#THE JEWISH PHENOMENON# “SEHEMU YA 9” #Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

#THE JEWISH PHENOMENON#

SEHEMU YA 9

#Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#

#JENGA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA, WEKEZA KUWA TAJIRI#

-Wayahudi ni jamii ambayo imekuwa ikishutumiwa sana kwamba ni watu wanaishi maisha ya ubahili na ndio maana wameweza kukusanya utajiri mkubwa, lakini wayahudi wenyewe wanapinga kwa kusema kwamba hawana ubahili bali wanaangalia zaidi vipaumbele kadiri ya hali ya kiuchumi waliyonayo.

Wayahudi wanasema hawana ubahili bali wana nidhamu ya matumizi kadiri ya kipato kinavyowaruhusu. Hata hivyo takwimu zinaonyesha kwamba wayahudi ndio watu wanaojitolea zaidi katika kusaidia na michango kwenye charity mbalimbali kuliko jamii nyingine.

-Kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha sio ubahili bali ni kuwa makini na maisha ya sasa na ya baadaye, wayahudi wanaamini katika matumizi sahihi ya fedha kupitia nidhamu ya matumizi ili kuijenga kesho iliyo bora zaidi kuliko leo.

-Licha ya kwamba wayahudi wana nidhamu kubwa sana ya fedha ukilinganisha na jamii nyingine Marekani, lakini ndio jamii inayoongoza kutumia fedha nyingi katika kununua vitabu.

Sio tu kwamba wayahudi wengi ni waandishi wa vitabu bora sana katika soko bali ni wanunuaji na wasomaji wakubwa sana wa vitabu kwani wanaamini maarifa ni kitu chenye thamani kubwa sana ambacho watu wengi hawawekei uzito unaostahili.

-Katika kupangilia vipaumbele kulingana na thamani husika wayahudi wanaamini kipaumbele namba moja ni elimu au maarifa, kipaumbele namba mbili ni fedha na kisha kipaumbele namba tatu ni mali.

-Wakati katika harusi nyingi za jamii mbalimbali watu huwapa maharusi zawadi tofauti za vitu, katika jamii ya wayahudi zawadi huwa ni fedha ambayo wanapewa kama sehemu ya kuanzia katika uwekezaji wowote watakaoenda kuuanza katika kufika ndoto zao za kifedha kifamilia.

#MAMBO AMBAYO WACHAGGA TUNAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA KWA WAYAHUDI#

Utangulizi

Watu wengi wanaamini kwamba utajiri ni kitu kinachomtokea mtu kwa bahati na kwa ghafla, wengi wetu hatujui kwamba utajiri ni kitu kinachoanzia kwenye msingi na kuongezeka kadiri muda unavyosogea mbele.

Watu wengi bado wako na imani kwamba kuna siku moja atapata pesa nyingi awe tajiri bila kujua kwamba kila pesa unayopata kila siku inatakiwa ichangie katika kukufikisha kwenye utajiri unaouota, kila pesa unayopata kila siku ukiipangilia kwa usahihi ni sehemu ya utajiri mkubwa utakaokusanya kadiri muda unayosogea mbele.

Mambo Ya Kujifunza Kwenye Fedha na Utajiri.

-Kamwe usitumie fedha yote unayoingiza bali weka akiba angalau kila asilimia 10% ya kipato unachopata kwa ajili ya uwekezaji wa baadaye.

Yaani nenda ukafungue fixed akaunti benki kisha weka angalau kila asilimia 10% ya pesa unayoipata, iwe kupitia mshahara, biashara au kazi yoyote, weka kwenye akaunti hiyo kabla hujaanza kutumia fedha hiyo.

Kwa mfano kama umepata Tshs 500,000 basi chukua angalau si chini ya Tshs 50,000 weka kwenye hiyo akaunti, kisha ndio unaanza kuipangia matumizi Tshs 450,000 iliyobaki, unaweza kuweka zaidi ya hiyo kadiri ya wewe mwenyewe unavyoweza kujibana na kipato kinavyoruhusu. Kama laki tano ilikuwa inakutosha basi hata laki nne na nusu inakutosha pia. Ukifanya hivyo kwa nidhamu ya hali ya juu bila kuacha baada ya miaka miwili mpaka mitano unaweza kujikuta una fedha ambayo unaweza kuiwekeza maeneo mbalimbali kwa mfano labda kununua kiwanja kwenye eneo ambalo unajua baada ya muda bei itakuwa imepanda na utauza kwa faida au kama umeshanunua viwanja kadhaa unaweza kutumia vingine kuchukua mkopo na kujenga nyumba za kupangisha au za biashara n.k.,. Au pia unaweza kuiwekeza hiyo fedha katika kununua hisa kwenye makampuni au hata kuitumia kama mtaji katika kuanzisha biashara unayoipenda au unayotamani kuanzisha muda mrefu lakini ukawa na changamoto ya mtaji. Wakati huo mambo yako mengine yakiendelea kama kawaida kwa sababu hiyo ni fedha uliyoweka akiba peke yake. Fedha unayoweka akiba ndio fedha inayokwenda kukuletea utajiri.

– Kuweka akiba ni tabia unayopaswa kuifanya maisha yako yote na hata kufundisha watoto, na iwe sehemu ya utamaduni.

-Punguza matumizi mengi yasiyo ya lazima, ni muhimu mtu kujiuliza kabla ya kutumia fedha yoyote endapo fedha unayotumia ina thamani ya hicho unachokwenda kutumia au kama ina umuhimu, fedha ni kitu kinachopatikana kwa kujitoa sana hivyo kinapaswa kitumike kwa vitu muhimu pekee na kuepuka visivyo muhimu. Kwa mfano kama mtu unaweza kula nyumbani huna haja ya kutumia fedha nyingi kununua vyakula kwenye migahawa, au kama bado kipato chako hakijawa kikubwa huna haja ya kumiliki gari ya bei mbaya sana mwanzoni, utakuja kununua gari ya bei mbaya kadiri kipato chako kitakavyoendelea kuruhusu huko mbeleni.

Kadiri unavyookoa pesa nyingi zaidi kwenye matumizi yasiyo ya lazima, unaongeza katika akiba zako, ambazo ndizo zitakuja kukuletea utajiri unaoutamani.

-Tujitahidi sana linapokuja swala la ndoa kuepuka misukosuko ya ndani ya ndoa au talaka kwa sababu mambo haya huchangia sana katika kuyumbisha uchumi wa familia kwa namna nyingi sana, ni muhimu sana kama umeamua kuingia kwenye ndoa basi jitahidi kuhakikisha inakuwa ndoa itakayodumu.

Hatari ya ndoa kuvunjika hupungua pale unapooana na mtu unayemfahamu vizuri tabia na mienendo yake au mtu ambaye mnatokea kwenye jamii moja na mmekuzwa na kulelewa wote katika mazingira ya jamii husika na mnafuata tamaduni za jamii ya kwenu, hii hupunguza hatari ya ndoa kuvunjika.

Kuvunjika kwa ndoa sio tu kuna madhara makubwa kisaikolojia na hasa kwa watoto bali kuna madhara makubwa kiuchumi pia. Licha ya kwamba ndani ya Marekani nusu au asilimia 50% ya ndoa zinazofungwa huvunjika, ni asilimia 12% tu ya ndoa za wayahudi ndani ya Marekani ndizo huvunjika, yaani ni wastani wa robo ya ndoa zinazovunjika, mafanikio haya ya kindoa kwa wayahudi yamesaidia zaidi katika kuimarisha uchumi wa familia hizi.

Pia katika dini ya wayahudi wamejiwekea sheria ngumu sana endapo mtu akitaka kuvunja ndoa.

-Jitahidi sana kuepuka mikopo isiyozalisha pamoja na kuepuka kuchukua mkopo kwa ajili ya kwenda kuanza biashara mpya ambayo hujawahi kuifanya kabisa, mikopo ina gharama kubwa na ni rahisi kukutana na anguko litakalokuumiza sana. Mkopo unaouchukua kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sio uzalishaji ni kujiongezea mzigo usiokuwa na ulazima kwani unaulipa kwa riba kwa sababu umeshindwa kuishi ndani ya kipato chako cha kawaida. Jitahidi sana uishi ndani ya kipato chako kwa matumizi ya kawaida kwa kupunguza zaidi matumizi yasiyo ya lazima sambamba na kuweka akiba kila kipato unachopata ili uje uingie kwenye biashara na uwekezaji. Kama tayari umeshaingia kwenye madeni basi jitahidi uyalipe na kuondokana nayo moja kwa moja.

Mkopo utakuja kuchukua wakati biashara imeshachangamka na ina faida kubwa na unaona kabisa kwamba ukichukua mkopo utaweza kulipa riba bila mashaka yoyote na faida bado utabaki nayo ya kutosha.

-Jitahidi sana kulinda afya yako. Afya yako ya mwili na akili inaathiri kipato chako moja kwa moja. Ni muhimu sana kuwa unamuona daktari ili kucheki afya mara kwa mara kujua hali yako ili kama kuna ugonjwa unakunyemelea au umeanza uweze kuudhibiti mapema, kwani ni gharama nafuu zaidi kudhibiti ugonjwa mapema kuliko kusubiri ukafika katika hatua ya hatari ambapo utakugharimu pesa nyingi sana kushughulika nao.

Fuata ushauri wa namna ya kula kwa afya badala ya kula hovyo bila utaratibu na fanya mazoezi kila siku. Faida za kula vizuri na kufanya mazoezi na hata kucheki afya mara kwa mara utaendelea kuziona zaidi kadiri umri unavyosogea mbele kufikia utu uzima zaidi. Ukifanya uzembe kwenye swala la afya yako, gharama za kujitibu zinaweza kuja kuwa kubwa sana mbeleni na ugonjwa pia utakugharimu muda wako mwingi badala ya kufanya kazi utakuwa unahangaika na matibabu.

Ahsanteni

TUTAENDELEA NA SIRI YA 6 Kwenye Makala Inayofuata

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *