MAADILI YA JUU ZAIDI KWA WACHAGGA (THE HIGHEST VIRTUE) ILIKUWA NI UJASIRI(BRAVERY).

– Kila jamii au kila nchi duniani kuna thamani inayowekwa kwenye matendo ambayo yamepewa ukuu na utakatifu zaidi kuliko mengine na yanahesabika kuwa ndio matendo mema zaidi(virtues) na kinyume chake ni matendo maovu na ya hovyo(vices).

– Hivyo watu wengi wa jamii husika hupenda kuhusishwa na matendo hayo ili kujenga ushawishi zaidi na hivyo matendo hayo hupewa kipaumbele na matokeo yake ndio huamua hatma ya jamii hiyo. Jamii zilizofanya makubwa zaidi kwa miaka ya zamani kuna matendo yaliyopewa ukuu ambayo yalihesabika ni ya kishujaa iwe ni kwa waaume au wanawake na hivyo kuisaidia jamii husika kujengeka katika eneo husika na kuwa na matokeo makubwa kwa upande huo.

– Wakati mwingine matendo haya makuu huhusishwa na matendo ya mtu anayekubalika zaidi katika jamii husika kwa aidha mambo aliyofanya makubwa sana kwa jamii au nchi husika au alisambaza propaganda nyingi za kuonyesha watu kwamba alikuwa mkuu sana. Vyoyote vile lakini jambo lolote alilofanya mtu huyo huonekana ni lenye maadili na kuhusishwa na ukuu fulani katika jamii husika na watu wengi kutaka kuliiga. Mfano rahisi ni kwenye dini ambapo Mtume au Masihi huonekana ni shujaa sana na kila alilofanya kuwa ndio kipimo cha maadili kwa wengine hata kama kwa mtazamo wa jumla linaonekana ni la kijinga.

– Kwa wachagga ujasiri ulihesabika kuwa ndio tendo kuu lenye heshima kubwa zaidi katika jamii huku kinyume woga ukihesabika kuwa ndio tendo ovu na la hovyo zaidi. Kwa mujibu wa Dr. Bruno Guttman kwenye kitabu chake anasema kwamba Kapteni Merker aliyekuwa gavana wa kijerumani Kilimanjaro kuanzia mwaka 1901 ambaye alijifunza kwa kina pia kuhusu wamasai anasema kwamba wachagga walikuwa na ujasiri wa juu na uimara kuzidi hata wamasai wenyewe.

– Kapteni Merker anasema ujasiri wa wachagga haukuwa ule wa kuthubutu kufanya tendo moja la kijasiri na kisha kukimbia bali ulikuwa ni ule ujasiri imara wenye mizizi imara sana mithili ya mti uliokita mizizi mirefu sana chini ya ardhi na hivyo kuufanya kuwa imara. Merker anasema wachagga walikuwa wakienda vitani wanapigana kwa ujasiri wa hali ya juu na vita hivyo vilikuwa vinapiganwa kwa nguvu na kwa uhakika mithili ya majeshi ya Sparta ya Ugiriki ya kale.

– Hivyo wachagga walijenga uwezo mkubwa kimapambano kiasi kwamba walikidharau sana hata kifo mbele ya vita. Mwanajeshi wa kichagga akiwa kijana kuna nyakati alitamani kwenda kufia vitani au kuja na mafanikio ambayo yatampa heshima kubwa sana kijamii kwa sababu tendo hilo liliambatana na heshima kubwa sana kwake kuliko kubaki nyumbani bila heshima yoyote. Watoto wa kiume nao walianza kujengewa ujasiri tangu wakiwa wadogo na hivyo walitamani kufanikisha mambo makubwa ya kishujaa katika maisha yao.

– Kinyume chake woga ulidharauliwa sana katika nchi ya wachagga na mtu mwoga alihesabika kuwa ni mtu wa hovyo sana. Kwenye historia tumeona jinsi maeneo mbalimbali ya Uchagga watu waoga walivyodharauliwa. Huko Kibosho watu walioonekana kuwa waoga walifukuzwa na kwenda kuishi maeneo ya mbali zaidi. Huko Old Moshi wanaume waoga walizalilishwa kwa kuvalishwa mavazi kike mithili ya kanga na kutishwa mikungu ya ndizi kichwani na kulazimishwa kusalimia watu kama vile wanawake wanavyosalimia na wao kusalimiwa kama wanamwali wa kike kwa salamu ya “Kapfonyi wapora”.

– Kupitia “Poetry and Thinking of the Chagga” Dr. Bruno Guttman anaelezea jinsi askari wa Mangi Mamkinga wa Machame walivyokuwa jasiri na kiasi cha kutoona utofauti wa kuishi na kufa pale ambapo wanapigania jambo lolote lenye maslahi kwa nchi. Wanaume walifananishwa na ngao ya kulinda nchi na sifa hiyo walijivunia kupitia ujasiri mkubwa waliokuwa nao.

– Tumeona hata jinsi Mangi Horombo alivyochukia watu waoga kiasi kwamba kuna kamanda wake ambaye hakuwa na ujasiri wa kutosha kwenda vitani akampa jina la utani “Lyanchonyi” ikimaanisha mtu anayejificha nyuma ngozi ya mbuzi na kuogopa vita. Hivyo ujasiri ilikuwa ndio tendo kuu na lililopewa heshima kubwa zaidi kwa wachagga. Tumeona jinsi Mangi Meli hakuwa na hofu yoyote hata mbele ya kifo zaidi ya kusema tu, “ndama anarudi tumboni kwa mama yake”.

– Maadili haya ya ujasiri wa hali ya juu sana yaliweza kuwapa mafanikio makubwa wachagga kwa sababu licha ya kuzuia jamii nyingine yoyote kuwaondoa kwenye eneo lenye mazingira bora kama Kilimanjaro lakini pia yaliwapa utulivu wa kufanya shughuli nyingine za kiuchumi zilizowawezesha kuimarika na kukua. Kuna jamii nyingi ambazo hazijulikana kabisa kwa sababu zilishapotea kabisa kutokana na kuteketezwa na jamii zilizo na nguvu kwa kushindwa kupambana nazo. Lakini pia ujasiri uliweza kuwaimarisha wachagga kujenga taasisi imara za utawala zenye nguvu ambazo ziliwapa faida zaidi kiutawala na kiuchumi mpaka miaka ya baadaye ukilinganisha na jamii nyingine nyingi ambazo aidha hazijawahi kuw ana mifumo ya utawala au zilikuwa na mifumo dhaifu.

– Tumeona pia licha ya kwamba wachagga ni jamii iliyowekeza kwenye shughuli za kilimo na ufugaji lakini ujasiri uliwawezesha kuvamia maeneo mengine mengi ya mbali. Katika kipindi cha utawawala wa Mangi Rindi Mandara kuanzia katikati ya karne ya 19 wachagga waliweza kuvamia maeneo mengi ya nje ya Kilimanjaro na kuyadhibiti kuanza Upare mpaka Usambara na maeneo mengi ya Tanga. Uvamizi huu ulienda mpaka maeneo ya Serengeti na Loita upande wa Kenya hivyo eneo la Uchagga kuwa na umashuhuri mkubwa, utulivu na utajiri.

Chaga people who lived on slopes of Mt. Kilimanjaro. Chaga tribe at the installation of the “Mangi Mkun (Chief) , Chaga tribe , Public Relations Office Tanganyika Territory , International Library of African Music , Tanzania , ILM00420_37 , Portrait , Black and white print

– Hata hivyo ujasiri huu kwa wachagga ulikuja kupungua sana mpaka sasa kwa sababu ya kutohimizwa na kusisitizwa na badala yake hofu nyingi kupandikizwa lakini bado una umuhimu mkubwa hata sasa. Ujasiri wa sasa hivi haupo kwenye vita na mapambano lakini msingi wake ni ule ule wa kuzishinda hofu na kuvaa ujasiri katika mambo mengi ambayo yanahitaji maamuzi magumu na kazi kubwa ili kuyafanikisha. Moja kati ya sifa muhimu kabisa za mtu kufanikiwa ni ujasiri wa kuzishinda hofu mbalimbali.

– Hatua yoyote ya kutaka tu kuanza jambo lolote inahitajika ujasiri, kuanzia ujasiri wa kuanza, ujasiri wa kutohofia watu wanasemaje au kukuchukuliaji, ujasiri wa kuwakabili watu ambao wako kwenye nafasi fulani ili uweze kupita, ujasiri wa kujieleza kwa watu waweze kukubaliana na wewe na ujasiri wa kuona kwamba licha ya kuwepo watu wote unaofikiri wana akili sana au wanakuangalia sana bado huogopi wala kujali kuendelea mbele na mipango yako.

– Ujasiri unapoambatana na maarifa sahihi na shauku ya kufika mbali basi una manufaa makubwa sana. Hivyo bado kuna umuhimu mkubwa kama zamani au hata zaidi ya kuweka kipaumbele kwa sifa muhimu kama ujasiri kwetu na kwa watoto wetu, isipokuwa kwamba ujasiri wa sasa unapaswa kuambatana kwa karibu sana na maarifa sahihi ya kule unakoelekea.

Karibu kwa maoni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *