Binti alipoolewa halafu yule Bwana harusi akakuta kwamba binti yule alikuwa ni bikra, ilikuwa ni desturi kwamba atachinja kondoo na kuwatumia nyama wazazi wa binti huyo, ambao nao pia watatuma tena kondoo kwa binti yao kwa kumshukuru binti yao kwa viwango vya juu vya maadili alivyozingatia.
Lakini ikiwa binti ameolewa na kukutwa kwamba hakuwa bikra, alirudishwa kwa baba yake mpaka atakapomtaja huyo mwanaume aliyelala naye na kupelekea kupoteza bikra yake. Kisha mwanaume huyo aliyelala na binti na kumsababishia kupoteza bikra yake akishajulikana hutakiwa kulipa fidia ya mbuzi wawili kwa baba wa binti ambaye naye aliwapeleka kwa mume wa binti yake.
Hata hivyo inasemakana kwamba baadaye wakati wa utawala wa Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu adhabu hii iliongezwa ikawa ni ng’ombe mmoja dume na mbuzi mmoja na ambapo adhabu hii ikakubalika uchaggani kote. Lakini hata hivyo inasemekana kwamba kwa maeneo mengi ya Rombo adhabu hii ilikuwa kubwa zaidi ambapo mwanaume aliyefanya kitendo hicho alipaswa kulipa kuanzia ng’ombe wawili mpaka watatu kama fidia.
Ikitokea mtu amempa mimba mwanamke ambaye tayari amechumbiwa na anasubiri kuolewa au kumwambukiza ugonjwa kupitia kufanya naye mapenzi, mwanaume huyo alitakiwa kulipa kiasi chote cha mahari ambacho kimelipwa na mchumba wa huyo binti kisha alipaswa kumuoa.
Ikitokea mtu amempa mimba mwanamke ambaye ni mke wa mtu mwingine alitakuwa kulipa faini ya ng’ombe wawili na mbuzi wawili na malipo mengine ya fidia ya mwanamke huyo wakati uzazi ambapo hataweza kuwa anafanya kazi. Lakini mara nyingi kwa kesi hii mume alimpeleka mke wake kwa mwanaume huyo aliempa mimba akaishi kwake mpaka alipojifungua na kulea huyo mtoto aliyezaliwa mpaka kufikia kuweza kujitegemea bila mama, ili huyo Bwana amgharamie mwenyewe.
Ikiwa mwanamke huyo atafariki wakati wa kujifungua basi atazikwa nyumbani kwa huyo mwanaume anayeishi kwake na sio kwa mume wake, lakini pia mwanaume huyo atatakiwa kulipa fidia ya ng’ombe watatu na mbuzi wanne. Katika mifugo hii ng’ombe mmoja na mbuzi mmoja alilipwa kabla ya mazishi na alilipwa kwa baba wa binti huyo, kama ilivyokuwa desturi pale ambapo mke anapofariki wakati wa kujifungua; huyo ng’ombe wa pili na mbuzi wa pili alilipwa kama adhabu ya kufanya uzinzi; ng’ombe watatu na mbuzi watatu alilipwa kama sehemu ya matunzo ya watoto aliyowaacha au kwa fidia ya “huzuni” aliyosababisha ikiwa hakuacha mtoto. Mbuzi alilipwa kwa ajili ya mila za mazishi.Ikiwa mtu atatoa taarifa za siri juu ya mahusiano ya kimapenzi kati ya watu ambao sio mume na mke atapaswa naye kulipa sehemu ya fidia zitakazotakiwa kulipwa. Hii ilifanywa hii kwa sababu iliaminika kwamba sio kazi yake kufuatilia maisha ya mke wa mtu bali hiyo ni kazi ya mume. Kwa sababu iliaminika kwamba ikiwa mtu anafuatilia maisha ya mke wa mtu mwingine maana yake ni kwamba anafanya kazi ya mume wa huyo mwanamke, yaani amejipa jukumu kama la mume wa huyo mwanamke hivyo amekuwa sasa yeye ndiye mume wa huyo mwanamke kitu ambacho tayari ni kosa la uzinzi pia.
Kosa kubwa zaidi lililotokana na mtu kufanya mapenzi kinyume na utaratibu katika nchi ya wachagga lilikuwa ni baina ya binti na kijana ambaye bado hajaenda jando(hajatahiriwa). Ikitokea kitendo hicho kimepelekea binti kupata mimba walilazwa chini mmoja juu ya mwingine kama wanafanya mapenzi kisha kuchomekwa mti wa mambo mgongoni kutokea tumboni na kupitiliza mpaka ardhini chini kabisa kisha kuachwa katika eneo. Kitendo hiki kilifanyika mwanzoni au mwishoni mwa shamba lililokuwa na mazao na miili yao iliachwa eneo husika bila hata kuzikwa. Hata hivyo inasemakana katika himaya ya (Chimbii)Shimbi, Rombo adhabu hii haikuwa inatekelezwa hivyo ikitokea kosa hili limefanyika wahusika wakipata nafasi waliweza kukimbilia Shimbi, Rombo na kuwa salama mpaka walipojifungua na baadaye kufanya taratibu za kurudi nyumbani.
Lakini ikitokea kwamba kijana ambaye tayari amekwenda jando(ametahiriwa) akafanya mapenzi na binti ambaye bado hajachumbiwa hili halikuhesabiwa kama ni kosa zaidi ilionekana kwamba ni tabia mbaya tu ya kawaida. Lakini kwa kesi hii baba wa binti alidai fidia ya mbuzi au ndama kwa binti yake kusababishwa kupoteza bikra yake kwa sababu binti huyo atakapoolewa huyo mume atakayemuoa atatumia kigezo cha binti kutokuwa na bikra kama sababu ya kutolipa mahari kamili. Lakini hata hivyo mara nyingi kwa kosa hili wahusika waliishia kuoana.
Ahsanteni.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com