UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 3.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

KUMCHAGULIA MTOTO JINA.

-Mtoto akifikisha umri huu baba na mama humchagulia jina. Basi mtoto mzaliwa wa kwanza ikiwa babu yake ni marehemu huitwa jina la babu wa upande wa baba, na ikiwa babu yake yu hai ataitwa jina la babu wa babu wake. Binti hupewa jina la bibi mkubwa.

Wazaliwao baadaye hupewa majina ya wajomba zao, au majina yanayoendana na vitendo vilivyowatokea wazazi au watu wan chi nzima vya furaha au vya kuhuzunisha.

Mfano mara kwa mara husikia Mchagga akiitwa “Ndemasa”. Maana yake “Nilichuma mali, Mungu ni mwema”, vile vile kwa jina hili likiwa limeongezwa mwishoni “Ndemasandalye” maana yake ni nyingine yaani “Nilichuma mali lakini sikuitumia”, labda kwa kuwa iliharibika, ilipotea au alinyang’anywa na kadhalika.

Mwingine humwita mtoto “Ngao”, Maana yake amekumbuka jinsi siku moja au wakati mmoja alipokuwa akipigana vita ngao yake ikamsaidia sana, ama kwa msaada wa kitu chochote kilichomlinda na kumfaa siku za shida. Mwingine humwita mtoto “Kirama” maana yake “Umoja ni nguvu”. Mwingine humwita mtoto “Maangie” maana yake “Aliyeshangiliwa”. Mwingine humwita mtoto “Kikari” maana yake “Shujaa” au “Jasiri” na kadhalika.

-Hakika majina ya Wachagga mengi yana sababu zake. Hufuata ukoo na mambo za hali za watu. Mengine ni kwa ajili ya ushujaa, hata mengine ni kama siri ya historia, kwa mfano “Msagoni” maana yake amezaliwa wakati usio na ng’ombe. Wanawake hupewa majina ya bibi na mengine ya vitendo kama vile “Mkunde”(Aliyependeka). Mkamsuri(Mwanamke Tajiri). Au huitwa majina ya ukoo au ya mahali katika nchi, na majina hasa yanayotokana na vitendo vya taabu na furaha.

-Mtoto akifika umri huu hubadilisha chakula na kuanza kula vyakula vya watu wazima na kula muda ambao watu wazima wanakula, wazazi hawajali tena kwamba mtoto anahitaji kuendelea kujaliwa vyakula vya afya ili azidi kuimarika anapoendelea kukua.

Kati ya makosa ambayo wazazi wa Kichagga hufanya ni kutokuweka nguvu tena kwenye kujali malezi ya mtoto hasa kiafya kutokana na kujishughulisha sana na kazi na hivyo mara mwingine hupelekea mtoto hudhoofika kiafya. Mtoto huendelea kufundishwa kazi ndogo ndogo za nyumbani na shughuli za kilimo, biashara na ufugaji. Waendapo shamba huchukua ndizi mbivu za kula au chakula. Chakula cha kulia shamba kwa Kichagga huitwa “kichau”.

-Basi tukiangalia katika umri huu binti huwa amezidishiwa kazi zake kuliko mtoto wa kiume wa rika lake. Watoto wa kiume hufundishwa ufugaji pamoja na shughuli nyingi za kijasiri. Watoto wote wa kike na wa kiume hufanya michezo mbalimbali ya kutumia nguvu kama vile kupigana na mieleka, kuruka juu ya miti na kutengeneza mashimo na mahandaki wanakojificha na kukimbizana. Watoto wa kiume walipigana vita vya michezo viitwavyo “kimandolu”, wakijiweka tayari na silaha zao hizi, na katika mapigano haya mtu aweza kuumia lakini ni hali ya mchezo tu.

Nao watoto wa kike huenda sokoni, kulima na kuchuma majani ya ng’ombe. Katika michezo yao ya wakati huu ambayo ni ya juhudi sana, iwapo yuko mvulana au msichana aliaye hovyo kwa sababu ya maumivu ya michezo, wenzake humwimbia wimbo wa kumcheka ili aache kulia. Wimbo wenye ndio huu;

“Manene korio kelya kya mbuonyi, Mikasia ukoriosepfo kingi”.

Maana yake; Mlialia hovyo alishwe chakula cha puani badala ya mdomoni na kikiisha azidishiwe kingine huko huko puani.

-Watoto wadogo hukaa nyumbani lakini wakifikia umri mkubwa wa kubalehe huchukuliwa kwenda kukaa na bibi na babu ili wafundishwe na kulelewa nao. Wakiwa kwa bibi na babu yao hujifunza mengi na kufanya kazi nyingi za mikono. Chakula kikiwa jikoni bibi huwasimulia hadithi nyingi za Kichagga kwa mfano hadithi ya Mregho ambayo nitaielezea baadaye.

-Watoto wa kiume hucheza mchezo wa “Oro” ambao mwandishi ameuelezea vizuri huku kwenye kitabu, ni mchezo mzuri wa ushindani na unaoweza kuburudisha sana watazamaji. Mchezo huu ulifaa sana kwa kuwafundisha watu kuweza kulenga wanyama wanaokimbia na adui vitani mikuki. Uliwafundisha pia umoja na utaratibu wa kufanya vita, kwani taratibu na sheria za mchezo huu ni ngumu na zilifuatwa kwa uangalifu sana. Huu ni mchezo ambao tungeweza kuundeleza na kuwa hodari sana katika huu mchezo na ukatupatia umaarufu mkubwa na manufaa ya kiuchumi.

-Kwa wastani wasichana walikaa kwa bibi zao kwa muda usiopungua miaka minane, watoto wa kiume hukaa muda mfupi zaidi kwa sababu wao huwa na mashughuli mengi yanayohusika na utawala wa Mangi wao na kusaidia nchi siku za shida.

ITAENDELEA.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *