SEHEMU YA 2.
8. NDEMASI.
(i) Ndemasi wa Mwika alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mwika tangu mwaka 1900 mpaka mwaka 1933 alipomwachia kiti cha utawala mtoto wake aliyeitwa Herabdieli Solomon. Mangi Ndemasi Solomon wa Mwika ambaye ni mtoto wa Mangi Tengio na mjukuu wa Mangi Kyasimba ndiye Mangi aliyewahi kukimbilia uhamishoni Nairobi sambamba na Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu na wafuasi wao kabla hajarudi baadaye na kuendelea kuwa Mangi wa Mwika tena tangu mwaka 1905 mpaka mwaka 1933.
(ii) Ndemasi wa Usseri alikuwa Mangi wa himaya ya umangi Usseri, Rombo tangu mwaka 1918 mpaka mwaka 1952. Mangi Ndemasi Matolo ni mtoto wa Mangi Matolo aliyeingia kwenye kiti cha utawala wa himaya ya Usseri baada ya kaka yake mkubwa aliyeitwa Mangi Salakana kufariki mwaka 1918. Baada ya utawala wa Mangi Ndemasi kiti cha utawala wa himaya ya umangi Usseri, Rombo kilienda kwa mtoto wake aliyeitwa Baltazari kwa muda mfupi na kisha kutawalishwa kwa mtoto wa Mangi Salakana aliyeitwa Alfred Salakana.
9. KEENJA
(i) Keenja wa Mbokomu alikuwa ni mtoto wa Mangi Marawite na ndugu yake Mangi Masha wa Mbokomu aliyetawala himaya ya umangi Mbokomu mwishoni mwa miaka ya 1700.
(ii) Keenja wa Mamba alikuwa ni Mangi wa Mamba himaya ya umangi Mamba mwishoni mwa miaka ya 1700 au mwanzoni mwa miaka ya 1800. Mangi Keenja wa Mamba alikuwa ni mtoto wa Mangi Ngawondo na aliitawala himaya ya umangi Mamba katika nyakati za Mangi Mashuhuri Horombo wa Keni ambaye Mangi Keenja akishirikiana na Mangi Ishosho wa Marangu walipigana naye vita na kushindwa ambapo Mangi Ishosho aliuawa huku Mangi Keenja akikimbilia uhamishoni Kirua Vunjo.
10. MARENGA/MARENGO.
(i) Marenga wa Kirua Vunjo alikuwa ni Mangi wa Kirua Vunjo katika miaka ya 1830’s/1840’s katika nyakati za Mangi Mamkinga wa Machame. Mangi Marenga wa Kirua Vunjo ambaye alikuwa ni mtoto wa Mangi Kikare na mjukuu wa Mangi Mosha alipinduliwa kwenye kiti cha umangi wa Kirua Vunjo na mtoto wake aliyeitwa Kirumi ambapo alijaribu kutafuta msaada wa Mangi Mamkinga wa Machame bila mafanikio.
(ii) Marengo wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu katika miaka ya 1860’s ambapo aliingia madarakani kwa kumpindua ndugu yake aliyeitwa Kinabo. Mangi Kinabo akishirikiana na Msanya aliyekuwa mke wa Mangi Itosi ambaye pia ni mama yake Mangi Ndaalio wa Marangu walikimbilia Old Moshi kwa Mangi Rindi Mandara kupata msaada wa kijeshi na kuja kumpindua Mangi Marengo na kumrudisha Kinabo. Marengo naye akakimbilia Kibosho kwenda kupata msaada wa kijeshi kutoka kwa Mangi Ngaluma wa Kibosho ambaye alikuja na kumpindua Kinabo na kumrudisha tena Marengo. Ndipo Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi na majeshi yake wakaja tena kwa mara ya tatu kuivamia Marangu, Mangi Marengo akauawa na askari wa Old Moshi na kisha kumtawalisha tena Kinabo katika miaka ya 1870’s.
11. SALEMA.
(i) Salema wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa Old Moshi kuanzia mwaka 1900 baada ya Mangi Meli kunyongwa. Salema alikuwa ni mtoto wa tatu wa kiume wa Mangi Rindi Mandara aliyeidumu kwenye kiti cha utawala Old Moshi kwa takriban miaka 20 ambaye pia ndiye baba yake Mangi Abrahamu Salema Mandara wa Old Moshi aliyekuwa pia Mangi Ang’anyi wa jimbo la Hai, Uchagga.
(ii) Salema wa Mengwe, Rombo alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mengwe iliyopo katikati ya himaya za umangi Mriti na Keni. Mangi Salema wa Mengwe pia ndiye baba yake Salia ambaye aligombea kiti cha umangi wa himaya ya umangi Keni-Mriti-Mengwe yeye na Wingia Ngache baada ya Mangi Herman Tengia kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
12. NYANGE.
(i) Nyange wa Kilema alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Kilema baada ya utawala wa baba yake aliyeitwa Mremi. Mangi Nyange wa Kilema alipinduliwa na kaka yake aliyeitwa Musuo baada ya baba yao Mangi Mremi kufariki na hivyo kwa msaada wa Mangi Mapfuluke wa Mamba Nyange alifanikiwa kurudi kwenye kiti cha umangi wa Kilema. Mangi Nyange wa Kilema ndiye baba yake Mangi Kombo wa Kilema na ndiye baba yake Mangi Mashuhuri Rongoma wa Kilema.
(ii) Nyange wa Mamba alikuwa ni Mangi wa mwanzoni sana wa himaya ya umangi Mangi akiwa ni mtoto wa Mangi Munyi wa Mamba. Hivyo kizazi chote cha utawala wa himaya ya umangi Mamba kimetokana na Mangi Nyange wa Mamba.
13. MKINDE.
(i) Mkinde wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa Old Moshi tangu mwaka 1917 wakati Mangi Salema wa Old Moshi na wamangi wengine wa Kilimanjaro walipopelekwa kifungoni huko Kismayu, Somalia kwa tuhuma za kutaka kuipindua serikali ya Uingereza. Mkinde alitawala kama Mangi wa Old Moshi kwa wakati huu akiwa ni mtoto wa Mangi Kitori wa Old Moshi ambaye alikuwa ni ndugu yake Mangi Rindi Mandara aliyekuwa amewekwa madarakani Old Moshi kama kibaraka wa Kibosho na majeshi ya Mangi Lokila wa Kibosho yaliyokuwa yamempindua katika miaka ya 1870’s, kabla ya baadaye Mangi Rindi Mandara kurudi tena madarakani Old Moshi kwa msaada wa jeshi la wamasai.
(ii) Mkinde wa Marangu alikuwa ni baba yake na Nathanieli kutoka kwenye ukoo wa Mtui katika kijiji cha Mshiri Marangu. Nathanieli alikuwa ni mwanahistoria mahiri na mashuhuri sana katika historia ya wachagga Kilimanjaro na ni moja kati ya wachagga waliokuwa na uwezo mkubwa sana kiakili miaka ya zamani. Nathanieli Mti ndiye mchagga aliyesaidia uandishi mkubwa sana wa historia za wachagga zilizoweza kuhifadhiwa.
14. LYAMARI.
(i) Lyamari wa Machame alikuwa ni ndugu yake Mangi Ndesserua Mushi wa Machame ambaye alitawala himaya ya umangi Machame tangu miaka ya 1850’s mpaka miaka ya 1870’s. Lyamari alikuwa ni kama Mangi wa Machame ya magharibi maarufu kama Masama kwa sababu licha ya kwamba alikuwa ni mtoto wa Mangi Mamkinga na ndugu wa Mangi Ndesserua lakini aliongoza majeshi ya Machame ya Magharibi au maarufu kama Masama kupambana na majeshi ya Mangi Ndesserua katika kupingana na utawala wa kikatili zaidi wa Mangi Ndesserua.
Lyamari aliunganisha watawala wote na koo zote za Machame ya magharibi au maarufu kama Masama ambao walijiona wakiwa wahanga zaidi wa utawala wa Mangi Ndesserua, hivyo kumkubali sana Lyamari na kuona kwamba ndiye mkombozi wao dhidi ya utawala wa kidhalimu sana wa Mangi Ndesserua na hivyo kupelekea vita vikubwa na vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Machame ya Mashariki chini ya utawala wa Mangi Ndesserua na Machame ya Magharibi iliyoitwa pia “Mashami Sinde” au maarufu zaidi kwa sasa kama Masama iliyoongozwa na Lyamari na kupelekea kuidhoofisha sana Machame kwa ujumla.
Hata hivyo licha ya Machame ya Magharibi(Mashami Sinde) maarufu zaidi kama Masama kushindwa kuangusha utawala wa Mangi Ndesserua, lakini baadaye mwaka 1951 walipojitoa Machame na kuanza kujiita rasmi Masama walimtangaza Lyamari kuwa ndiye Mangi wao wa kwanza katika historia wanayemtambua kutokana na uhasama mkubwa waliokuwa nao dhidi ya ndugu zao wa Machame ya Mashariki.
(ii) Lyamari wa Old Moshi alikuwa ni moja kati ya watawala wa ukoo wa Kimambo katika kijiji cha Mowo, Old Moshi akiwa ni mtoto wa injinia maarufu wa mifereji(mifongo) na mtoto wa mtawala wa ukoo wa Kimambo kijiji cha Mowo, Old Moshi aliyeishi katika miaka ya mwishoni ya 1700.
ITAENDELEA KESHO.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com