#THE JEWISH PHENOMENON# “SEHEMU YA 8” #Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

#THE JEWISH PHENOMENON#

SEHEMU YA 8

#Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

JENGA UWEZO WA KUJIAMINI KATIKA KUJIELEZA.

Kujiamini na kujieleza ni kati ya changamoto kubwa sana tulizonazo katika nchi hii, japo hili linachangiwa pia na kutofahamu mambo mengi lakini aina ya malezi tuliyokuwa nayo kwenye familia mpaka kwenye nchi yamechangia kwa kiasi kikubwa, na ubaya ni kwamba jambo hili linaturudisha nyuma na kutukosesha fursa nyingi sana. -Kujenga uwezo wa kujiamini, kuwa na ujasiri wa kuhoji vitu mbalimbali yakiwemo maamuzi ya mamlaka za juu, kuhoji na kutoa changamoto kwa taratibu ambazo zimepitwa na wakati ni moja ya sifa muhimu za wayahudi zilizochangia kuwasaidia kupiga hatua kubwa.

#UWEZO WA KUJIELEZA NI SEHEMU YA DINI YA UYAHUDI.#

Wayahudi wamekuwa wakifundishwa tangu utotoni kuanzia kwenye vitabu vya dini mpaka kwenye maisha kuhoji uhalali wa kila kitu zikiwemo mamlaka au mafundisho mbalimbali.

Tofauti na wakristo wayahudi wanasoma biblia na kuhoji uhalali wa hadithi zote zilizomo kwenye biblia bila hofu yoyote.

-Wanasoma hadithi kama ile ya Musa kuichapa bahari ya shamu na njia kutokea kisha wana wa waisrael kupita juu yake, na kisha kuhoji uhalali wa hadithi hiyo.

Wanahoji hadithi ya mapigo kumi ambayo Farao wa Misri alipigwa na Mungu alipokuwa anakaidi amri ya kuwaachia wana wa Israel kutoka utumwani Misri.

-Wanahoji uhalali wa hadithi kama ya Nuhu kutengeneza Safina, Yona kumezwa na samaki na kukaa tumboni mwa samaki siku tatu kisha kutapikwa na kuendelea na shughuli nyingine pamoja na hadithi nyingine mbalimbali katika vitabu vya dini.

-Watoto na vijana wa kiyahudi wamekuwa wakihoji asili ya uumbaji kwa kulinganisha maelezo ya vitabu vya dini na nadharia za kisayansi kama zile za kina Charles Darwin katika kutafuta kujua ipi inaweza kuwa na uhalisia zaidi.

-Wazazi wa kiyahudi wamekuwa wakiwahimiza watoto wao kufikiri kwa kina na kufahamu kila kitu, wamekuwa wakiwahimiza kuuliza maswali mengi kadiri wanavyotaka na kujitahidi kuwatafutia majibu ambayo yanaweza kuwajengea shauku zaidi ya kujifunza zaidi.

-Katika maazimisho ya sherehe mbalimbali za kiyahudi watoto wamekuwa wakipewa nafasi ya kuuliza maswali na hasa katika kujua maana ya sherehe za maazimisho hayo na umuhimu wake katika maisha yao kama jamii ya wayahudi.

-Katika jamii ya wayahudi mtoto akifikisha umri wa miaka 13 anaanza kuhesabika kama mtu mzima na mwenye uwezo wa kufanya maamuzi juu ya msimamo wake katika dini na kuwajibika kwao.

-Uwezo wa kujiamini katika kujieleza umeweza kuwasaidia wayahudi kupata mafanikio sana katika tasnia mbalimbali kama vile katika filamu, vichekesho(comedy) n.k.,.

-Katika filamu wayahudi ndio waanzilishi wa Hollywood ambayo ndio tasnia ya filamu ya nchini Marekani na wameweza kuitumia sana katika kujenga ushawishi kwenye maeneo mengine kama vile mavazi na kukuza sana pia viwanda vya mavazi vinavyomilikiwa zaidi na wao wenyewe.

Wayahudi wengi sana wana mafanikio makubwa katika tasnia ya filamu nchini Marekani maarufu kama Hollywood, hata Steven Spielberg ambaye ndiye bilionea mwenye mafanikio zaidi katika tasnia ya filamu Marekani ni Myahudi.

-Uwezo wa kujiamini na kujieleza umewasaidia pia wayahudi kuwa na mafanikio sana na kuitawala sana pia tasnia ya habari kama waandishi, wahariri na watangazaji wanaofanya vizuri sana katika tasnia husika.

#MAMBO AMBAYO WACHAGGA TUNAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA KWA WAYAHUDI.#

1. Tuhimize Watoto Wetu Kuuliza Maswali.

Uwezo wa kuongea na kujiamini katika kujieleza huanza mapema sana kwa mtoto. Wahimize watoto kuuliza maswali na wahakikishie kwamba ni sahihi kabisa wao kuuliza maswali na waulize maswali mengi kadiri wanavyohitaji.

Mawasiliano kati ya mzazi na mtoto ndio kitu cha mwanzo kwa mtoto katika kuingiliana na jamii, na ni kitu muhimu sana. Kama watoto watajibiwa maswali yao kwa shauku na kupewa majibu mazuri yanayoeleweka wataendelea kuuliza zaidi na kujenga uwezo mzuri wa kuwasiliana na kujieleza. Lakini kama maswali ya mtoto yataonekana kama ni usumbufu, uwezo wake wa kuwasiliana utashuka na uwezo wa kujieleza utakuwa chini sana.

2. Tujitahidi Kuwa Tunawafundisha na Kuwaeleza Watoto Mawazo na Idea Mbalimbali.

Kwa watoto dunia ni mpya na vitu vingi ni vipya kwao, vitu ambavyo mtu mzima utachukulia kawaida kwa mtoto ni vitu vya tofauti na vinavyomvutia sana. Unapomweleza mtoto vitu vipya vinamuongezea kujiamini na kuitazama dunia kwa utofauti. Jaribu kumwelezea mtoto vitu kama jua, anga, nguvu ya uvutano ya dunia(gravity) na namna vinafanya kazi.

Mwelezee mambo yote unayojua kuhusu taaluma mbalimbali kama vile, umeme, afya, historia, siasa n.k.,. Mwambie namna fedha inatafutwa na changamoto za namna ya kuipata pamoja na sheria mbalimbali za fedha sambamba na gharama za maisha ukilinganisha na wastani wa kipato. Watoto wanapoanza kupata uelewa wa namna dunia inafanya kazi wanaanza kuona namna dunia inawahusu na kuanza kuhshiriki, na kadiri wanavyotamani kushiriki katika kuchangia kwenye dunia ndivyo kadiri wanavyoongeza uwezo wakujiamini na kujieleza.

3. Kula Chakula Cha Jioni Pamoja Kama Familia.

Kati ya majadiliano ya mawasiliano ya mwanzo kabisa kati ya mzazi na mtoto yanafanyika katika meza ya chakula cha jioni. Watoto kujieleza mbele ya familia nzima ni mwanzo mzuri wa wao kujijengea kujiamini mbele za watu. Kama mzazi jaribu kufahamu ratiba ya mchana ya mtoto, kumhoji na kumsikilizi ni nini anazungumza. Jaribu kumhoji na kumpa changamoto za kwa nini anafikiri mambo yako kama anavyofikiri ili kumjengea kufahamu kiundani kile anachofikira. Kwenye familia za kiyahudi mazungumzo katika meza ya chakula cha jioni ni muhimu na huwajenga sana watoto katika kujijengea kujiamini.

4. #Wahimize Watoto Kushiriki Katika Sanaa na Michezo.#

Hata kama mtoto hana vipaji vya michezo lakini bado kuna faida kubwa kwake kushiriki katika michezo mbalimbali. Kikubwa ni aweze kujenga kujiamini akiwa mbele za watu. Anaweza kuwa anatoa hotuba mbele za watu, kuimba, kupiga vyombo na kushiriki michezo mbalimbali. Ile presha ya kusimama mbele za watu itamjenga sana na kumjengea kujiamini zaidi.

Ahsanteni

TUTAENDELEA NA SIRI YA 5 Kwenye Makala Inayofuata.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *