– Ukoo wa Nkini ni moja kati ya koo kongwe kabisa na mashuhuri sana katika eneo la Siha/Sanya Juu. Ukoo wa Nkini sambamba na koo nyingine katika eneo hilo walishuka kutoka kwenye plango ya Shira(Shira Plateau) na kuweka makazi yao katika vijiji vya ukanda wa juu wa himaya ya umangi Siha/Sanya Juu hususan kijiji cha Samaki Maini ambacho ndio kikongwe sana.
– Ukoo wa Nkini walikuwa ni wachagga maalum wa eneo hili waliokuwa na kazi ya kufanya ibada takatifu ya kuombea mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaendelea katika nchi. Jambo hili lilifanya wachagga wa ukoo wa Nkini kuheshimiwa sana na wachagga wengine wote kwani mambo yote ya mila na tambiko takatifu kabla ya kuingia kwa ukristo yalifanywa na wao. Hivyo jambo lolote lilipotokea ambalo lilihitaji kufanyika kwa ibada takatifu wachagga wengine wote waliwategemea ukoo wa Nkini kufanya mchakato huo.
– Kutoka kwenye historia tunajifunza kwamba pia ukoo wa Nkini ndio wachagga wa kwanza kushuka kutokea kwenye plango ya Shira(Shira Plateau) na kuweka makazi yao katika ukanda wa chini zaidi katika kijiji cha Samaki Maini. Eneo walilotokea wachagga wa ukoo wa Nkini katika plango ya Shira ambalo linafahamika kwa jina la “Wawa” pia ndilo lililokuwa eneo la kuabudia la wachagga wa eneo la Sanya Juu, hiyo ikawa ni ishara nyingine ya jukumu walilokuwa nalo wachagga wa ukoo wa Nkini.
– Tunaona kwamba wachagga wa ukoo wa Nkini baada ya kuhama kwenye plango ya Shira walihamia katika eneo lililojulikana kama “Kihubihu” ambalo ndilo pia liliendelea kuwa eneo takatifu zaidi la kuabudia la wachagga wa eneo la Siha/Sanya Juu kwa ujumla. Hiyo ilipelekea wamisionari wa kilutheri walipofika Siha pia waliamua kuanzisha kituo chao cha kwanza cha misheni ya kilutheri katika eneo hilo la Kihubihu na kuanzisha misheni ya kwanza ya Siha Sango.
– Lakini pia kutokana na jukumu zito walilokuwa nalo wachagga wa ukoo wa Nkini kwenye mambo ya kiroho na ibada takatifu za wachagga, wamisionari wa kilutheri waliona ni muhimu kwao kuwapa kipaumbele ukoo wa Nkini kwenye mambo ya misheni kwani walikuwa wamebeba imani kubwa ya wachagga wengine kwenye mambo ya kiroho. Mfano mmojawapo ni Mchungaji Jeremiah Nkini ambaye alikuwa ni moja kati ya wachungaji wa mwanzoni sana katika eneo hili akiwa ni mtoto wa Mzee Nsairo Nkini aliyekuwa Mzee mashuhuri wa ukoo wa Nkini.
– Wachagga wa ukoo wa Nkini pia walikuwa ni matajiri wakubwa wa mifugo na wakulima hodari wa mazao mbalimbali hususan ulezi. Wachagga wa ukoo wa Nkini wanaonekana kupatikana zaidi katika eneo la Siha/Sanya Juu peke yake hivyo pengine hawako kwa idadi kubwa sana. Chimbuko lao zaidi ni katika kijiji cha Samaki Maini japo wanapatikana katika vijiji vingine pia.
Tunaomba mchango wako wa mawazo zaidi juu ya ukoo huu wa kipekee sana wa Nkini.
1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Nkini?
2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Nkini?
3. Kama wewe ni wa ukoo wa Nkini una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?
4. Bado mna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?
5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Nkini?
6. Wanawake wa ukoo wa Nkini huitwaje?