HADITHI ZA WACHAGGA ZINAZOONYESHA UTHABITI NA UHAKIKA WA MIPANGO YA “RUWA/IRUWA”.


Hapo zamani za kale katika nchi ya wachagga inasemekana kwamba kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mwizi kuzidi watu wote. Siku moja mtu huyu mwizi alienda kwenye nyumba ya watu wengine usiku wa manane kwenda kuiba ulezi. Usiku huo huo mke wa huyo mwenye nyumba aliyoenda kuiba alikua amejifungua mtoto wa kike. Lakini katika nyakati hizo za usiku sana alizoenda kuiba mwizi huyo watu walikuwa wamechoka sana na shughuli hiyo ya uzazi hivyo wote wakawa wamechoka sana na kulala fofofo.


Mwizi yule alipofika alichungulia ndani na kuona kuna mwanga, akaogopa na kujisemea; “Labda wenyewe bado hawajalala.” Lakini alipochungulia ndani ya nyumba aliona kwamba watu wote wamelala. Lakini alipoangalia kwa makini zaidi aliona watu wawili waliokuwa wamevalia mavazi meupe; mmoja amekaa juu ya moto na mwingine chini ya moto huo. Watu hawa wawili walikuwa wanajadili juu ya mtoto aliyezaliwa usiku huo.


Mmojawapo akasema; “Kwa hiyo sasa huyu mtoto atafariki lini?” Mwenzake akamjibu; “Nafikiri ni sawa mtoto huyu atafariki pale atakapokuwa ameweza kuanza kuwafanyia kazi wazazi wake.” Yule mwenzake akamjibu; “Sidhani kama itakuwa ni sawa ikiwa hivyo, kwa sababu akifa wakati huo, atakuwa bado ni mdogo sana na wazazi wake watahuzunika sana kwa kumpoteza binti yao akiwa bado ni mdogo sana. Kwa mimi nafikiri itakuwa vizuri mtoto huyu aishi mpaka kufikia kuolewa, na hata baada ya kuolewa aendelee kuishi na mume wake mpaka atakapozaa watoto wawili, mtoto wa kwanza awe wa kike kama yeye na mtoto wa pili awe wa kiume kama baba yake, ili angalau kila upande upate mtoto mmoja. Baada ya hapo basi acha tu mtoto huyu aliyezaliwa leo afariki na kuacha watoto wawili duniani.” Mwenzake akamjibu; “Ushauri wako huu ni mzuri, sasa turudishe taarifa kwa Ruwa ambaye ametutuma”.


Baada ya kuongea hayo yule mwizi ghafla akashangaa watu hao wametoweka; Hakuwaona tena na hakuelewa hata wameelekea wapi, yaani ghafla tu walipotea. Alishangazwa sana na kile alichokiona na kusikia, lakini ghafla alizinduka kiakili na kugundua kwamba wale ni wajumbe wa Ruwa, ni roho zinazoilinda nyumba ile na wametumwa pale na Ruwa. Kisha mwizi yule akaingia kwenye stoo ya ulezi ya nyumba ile, akajaza ulezi kwenye gunia lake na kwenda zake nyumbani usiku huo. Lakini hakumhadithia mtu yeyote juu ya yale aliyosikia na kuona.


Kisha mwizi yule alikaa kwa miezi mitatu akitafakari yale aliyoyaona na kusikia kisha akajisemea moyoni: “Kama kweli wale waliotumwa walikuwa ni wajumbe wa Ruwa nitawahakikisha kama yale waliyosema juu ya mtoto aliyezaliwa yatakuwa kweli.” Hivyo alienda kunoa kisu mpaka kikawa na makali kabisa. Kisha alienda kwenye nyumba ile kumchungulia mtoto yule na alipokuta kwamba mama yake hayupo, alimchoma yule mtoto kisu cha kifuani kwa nguvu mpaka kikatokea upande wa pili. Baada ya kufanya hivyo alikimbia na kujisemea mwenyewe: “Nimemmaliza, alikuwa amepangiwa kuishi mpaka kufikia kuolewa na kuzaa watoto wawili lakini amefariki”.


Mama wa mtoto aliporudi nyumbani, duh! alikuta kitanda kimetapakaa damu! Akapiga yowe kubwa na watu wengi wakaja. Wakaona jeraha kubwa kwenye mwili wa mtoto. Wakasubiri wakifikiri mtoto huyo atafariki hivi punde lakini hakufariki. Kwa sababu yule mwizi alipomchoma mtoto huyo kisu cha kifuani hakuugusa moyo kwa hivyo mtoto huyo hakufariki. Hivyo mtoto aliendelea kuishi na alihudumiwa na mama yake mpaka alipopona kabisa.


Hivyo mwizi yule hakuendelea kujutia kitendo alichokifanya na badala yake aliamini akajisemea; “kweli watu wale wawili aliowaona wakijadili hatma ya mtoto huyo usiku ule walikuwa wametumwa na Ruwa. Mwizi yule akajisemea kwamba nitapambana mpaka nihakikishe nimemuoa binti huyo ili awe mke wangu, anizalie watoto hao wawili na kisha atafariki. Hivyo atakapofariki ataniachia watoto wawili, mmoja atakuwa wa upande wa mke wangu na mmoja atakuwa wa upande wangu; watakuwa wananitosha.”


Mwizi yule alienda nyumbani kwa wazazi wa binti yule na kuwajulisha kwamba anahitaji kuoa binti yao huyo. Wazazi hao walikataa kwa sababu walifahamu sifa yake mbaya ya wizi. Alijitahidi kuwashawishi sana na kuwahakikishia kwamba amekuwa mtu mwema na yuko tayari kulipa mahari kubwa sana ili kuweza kumuoa binti huyo. Mwisho wazazi wa binti walishawishika na kukubali kwamba binti yao ataolewa naye.
Alimuoa binti yule na kweli walifanikiwa kupata watoto wawili, ambapo wa kwanza alikuwa wa kike na wa pili alikuwa ni wa kiume.

Yule mtoto wa kiume alipokuwa na kufikia kuweza kutembea mama yake alianza kuumwa. Lakini kabla hajafariki watu walimwambia yule mume wake; “Jaribu kwenda kwa daktari, waganga na watabiri waweze kukwambia nini cha kufanya ili kumponya mke wako na ugonjwa wake huu”. Yule mume wake hakuwajibu chochote wala kufanya, aliwapuuza na kuendelea na mambo yake. Kwa sababu alijua kwamba ni Ruwa ndiye anatimiza unabii wa kile kilichosemwa na wale wajumbe wawili kuhusiana na mwanamke huyo wakati amezaliwa.


Mwanamke huyo alifarika na kuzikwa. Kisha Bwana yule aliyekuwa mwizi akawaita wazazi wake ndugu na jamaa zote na kuwalezea kila kitu mpaka kuhusiana na kile kisu. Wote kwa pamoja walishangazwa sana na matendo makuu ya Ruwa na kutazama juu mawinguni na kisha kutema mate mara tatu huku wakilitaja jina la Ruwa na kusema; “Hakuna binadamu anayeweza kuzuia matendo ya Ruwa.”


…………………………………………………………………………………………………………………….


HADITHI NYINGINE YA WACHAGGA JUU YA UKUU WA RUWA/IRUWA.


Hapo zamani za kale katika nchi ya wachagga, alikuwepo Bwana mmoja aliyekuwa mvivu sana. Mke wake alikaribia kujifungua lakini huyu Bwana hakujingaisha juu ya taabu zitakazomkuta mke wake baada ya kujifungua badala yake aliendelea kuwa mvivu na mtu wa kujivuta sana.


Siku ambayo mke wake anajifungua Bwana huyu alichukua shoka na kisu na kuelekea msituni kukata kuni ili zije kusaidia katika kuandaa vyakula. Alipofika msituni katikati aliangalia mbele yake na kuona watu wawili wanaong’aa kama jua. Alipowakaribia alisikia mazungumzo yao, akasikia kwamba walikuwa wanamzungumzia yeye na jinsi alivyokuwa mvivu na wakamzungumzia mke wake pia.


Kisha akasikia mmojawapo akisema; “Sasa huyu mtu mvivu mke wake amejifungua mtoto wa kiume lakini hatakuwa mvivu kama baba yake, atakuwa mwenye uwezo mkubwa na mwenye maarifa mengi. Lakini atakufa katika umri mdogo.” Yule mwingine alimjibu akasema; “Hapana, isiwe hivyo, kwangu naona itakuwa vyema mtoto huyo anapaswa kuishi mpaka aoe na kuwa mtu mzima. N asiku hiyo ya harusi yake ndio siku atakayofariki akiwa anaoa. Kwa sababu baba yake ni mvivu na amekuja leo tu kutafuta kuni huku msituni.” Yule mwenzake akasema; “Ni sawa, acha iwe kama jinsi ulivyosema, sasa twende turudishe taarifa hizi kwa Ruwa.”


Ghafla yule Bwana mvivu akashangaa kuona wametoweka kama vile wamezimika hivi. Alijua kwamba wajumbe hao wametumwa kwake kutokea kwa Ruwa. Alitetemeka sana na kisha kukimbilia nyumbani. Alipofika nyumbani akakuta mke wake amejifungua mtoto wa kiume.


Mtoto yule alikuwa mkubwa na aliweza kuwa hodari sana na mchapakazi ukilinganisha na baba yake aliyekuwa mvivu. Akaendelea kukua akafikia kuwa mtu mzima. Mama yake alitaka mtoto yule wa kiume aoe mke mapema akiwa bado ni mdogo sana kiumri. Lakini baba yake alikataa akasema; “Bado, mtoto wangu hajakusudiwa kuishi na mwanamke.” Baba yake aliendelea kusema hivyo mpaka mdogo wake wa kiume naye alipokuwa mkubwa kiasi cha kuweza kuoa na watu wakamuomba baba yake amuozeshe mtoto.


Hivyo sasa baba yake alikubali kijana wake aoe na siku ya harusi yao kabla sherehe ya harusi haijaishi kijana wake yule mkubwa alifariki hapo hapo wakati harusi ikiendelea. Watu wote walishangazwa sana na tukio hili la ghafla na la kusikitisha na baba yake hapo hapo akamwagiza mdogo wake kuchukua nafasi ya kaka yake aliyefariki. Tukio hili lilitokea kwa namna ambayo hata bibi harusi mwenyewe hakujua kama yule aliyekusudiwa kuolewa naye amaefariki na sasa anaolewa na mdogo wake. Hakujua kwamba mume halisi amefariki.


Baada ya kumzika yule kijana mkubwa aliyefariki baba yao aliitwa watu na wageni waalikwa wa sherehe hiyo. Kisha aliwaolezea hadithi nzima tangu mwanzo mpaka mwishoni, kuhusiana na yote aliyoyaona na kusikia juu ya kijana wake aliyefariki. Na watu wote waliosikia hayo walishangazwa na kupigwa na butwaa. Kisha wote walitazama juu mawinguni na kutema mate mara tatu wakilitaja jina la Ruwa.
Na kuanzia siku hiyo wachagga wamekuwa wakisema; “Siku ambayo mtu anazaliwa maisha yake yote yanakuwa yamepimwa.” Hivyo mtu yeyote anapofariki haikutakiwa kusema amefariki mapema au amechelewa kufariki.


Ahsanteni.
Kesho tutaendelea na nyingine.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *