– Moja kati ya jukumu kubwa sana na muhimu kabisa tulilonalo ni kufundisha historia kwa kizazi kinachokua kisha iendelee kurithishwa kwa vizazi vinavyofuata ili waweze kujua umuhimu wa vitu na watu mbalimbali kadiri ya michango yao kwenye jamii husika. Lakini kwa bahati mbaya sana kwa upande wa wachagga historia ilififia zamani sana ukilinganisha na hapo tulipo sasa, yaani mpaka kizazi cha watu wenye miaka 70 na hata zaidi wana uelewa mdogo sana wa historia kwa sababu historia ilipuuzwa tangu zamani sana.
– Kwa sehemu kubwa nafasi tuliyobaki nayo ni kujifunza historia yetu kutokea kwenye vitabu tukaielewa kwa undani na kuendelea kuirithisha. Lakini hata kama kwetu inaweza kuwa na changamoto kidogo kwa watoto ni rahisi kupandikiza kupitia kufundishwa kwa vitabu na ikaeleweka sana. Inapaswa tujue kwamba hakuna jamii inayoweza kujitambua na kufanya mambo ya maana kama jamii bila kwanza kuelewa historia ya kipindi kisichopungua angalau mika 300 iliyopita ili kuweza kuunganisha matukio kwa usahihi.
– Sio kwamba tu kuna faida nyingi za kujua historia lakini kuna hasara nyingi na uharibifu mkubwa unaotokana na watu kutojua historia yao. Kwanza kuna makosa mengi yanayoweza kurudiwa lakini pia na mbaya zaidi kuna fikra nyingi potofu na zisizo na maana na zaidi zinaweza kuleta uharibifu mkubwa kusambaa na kuaminika kwamba ndio viwango sahihi vya kimaadili na kupekea anguko kubwa. Ni vyema kujua pia kwamba hakuna historia mbaya bali usimuliaji na mtazamo na malengo wa wale wanaoiandika ndio unaweza kuamua iwe mbaya au nzuri na hilo ni kwa kila kitu. Na hilo ndio maana ni muhimu sana historia ya watu kusimuliwa na watu wenyewe na sio watu wa nje au hata majirani tu kwa sababu ya hisia za wivu na chuki zinazoweza kupelekea watu hao wa nje kufanya upotoshaji ili kuharibu taswira ya jamii husika.
– Historia sahihi ya jamii iliyoandikwa na wahusika wenyewe ni muhimu sana katika kuipa jamii husika uhai. Kifo cha jamii yoyote huwa kinaanza na kifo cha historia ya jamii husika. Hakuna jamii inayoelewa historia yake kwa usahihi ikafa, jamii inayotunza na kuenzi historia yake ambayo imetokana na wao wenyewe ni jamii inayoweza kuishi hata miaka 5,000. Hata sisi wenyewe bado hatujachelewa tukiamua kuweka nguvu katika kufundisha historia sahihi sasa na kwa vizazi vijavyo tuna uhakika wa kuiokoa jamii yetu na ikadumu tena kwa maelfu ya miaka mbeleni. Tuna mfano wa jamii kama Wayahudi ambayo historia inawalinda mpaka leo na nchi nyingi mbalimbali zimesimama kwa sababu ya historia zao. China wameweka mpango mkakati wa wanafunzi kujifunza historia za kuanzia hata kabla ya zama za Confucius zaidi ya miaka 2,600 mpaka sasa.
– Uhai wa jamii yetu utatokana na uhai wa historia sahihi inayojenga hamasa kwa vizazi na vizazi na ambayo imesimuliwa kwa namna inayoweza kujenga ufahari na kujiamini zaidi kwa watu wetu.- Binafsi sifahamu ni utaratibu gani ambao huwa unatumika katika kuzipa majina barabara mbalimbali lakini nilipata ukakasi kidogo kujua kwamba barabara inayopandisha Kilema kutokea pale Himo inaitwa barabara ya Nyerere. Lakini ninaamini bila ya shaka yoyote kwamba barabara hii kupewa jina hilo ni matokeo ya wahusika kutojua historia sahihi ya eneo hilo ikachanganyika na propoganda za kisiasa za miaka na miaka za kumtukuza sana huyo aliyepewa jina la barabara hiyo bila kufuatilia kwa undani mchango wake katika eneo husika mpaka kupewa jina la barabara hiyo.
– Historia inatuonyesha Kilema ni himaya ya umangi iliyokuwa mashuhuri sana na iliyokuwa na watawala mashuhuri na waliofanya makubwa katika historia ya wachagga, Kilimanjaro. Tuna mtawala kama Mangi Rongoma ambaye alitawala mwishoni mwa miaka ya 1700 anayetajwa kuwa katika ya watawala wakuu sana katika historia ya Kilimanjaro akitawala eneo lote la Vunjo. Kilema ina mtawala kama Mangi Fumba/Pfumba ambaye aliitawala Kilema kwa miaka mingi sana tangu miaka ya 1870’s mpaka mwaka 1905. Mangi Kilema alijitahidi kutoa ushirikiano kwa wamisionari akisisitiza kwa nguvu zote maendeleo ya Kilema. Yeye ndiye aliwakaribisha wakasaini mpaka mkataba na kuwapa ardhi wamisionari hawa na hata namna walivyoingia mikataba tumeweza kuona kwenye historia.
– Kilema ina watawala kama wakina Mangi Masaki ambaye mwaka 1848 alikuwa mtawala wa kwanza mchagga kumpokea mzungu wa kwanza kuingia Kilimanjaro na kuuona mlima Kilimanjaro Rev. Johannes Rebmann. Kilema ina mtawala kama Mangi Kirita mtoto wa Mangi Fumba/Pfumba ambaye alifanya kazi kubwa sana akisaidiana na wamisionari kuhakikisha shule nyingi zinajengwa Kilema ili kuchochea maendeleo ya eneo la Kilema. Ikumbukwe kwamba katika suala la maendeleo ya maeneo yao wamangi wa Kilimanjaro walikuwa wako kwenye ushindani kabisa. Mangi Kirita mwenyewe aliyeitawala Kilema kwa miaka 20 alipewa heshima hata na kanisa na kuzikwa pale juu ya Mlima Ngangu, Kilema ambako ni eneo takatifu la kanisa.
– Je kutoa jina la barabara muhimu na kuu inayoingia Kilema ambayo ilikuwa ndio lango kuu la kuingia Kilimanjaro katika zama za zamani kwa mtu ambaye hajawahi kuwa na mchango wa moja kwa moja kwa Kilema sio dhihaka na kutafuta dhambi na laana kwa watawala hawa walioleta ukuu na heshima kubwa kwa Kilema?
– Lakini jambo la ajabu zaidi ni kwamba huyo Julius Nyerere aliyepewa heshima hiyo ya kupewa jina la barabara muhimu kabisa ya Kilema historia inamtaja kama mtu aliyeasisi kuhujumu maendeleo ya Kilimanjaro. Dr. Reginald Mengi anaeleza katika kitabu chake cha “I can, I must, I will” jinsi serikali ya Julius Nyerere ilivyoua kwa makusudi vyama vya ushirika ambavyo viliiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi Kilimanjaro bila kujali mchango wa vyama hivyo huku yeye mwenyewe akipata ufadhili kupitia wao kuweza kwenda kusoma Uingereza. Baadaye serikali ya Julius Nyerere iliamua kufuta kabisa vyama hivyo vya ushirika moja kwa moja. Abisai Temba mwenyewe pia anaeleza kupitia kitabu chake cha “300 Years on Kilimanjaro Mountain Area” jinsi serikali ya awamu ya kwanza ilivyoweka sera za kuizuia Kilimanjaro kupiga hatua kimaendeleo kwa kuiweka nyuma kabisa kwa vipaumbele kwa hoja dhaifu kwamba Kilimanjaro inabidi isubiri kwanza kwa sababu imeshaendelea. Na hili lilitekelezwa kuanzia kielimu mpaka katika miradi ya maendeleo. Wazee wengi wasomi walioko vijijini wengine wakiwa wamesoma sana ambao walikuwa wana uelewa mpana wa mambo katika awamu ya kwanza wanadai wazi kwamba serikali ya awamu ya Julius Nyerere ilifanya hujuma ya makusudi kwa maendeleo ya Kilimajaro kwa sababu ya chuki, wivu na roho ya husda juu ya maendeleo ya watu wengine aliyokuwa nayo Julius Nyerere mwenyewe binafsi na sio sera za usawa ambazo alikuwa anazitumia kuficha hoja zake, hoja ambazo hata hivyo bado hazikuwa na mashiko. Hili lilihalisha chuki na hata baadaye matamanio ya waliofuatiwa kuendeleza sera za kuidumaza au kuipuuza Kilimanjaro kwa hoja kwamba kuna maeneo mengine bado hayajaendelea mpaka kufikia kurudi nyuma kabisa.
– Hata Rais Ali Hassan Mwinyi mwenyewe anakiri kupitia kitabu cha cha “Safari Ya Maisha Yangu” kwamba kufuta vyama vya ushirika yalikuwa ni makosa makubwa na yeye aliruhusu virudishwe. Lakini hata hivyo vilirudi kwa sheria za tofauti na katika mazingira tofauti kiasi kwamba havijawahi tena kuwa na nguvu yoyote wala ushawishi wa maana.
– Sasa hayo yote yanafanikiwa kufanyika kwa sababu ya watu kutopenda kujifunza na kujadili mambo mbalimbali lakini mbaya zaidi kutojifunza historia na kuirithisha kwa vizazi vinavyofuata. Hili lingekuwa limefanyika kwa vizazi vya nyuma ni wazi kwamba tungeepuka kuwatukuza watu wasiostahili na kuwapa heshima watu wanaostahili, jambo ambalo linaongeza ari, kujitambua, kujithamini na kujiamini zaidi kwa vizazi vinavyoendelea kuja. Nchi kama China, Israel, Korea hatua kubwa za kimaendeleo wanazopiga zinachangiwa sana na wao kujifunza sana na kuelewa historia yao kwa usahihi kwa sababu kupitia historia wanagundua kwamba wanaweza kufanya mambo mengi sana.
– Kama tutashindwa kupigania kumbukumbu sahihi za watawala wetu tuna nini cha kujivunia na kurithisha kwa vizazi vinavyofuata? Kama Kilema wameshindwa kabisa kupigania watawala muhimu kama Mangi Rongoma, Mangi Masaki, Mangi Fumba/Pfumba, Mangi Kirita, Mangi Wilbald Kirita, watoto wa kichagga wanaokuwa wana nini cha kujivunia? Wanapata wapi ujasiri wa kutembea kifua mbele kwa yale waliyofanikisha wazee wao ili na wao waweke bidii kubwa na kufanya makubwa zaidi?
– Ninaweza kusema tunashukuru angalau wakati wa utawala wa waingereza kuna baadhi ya barabara za Moshi mjini zilipewa majina ya watawala wa eneo hilo. Mangi Rengua Mushi wa Machame alipewa jina la barabara Moshi mjini, Mangi Mamkinga Mushi wa Machame naye alipewa jina la barabara Moshi mjini, Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi naye amepewa jina la barabara Moshi mjini. Kuna eneo pia linaloitwa Kiusa Moshi mjini sina hakika kama eneo hilo limepewa jina hilo kwa heshima ya Mangi Meli ambaye naye aliitwa pia jina hilo.
– Serikali ya waingereza pia walizipa kambi mbili za kupanda mlima Kilimanjaro majina ya watawala wa Uchagga. Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi alipewa jina la kambi ya kwanza ya kupanda mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu ya Mandara hut. Mangi Horombo wa Keni, Rombo akapewa jina la kambi ya pili ya Horombo hut. Na hiyo ilikuwa ni zamani sana karibu zaidi ya miaka 80 iliyopita, na mpaka leo hakuna tena mtu aliyekumbuka kuwaheshimu waliojenga misingi ambayo ushawishi wake unaonekana mpaka kutokea miaka zaidi ya 200 iliyopita.
– Je, sio kwamba kuna namna hata sisi wenyewe tumelala? Hivi isingekuwa ni sahihi zaidi barabara kama hiyo ya Kilema kupewa jina la mtawala kama Rongoma, Masaki, Fumba, Kirita n.k.? Na hiyo ni kwa kesi ya Kilema tu nimezungumzia lakini Kilimanjaro kote historia haijaenziwa kabisa. Angalia kwa mfano lile soko kubwa ya Moshi kwenye eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya uwanja mkubwa wa mpira lilipewa jina la “King George Memorial”, maarufu zaidi kama Maimoria kwa heshima ya Mfalme George wa VI wa Uingereza ambaye ni baba yake Malkia Elizabeth II aliyeko sasa mpaka leo bado limebaki vile vile. Huo sio ukoloni? Si ingekuwa ni busara zaidi soko lile likaitwa pengi Mangi Sina Memorial kwa sababu liko kwenye ukanda wa chini wa eneo la Kibosho? na mengine kama hayo. Au hata mtawala mwingine aliyewahi kufanya makubwa kwa ajili ya Kibosho? au hata mtawala mwingine yeyote wa kichagga.
– Na hata sasa usishangae kusikia huko Mkuu, Rombo wameanzisha maktaba ya kijamii ya Mkuu, na badala ya kuiita Selengia Kinabo Community library ili kuwajengea watoto wa eneo hilo self esteem na shauku ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu Selengia Kinabo utakuta wameiita J. K. Nyerere Community Library licha ya kutokuwepo kwa kitu kingine chochote hata benchi tu lililopewa jina la “Selengia Kinabo”. Na hiyo ipo kwa Kilimanjaro yote. Sina hakika hata kama Mangi Mkuu wa wachagga ana ukumbusho wowote mkubwa wa taasisi ya kijamii kwa sababu hata kuna shule Moshi mjini ilipewa jina obvious sana J.K. Nyerere wakati ni jina common kila kona ya nchi. Sio kwamba tunahitaji kujitofautisha na kuonyesha kwamba tunajielewa na kuelewa zaidi kuhusu sisi wenyewe na upekee wetu katikati ya propaganda na hadaa nyingi za kisiasa?
– Tutawajengea vipi kujiamini watoto wetu wanaokuwa ukijaribu kulinganisha na watoto wa China, Japan, Israel, Korea, Italy wanaofundishwa historia za mashujaa wao tangu miaka 3,000 iliyopita walitokana na kizazi chao. Tumefanikiwa kuandika historia ya miaka 700 ya wachagga inayoonyesha kumbukumbu za maisha na utawala vinavyokwenda na vizazi mpaka karibia miaka 500 iliyopita ambayo itatoka hivi karibuni, ni muhimu sana tukaanza kuhakikisha basi watoto wetu hawapotea. Watoto wetu hata wanawapa watoto wao majina ya mashujaa wanaotokana na babu zao badala ya kubebwa na kila aina ya taarifa na propaganda inayokatiza kwenye tv na mitandao.
Nini maoni yako?
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com