NAMNA YA KUGUNDUA UTAPELI KATIKA UWEKEZAJI.

– Moja kati ya watu matapeli waliowahi kujipatia umaarufu mkubwa sana duniani aliitwa Victor Lustig. Huyu Bwana Lustig alikuwa ni tapeli mwerevu kiasi kwamba aliwahi kuuza mnara maarufu wa jijini Paris, Ufaransa unaojulikana kama “Eiffel Tower” mara mbili. Siku moja aliwahi kuulizwa kwa nini anafanikiwa kutapeli watu mara nyingi na kirahisi bila kugundulika, na jibu alilotoa alisema “kwa sababu wajinga wanazaliwa kila siku”.

– Kwa maana hiyo basi ili mtu kuepuka kutapeliwa unapaswa kutokuwa mjinga. Lakini hata hivyo hii dunia ina mambo mengi kiasi kwamba huwezi kuepuka kabisa kutokuwa mjinga kwenye kila kitu. Lazima kuna mambo mengine mengi ambayo hutaweza kuyajuwa hata uwe nani. Hata hivyo licha ya kwamba huwezi kujua kila kitu lakini kuna misingi na kanuni ambazo ukizijua utaepuka sehemu kubwa sana ya utapeli unaotokea kila siku na watu kulizwa, hususan wa utapeli wa kuahidiwa kupata kikubwa kutoka kwenye kile ulichotoa.

– Mara nyingi matapeli hucheza na hisia kuu mbili za binadamu ambazo ni hisia ya tamanaa na hisia ya hofu. Hisi ya tamaa ni ile ya kupata zaidi na hisia ya hofu ni hofu ya kupoteza. Matapeli hutumia tamaa na hofu kuhakikisha wanakunasa kwenye mitego yao na hupata watu wengi. Mara nyingi utakuta wanakwambia ukiweka kiasi fulani cha pesa basi utapata kiasi fulani kikubwa sana cha pesa ndani ya muda mfupi. Hapo ndipo unakuta wanacheza na tamaa yako ya kupata kikubwa, halafu utakuta wanakwambia fursa hii wanayokupa ina kikomo, ukichelewa utaipoteza na utakuwa umepoteza nafasi adimu ya mafanikio ya haraka na rahisi ambayo utaijutia maisha yako yote, na hapo ndipo wanapocheza na hisia zako za hofu ya kupoteza.

– Hivyo sehemu ya kwanza ya utapeli ni kuangalia namna hii ya wao kukushawishi kwa kukutamanisha mafanikio makubwa huku wakikutisha kwamba unaelekea kupoteza nafasi hiyo na hivyo kukusukuma ufanye maamuzi ya haraka kabla muda haujaisha. Hizi ni dalili za mwanzo za kushawishiwa unase katika utapeli, huwa inaweza kuwa ni mojawapo ya hisia hizi mbili au ni zote mbili kwa pamoja ambapo ndio huwa na nguvu kubwa sana.

– Sehemu nyingine muhimu ya kuangalia katika utapeli hasa ambao unaambiwa ni uwekezaji ni kuangalia ni thamani gani inayozalishwa hapo au kutengenezwa inayopelekea wewe kupata mafanikio hayo. Ikiwa hakuna thamani inayoonekana kuzalishwa kutokana na uwezekaji huo unaombiwa uingie basi unapaswa kushtuka kwamba huenda utakuwa unatapeliwa.

– Huwa iko hivi Meku, hakuna kipato chochote cha bure duniani, hakuna fedha inayopatikana bure duniani. Uchumi ni sayansi. Hivyo fedha ambayo inawakilisha thamani inayotunzwa ndani yake ni zao la thamani fulani iliyotengenezwa. Thamani inaweza kuibiwa pale inapokuwa haijawekewa ulinzi lakini thamani haiwezi kutokea tu hewani. Hivyo kipato chochote unachopata kinapaswa kuwa kimetokana na thamani fulani iliyotengenezwa, tofauti na hapo basi unatapeliwa, hiyo ni kanuni muhimu sana ya kuzingatia wakati wowote ule unapoletewa fursa inayoonekana kuwa nzuri sana kwako. Usihadaika na uzuri wa fursa kabla hujajiridhisha kama ni ya kweli au ni feki.

– Je thamani inatokana na nini? Thamani inatokana na kazi iliyofanyika ambayo imewekewa juhudi fulani kuifanya kwa viwango vilivyofanyika. Thamani hiyo huongezeka kwenye bidhaa au huduma inayoweza kuuzwa na kununulika kama itahitajika hivyo. Kwa mfano mtu ukifagia uwanja ni thamani fulani umeongeza katika mazingira na thamani hiyo unaweza kulipwa kwa kiasi fulani cha fedha.

– Je sasa fedha inatokana na nini? Fedha ni karatasi au sarafu inayotengenezwa kwa ajili ya kuwakilisha thamani iliyotengenezwa. Kwa miaka ya sasa jukumu la kutengeneza fedha ni jukumu la serikali pekee. Yaani kwa mfano mtu umetengeneza panga kutoka kwenye chuma na mbao, lile panga linakuwa na thamani fulani ambayo itaamuliwa kutokana na sababu mbalimbali hususan zinazotokana na uadimu wa kufanikisha kitendo hicho kilichopelekea kutengenezwa kwa panga. Fedha ambazo hutengenezwa ili kuwakilisha thamani, thamani ya panga hilo linaamuliwa kwa vipande fulani vya fedha. Zamani kabla ya kuwepo kwa fedha biashara ilifanyika ya mali kwa mali(barter trade) ambayo iliweza kupima thamani ya kitu na kitu.

– Kwa sasa fedha imeondoa hiyo “barter trade” au biashara ya mali kwa mali kwa kurahisisha thamani kupimwa kwa fedha za makaratasi na sarafu zilizopewa thamani ambayo pia hutumika kupima thamani zilizotengenezwa kwa njia mbalimbali kupitia shughuli za kiuchumi.

– Sasa turudi kwenye mada yetu kwamba mtu anapokwambia kwamba ukiwekeza hapa utapata fedha nyingi sana baada ya muda fulani, muulize ni thamani gani inakwenda kutengenezwa hapo mpaka mimi nipate hiyo fedha? Kwa sababu kwa kawaida hakuna kipato kinachokuja bure tu. Akishindwa kukujibu kwamba ni thamani gani inayokwenda kutengenezwa hapo basi ujue huenda unatapeliwa.

– Hata hivyo tunafahamu kwamba ukiwekeza kwenye masoko ya mitaji au maarufu zaidi kama masoko ya hisa, ambapo kwa Tanzania soko maarufu la hisa ni Dar es Salaam au Dar es Salaam Stock Exchange(DSE) unaweza kupata kipato bila kufanya kazi yoyote. Hili ni kweli kabisa na sababu ziko wazi kwamba fedha zako zinaenda kuwekezwa kwenye mitaji ya kampuni au makampuni uliochagua mwenyewe kuwekeza kisha kampuni hiyo ikipata faida nawe unapata gawio lako kulingana na kiasi ulichowekeza. Hivyo uwekezaji kwenye masoko haya ya hisa uko wazi na shughuli zote za kampuni unayowekeza zinaeleweka na hata wewe mwenyewe ukitaka unaweza kupewa taarifa ya ripoti ya mwenendo wa kampuni husika kwa kipindi unachohitaji kufahamu, kwa sababu ukishawekeza unakuwa umenunua sehemu ya umiliki wa kampuni hiyo, hivyo nawe ni mmiliki.

– Hata hivyo uwekezaji huu wa kwenye masoko ya hisa kama vile DSE hauna mafanikio ya haraka wala makubwa sana kwa kiwango kidogo cha fedha. Kuwekeza kwenye masoko haya ili kuona manufaa yake unapaswa kuwekeza kwa muda mrefu, yaani kwa miaka huku ukiwa mvumilivu sana kusubiri uweze kufikisha uwekezaji mkubwa utakaoweza kukupa faida yenye tija. Kwa mfani kama bado umri wako ni mdogo, labda uko kwenye miaka ya 20 – 29 au 30 – 39 ukawekeza kwa bidii, utakapofika angalau kuanzia miaka ya 50 – 59 au 60 – 69 utakuwa umeanza kufikia kupokea gawio kubwa lenye tija, hususan kama ulikuwa unawezekeza kwa bidii katika riba mkusanyiko “(compound interest)”.

– Hata hivyo kwenye makampuni hayo bado hauko salama kwa 100% kwani ikitokea kampuni imefilisika nawe pia unakuwa umepoteza uwekezaji wako wote. Kampuni ikiendeshwa vibaya au kuyumba kutokana na sera mbovu za serikali na ikafilisika au kufungwa basi nawe unakuwa umeopoteza uwekezaji wako. Hiyo ni hatari ambayo mtu unakuwa unaibeba pale unapoamua kufanya uwekezaji kwenye makampuni.

– Lakini tofauti na uwekezaji kwenye masoko ya hisa au mwingine unaofanana na huo basi mtu utakuwa umejiingiza mwenyewe katika kutapeliwa ikiwa hutazingatia suala la thamani inayotengenezwa.

Kwa nini nimeamua kuandika hii makala?

– Nimeandika makala hii kutokana na usumbufu mkubwa ninaouona huko kwenye makundi ya kijamii hususan telegram ambapo kuna watu wengi sana hasa kutoka nchi za nje wanajaribu kushawishi watu kuwekeza kwenye maeneo tofauti tofauti na hasa kwenye fedha za mitandaoni (digital currencies maarufu kama cryptocurrency). Biashara za kuwekeza sehemu ambazo huelewi ni thamani gani inatengenezwa, ikiwa una bahati sana unaweza kufaidika mwanzo na kwa haraka lakini kwa gharama ya kuumia kwa watu wengine kwani kufaidika kwako kunakuwa kumetokana na watu wengine kuliwa (pata potea) au kwa kiingereza inaitwa zero sum game.

– Lakini uwezekano mkubwa ni kwamba utakuwa unapoteza kwani unaweka fedha zisizozalishwa hivyo zinaweza kuibiwa au kutaifishwa kwani watu wanaoziwinda huko ni wengi na hakuna kinachofanyika kuzizalisha ziwe nyingi kama inavyofanyika kwenye biashara halisi katika kuongeza thamani. Ni vyema kuwa makini sana ukatunza fedha zako vizuri na aidha kuziwekeza sehemu sahihi au kuzifanyia jambo lingine lenye manufaa kwako.

– Kumbuka kwamba wengi huliwa na kukaa kimya kwa kuogopa ile aibu ya kuonekana wameliwa au wamepoteza, majuto siku zote ni mjukuu na yanaweza kupelekea hata kudhuru afya yako ya mwili na akili.

– Kanuni ya kupata fedha ni kupitia kutengeneza thamani, kanuni hiyo ni rahisi sana, ifuate. Tofauti na hapo yanaweza kukukuta majanga. Ni aibu kwako mchagga kutepeliwa kiurahisi.

Ahsanteni.

Karibu kwa maswali, maoni au shuhuda.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *