*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*
Uchambuzi by Mary Assenga.
MAZISHI YA WAMANGI.
-Mangi walizikwa mchangani kama watu wengine, lakini kabla ya kuzikwa walitiwa ndani ya chombo cha mti uliochongwa ndani yake wazi kama mzinga wa nyuki mkubwa kama pipa. Kifo cha Mangi hapo zamani kilifichwa sana, pia siku hizo Mangi alikuwa haonekani na watu wote kama aonekanavyo siku hizi. Kazi zake nyingi zilifanywa na nduguye na mawaziri na wachili wa mtaani.
Watu matajiri vile vile walisaidia nchi kwa kila njia wakapewa heshima na wao walikomesha fitina katika nchi wakimtii Mangi wao tu na watu wengine walikubali wakiona wale wakubwa na wazee wa nchi wamejiweka chini ya utawala. Basi walificha habari za kifo cha Mangi kwa muda wa mwaka mmoja watu wasijue, hasa watu wa nchi majirani, kwa sababu jambo kama hili likijulikana mapema ilikuwa pengine maadui walishambulia nchi hii katika msiba wao mkubwa huu na kuuharibu, na nchi itachafuka kabla ya kumtawalisha mtoto mrithi wa Umangi.
Basi kifo chake kilifichwa, watu wakadanganywa kuwa Mangi ni mzima wa afya wakati ng’ombe zikichinjwa na pombe kunyweka sana, watu wajirusha usiku kucha wakisherehekea. Nyimbo za kumsifu Mangi na watu wake ziliimbwa na mambo mengine mengi, hapo Mangi alikwisha kufa kitambo.
-Jambo hili hujulikana tu kwa ndugu mrithi wa Mangi, waziri, mama wa Mangi, watoto na ndugu zake wakubwa na pengine kwa watu wakubwa wa nchi tu. Mambo haya ya kuficha kifo cha Mangi yakiendelea kwa muda basi waziri na ndugu za Mangi huanza kutengeneza habari za kumtawalisha mtoto mrithi wa marehemu; wale watu wakuu wa nchi na wachili wakubwa waliitwa kuapa kwamba watakaa kwa uaminifu na utii chini ya utawala mpya.
Wakimaliza huandaa siku maalum ya kumtawalisha mtoto mrithi wa nchi wa marehemu; wale watu wakuu wa nchi na watu wote wa nchi waliitwa, ng’ombe wengi walichinjwa na pombe nyingi ilitengenezwa. Mambo ya taratibu za kumtawalisha Mangi yalifanywa na watangulizi wa nchi. Watu huambiwa Mangi mzee sasa na hali yake sio nzuri, kwa hiyo mwanawe ametawalishwa aongoze nchi; mwenye akili zake hujua Mangi ameshafariki, lakini wengi huchukua habari hizi kama walivyoambiwa na wazee wakuu wa nchi.
Wakishamaliza hizi taratibu na kuimarisha nchi basi waziri au ndugu mkubwa wa Mangi alitangaza wazi kwamba Mangi mzee alikufa na kuwaambia kwamba wako kwenye msiba mkubwa. Watu walilia na kuhuzunika sana lakini nchi ilikuwa imara kwa sababu watu wakubwa walikuwa wanaelewa siri zote.
ITAENDELEA ….!!
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255 754 584 270.