu Sio Maendeleo Ya Kiuchumi Moja Kwa Moja, Maendeleo Ya Kiuchumi ni Matokeo Ya Uimara Katika Maeneo Mengine Ambayo Hayaonekani Kwa Macho Wala Kushikika.

Kitu Kikubwa Sana Katika Kujenga Uimara Utakaoleta Ufahari Kama Jamii ni Kujitambua, Kutambua Utambulisho Wetu na Yapi Muhimu Zaidi Kwetu Yanayostahili Kupewa Kipaumbele. Kujitambua ni Kuweza Kujifahamu Kwa Kina Kama Jamii, Kwamba Tumetoka Wapi, Tuko Wapi Sasa na Tunapanga Kwenda Wapi.

Kuna Mambo Ambayo Yakipewa Kipaumbele Katika Jamii Yetu Yanaweza Kuchochea Kutufikisha Mbali Sana Kama Jamii. Lakini Kwa Bahati Mbaya Hakuna Mamlaka Yoyote Ambayo Iko Kisheria au Hata Ya Kiroho Ambayo Inahusika Moja kwa Moja Kusukuma Mbele Agenda Yoyote Yenye Maslahi Ya Moja Kwa Moja Kwa Wachagga Kama Jamii.

Hata Hivyo, Katika Hilo Bado Kuna Tumaini Kubwa Sana Ambalo Aidha Hatujaliona au Tunalipuuza Ambalo Linaweza Kuwa na Nguvu Kubwa Ya Kusimama Kama Mamlaka Ya Kusimamia Chochote Tunachoweza Kupanga kwa Uhakika na Kwa Viwango Bora Kuliko Hata Mamlaka za Kiserikali na za Kiroho.

Mamlaka Hizi ni Mamlaka za Koo. Kwa Wachagga Kwa Miaka Ya Zamani Hata Kabla Taasisi za Umangi Hazijajengeka na Kuwa na Nguvu, Koo Ndizo Zilizokuwa na Nguvu Kwa Watu na Hata Sheria na Taratibu Nyingine Nyingi za Kufuata Zilikuwa Zinatoka Kwenye Koo. Wazee wa Koo Waliheshimiwa sana na Kusikilizwa Kwenye Maamuzi Ya Mwisho Ya Katika Kila Kitu. Sote Tumeona Kupitia Historia Jinsi Koo Zilivyokuwa na Umoja na Mshikamano Katika Kupambania Suala Zima La Utawala.

Koo Ziliendelea Kuwa na Nguvu Hata Baada Ya Taasisi za Umangi Kuimarika na Bado Mambo Mengi Sana Yalikuwa Yanafanyika Kupitia Koo na Kumalizika Huko. Sote Tunajua Kwamba Ukoo ni Familia Kubwa na Siku Zote Familia Zinahitajiana na Kushirikiana Hata Kama Hazina Maelewano.

Kwa Bahati Nzuri, Hata Mpaka Leo Bado Koo Zina Nguvu Sana na Kwa Sehemu Kubwa Zimeendelea Kuwa na Ushirikiano. Hata Yanapotokea Mambo Makubwa Muhimu Yanayoathiri Watu wa Jamii Kama Vile Ugonjwa, Sherehe Kubwa, Kesi Kubwa Mahakamani, Vifo n.k., Tunaona Jinsi Koo Zinavyoshirikiana Kutatua Changamoto Hizo au Kufanikisha Jambo Husika.

Hata Zamani Wakati Chama cha Kisiasa cha Wachagga Wahafidhina cha Kilimanjaro Chagga Citizens Union (KCCU) Kinajaribu Kupambania Kufanikisha Kuwa na Taifa La Wachagga, Katika Sera na Mipango Yao Walikuwa Wameazimia Zaidi Kuimarisha Jamii Ya Wachagga Kiuchumi na Kimaadili Kupitia Mamlaka za Koo.Watu Ukoo Mmoja Wanafahamiana Kiundani na Wanafahamu Uimara na Udhaifu Wao, Pia Wanafahamu Historia Ya Ndani Zaidi Ya Familia za Ukoo Husika na Hivyo ni Rahisi Hata Kuweza Kufahamu Jinsi Watakavyoweza Kufanikisha Maazimio Yao.

Hivyo ni Rahisi Kusukuma Agenda Nyingi za Jamii Ya Wachagga Kupitia Koo na Zikawa na Nguvu Katika Utekelezaji Kuliko Kupitia Chombo Chochote Cha Kisheria. Na Kwa Bahati Nzuri Koo Tayari Zipo na Nyingine Zina Mamlaka Imara Sana, na Sio Kitu Cha Kuanzisha au Kuunda Upya.

Muhimu ni Kuhimiza Uimarishwaji wa Mamlaka Hizi za Koo Kwa Maslahi Ya Maendeleo Ya Koo Hizi Husika. Tunaweza Kutengeneza Ushindani Wenye Afya Baina Ya Koo Zote Ambao Utachochea Mshikamano Zaidi na Ushirikiano wa Wachagga wa Ukoo Husika Katika Kutekeleza Agenda Mbalimbali Zenye Maslahi Mapana Kwa Wachagga.

Kama Ukoo ni Mkubwa Sana au Kuna Uhasama na Kutoelewana Kwa Kiasi Kikubwa Miongoni Mwa Wanaukoo, Bado Ukoo Unaweza Kugawanywa Katika Matawi Mbalimbali Kupunguza Ukubwa Wake au Kutenganisha Wale Wenye Uhasama Mkubwa Sana Walioshindikana Kupatanishwa. Ukoo Ndio Wenye Jukumu La Kurudisha Familia Zilizopotea au Kufarakana.

Tumeweza Kuona Katika Sherehe za Mwisho wa Mwaka Kwamba Kuna Baadhi Ya Koo Ziko Imara Sana, Zina Uongozi Imara Sana na Zinafanya Vizuri Sana Katika Mambo Yao. Baadhi Ya Koo Zina Ubunifu Mkubwa Sana Katika Kukutana Kwao na Kuna Ushirikiano Madhubuti Sana Miongoni Mwa Wanaukoo. Katika Eneo La Rombo Jambo Hili Liko Katika Viwango Vikubwa Zaidi.

Utekelezaji wa Agenda Zenye Maslahi Mapana Kwa Jamii Ya Wachagga Kwa Ujumla Kupitia Koo Kutasaidia Hata Kuzipunguzia Koo Zenyewe Mizigo Ambayo Imekuwa ni Changamoto Katika Ukoo Husika Kwa Sababu Mbalimbali. Hivyo Koo Zitakuwa Zinafanya Kazi Yenye Maslahi Hata Kwa Ukoo Wenyewe.Ahsanteni.Karibu Kwa Maoni, Maswali au Nyongeza.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *