UISLAMU UCHAGGANI.

– Kupitia historia tunafahamu kwamba wachagga wa kwanza kuoandoka kwenye dini asili ya wachagga na kujiunga na dini za kigeni ilikuwa ni katika muongo wa mwisho wa karne ya 19. Hii ilikuwa ni mwaka 1892 wamisionari wa misheni ya kianglikana ya CMS ilipowabatiza wachagga wawili katika kijiji cha Mdawi, Old Moshi mwezi Julai 1892 kwa majina “Tomasi Kitimbo Ringo” na “Yohana Nene Tenga” baada ya kuwepo Uchaggani kwa kipindi cha miaka 7 tangu wameanzisha misheni hiyo Kitimbirihu, Old Moshi bila kufanikiwa kubatiza mchagga yeyote kuwa mkristo. Kabla ya hapo hakuna mchagga yeyote alikuwa amewahi kujiunga na dini yoyote ya kigeni.

– Hata hivyo hii sio kumaanisha kwamba wachagga walikuwa hawashawishi kujiunga na dini za kigeni. Hili lilikuwa linatokea mara nyingi sana. Mmisionari wa kwanza kuingia Uchaggani, Kilimanjaro ilikuwa ni mwezi Mei mwaka 1848 mmisionari mjerumani wa misheni ya CMS ya London, Uingereza alifika Uchaggani na kwa mara ya kwanza kabisa alifika Kilema na kuonana na Mangi Masaki wa Kilema wakati huo. Johannes Rebmann ambaye alikuwa na lengo pia la kutangaza injili ya Yesu Kristo aliondoka Kilema na kwenda moja kwa moja mpaka Machame na kuonana na Mangi Mamkinga ambaye alijaribu kumhubiria injili ya Yesu Kristo mwanzoni mwa mwaka 1849 bila mafanikio yoyote. Sio tu kwamba Johannes Rebmann mwaka 1849 alishindwa kumhubiria injili ya Yesu Kristo Mangi Mamkinga wa Machame bali yeye mwenyewe alilazimishwa kushiriki ibada ya kichagga ya tambiko takatifu lililomhusu yeye mwenyewe kinyume na matakwa yake.

– Bahati mbaya zaidi kwa Johannes Rebmann ni kwamba alifika Uchaggani miaka mingi kabla ya utawala wa wakoloni wa kizungu kuingia hivyo hakuweza kuwa na mamlaka yoyote inayomuunga mkono na kumsaidia katika lengo lake kama ilivyokuja kutokea kwa wamisionari waliofika mwishoni kwa karne ya 19. Hata hivyo sio tu Johannes Rebmann bali pia mmisionari mwingine muingereza kutoka katika kanisa ya United Methodist Church la London, Uingereza Rev. Charles New alijaribu kuhubiri injili ya Yesu Kristo Uchaggani mwanzoni mwa miaka ya 1870’s bila mafanikio.

– Charles New alipewa eneo la Kitimbirihu katika kijiji cha Mdawi, Old Moshi na Mangi Rindi Mandara kwa ajili ya kuanzisha shule ili wachagga wasome lugha na teknolojia. Charles New alijenga shule hapo Kitimbirihu, Old Moshi mwaka 1872 pengine na kituo kidogo cha misheni lakini alikatazwa kueneza dini ya kikristo na kuruhusiwa kuanzisha shule pekee. Lakini mwisho aliishia kushambulia na majeshi ya Mangi Rindi Mandara akaporwa mali zake na kufukuzwa kabisa Kilimanjaro. Charles New aliondoka na kuelekea Pwani ya Mombasa lakini hata hivyo alifariki njiani kabla ya kufika Mombasa.

– Baadaye mwaka 1878 Mangi Rindi Mandara aliwaandikia tena barua wamisionari wa CMS kutokea London, Uingereza kuja kuanzisha shule Uchaggani huku yeye mwenyewe akiahidi kuongoza wachagga kusoma katika shule hiyo. Ilichukua muda mrefu kidogo mpaka mwaka 1885 ndipo wamisionari wa CMS waliitikia wito wa Mangi Rindi Mandara na kuja kuanzisha kituo cha misheni katika eneo lile lile la Kitimbirihu alipoanzisha shule mmisionari Charles New mwaka 1872. Wamisionari wa CMS walianzisha shule ya boarding na hospitali lakini hawakuruhusiwa kusambaza injili kwa wachagga kwani Mangi Rindi Mandara aliamini kwamba wachagga wana dini zao na desturi zao ambazo bora na zinazowafaa. Mangi Rindi Mandara aliwasisitiza kwamba anahitaji shule kwa ajili ya kufundisha lugha na teknolojia za kutengeneza samani(furnitures) wanazonunua Ulaya pamoja na silaha zikiwemo canons(mizinga ya moto). Hivyo wamisionari hawa walichunguzwa na kuzuiwa kabisa kubatiza wachagga na kuwageuza wakristo.

– Hivyo japo waliweza kufundisha mambo mengi ikiwemo kusoma na kuandika na hata hadithi za kwenye biblia na namna ya kusali lakini wamisionari hawa walishindwa kubatiza mchagga yeyote mpaka wakati anafariki Mangi Rindi Mandara mwaka 1891. Mwaka 1892 ndipo wachagga wawili wa mwanzoni walibatizwa na kuwa watu wachagga wa kwanza kabisa kuondoka kwenye dini ya asili na kujiunga na dini za kigeni. Baadaye walikuja wamisionari wa kilutheri walioelekea Machame na kuendelea kubatiza wachagga wengi na hata wamisionari wa kanisa katoliki walioanzia Kilema na kuanza kubatiza wachagga. Japo wamisionari wa kanisa katoliki walipata shida sana mwanzoni Kibosho kutokana na kukataliwa na Mangi Sina kuingiza dini Kibosho lakini kwa msaada wa serikali ya wajerumani walikuja kufanikiwa na kuanza kubatiza watu. Hata hivyo kwa Kibosho hali ilikuwa ni ngumu sana kwani hata baada ya miaka zaidi ya 50 baadaye takriban nusu ya wachagga Kibosho walikuwa wamegoma kubatizwa na kujiunga na ukristo.

– Sasa kwa upande wa uislamu dini hii ilichelewa kidogo kuingia Uchaggani na pengine hiyo ndio sababu ilishindwa kusambaa na kukubalika na wengi kwani ilikuta ukristo umeshaota mizizi kiasi cha kupambana kuuzuia uislamu usisambae. Hii haimaanishi kwamba waislamu hawakujaribu kujipenyeza kusambaza dini ya kiislamu Uchaggani tangu mwanzoni. Waislamu walifanya majaribio mengi ya kueneza dini ya kiislamu tangu mapema sana kabla hata ya ukristo katika pwani ya Afrika mashariki na hata bara. Bila kutumia nguvu kubwa sana waislamu walifanikiwa sana kusambaza dini ya kiislamu katika ukanda wa pwani na hata ndani zaidi kwani hata mpaka maeneo ya Lushoto, Usambara watawala walikwa wamekubali kupokea uislamu na hata kujenga misikiti.

– Lakini Uchaggani uislamu ulikataliwa kabisa na watawala wenye nguvu kwani walikuwa wanafahamu namna ulivyofanya kazi katika maeneo ya pwani na hawakulifurahia jambo hilo. Kwa mfano Mangi Rindi Mandara alikuwa akipokea misafara mikubwa ya kibiashara kutokea pwani ilikuwa inaongozwa na waswahili na waarabu ambao walikuwa ni waislamu kindakindaki ambao walijaribu kumshawishi kubadili dini bila mafanikio. Kama alivyotueleza Alexander Le Roy katika kitabu cha “Missiona To Kilimanjaro” historia pia inatuambia kwamba Mangi Rindi Mandara mwenyewe ndiye alikuwa anawahuburia waislamu hao juu ya ukuu wa tamaduni na dini ya wachagga na kuzuia mchagga yeyote kujiunga na uislamu. Hii ni licha ya kwamba Mangi Rindi Mandara alikuwa na mabalozi waislamu kutoka Zanzibar katika Ikulu yake wakimwakilisha Sultan wa Zanzibar na yeye akiwa na mabalozi Zanzibar pia kwa Sultan.

– Mangi Sina wa Kibosho pia alikuwa akipokea wageni wengi kutokea Mombasa na Pangani waliotembelea Uchaggani lakini hawakufanikiwa kuwashawishi wachagga kuondoka kwenye dini yao ya asili na kujiungana uislamu. Hivyo ukristo kwa msaada pia wa kimamlaka kutoka kwa serikali ya wakoloni walifanikiwa kuingiza dini ya kikristo kiurahisi zaidi na kutokana na kuwa waliwahi na kupata kuungwa mkono na serikali iliyokuwa inatawala Uchaggani waliweza kudhibiti na kuzuia uislamu ambao walikuwa wamechelewa na pia hawakuwa na mamlaka za kuwapigania kufanikisha lengo lao.

– Hata hivyo uislamu ulikuwa umeingia Moshi mjini tangu mwaka 1899 ambapo msikiti wa Riadha ulikuwa msikiti wa mwanzoni kujenga. Lakini uislamu huu wa Moshi kwa mwanzoni haukuwa ni kwa ajili ya wachagga bali wahindi waliokuwa wameletwa na wazungu sambamba na waswahili waliokuwa wanakuja Moshi kwa kuletwa na wakoloni au sababu nyingine za kibiashara. Hivyo uislamu wa Moshi mjini ambao ulitambulika na kuwa na mahusiano kutokea pwani kiasi cha kutumiwa hata viongozi wa kidini wa kuswalisha waislamu wa Moshi ndio ulikuwa uislamu pekee Kilimanjaro.

– Uislamu ulianza kuingia Uchaggani na hususan eneo la Machame katika miaka ya 1930’s. Anaandika Mohamed Said kwenye kitabu ambacho anajaribu kumuelezea mtu aliyeitwa Rajabu Ibrahimu Kirama au Kirama Muro kutoka kwenye ukoo wa Nkya wa kijiji cha Nkuu, Machame kama jemedari wa uislamu Uchaggani. Mohamed Said ushawishi wa dini ya kiislamu Uchaggani huenda ulianzishwa na wasomali ambao walikuwa na kituo maeneo ya ukanda wa chini kidogo ya Uchaggani karibu na Bomang’ombe maarufu kama kwa wasomali waliokuwa wameanzisha kituo kwa ajili ya kufanya biashara ya kahawa.

– Mohamed Said ambaye anaeleza historia ya uislamu Uchaggani na hususan Machame ilianza baada ya mtu aliyeitwa Shariff Muhsin kutokea Mombasa alipomtembelea rafiki yake aliyeitwa Sheikh Mussa Minjanga ambaye alikuwa ni Liwali na Imam wa msikiti wa Riyadha msikiti wa kwanza Moshi mjini. Shariff Muhsin kutokea Mombasa aliyemtembelea Sheikh Minjanga alijaribu kuhubiria watu kuhusu uislamu Moshi mjini ili kuwasilimisha na baadaye akaamua kuelekea Machame akiamini ataweza kufanikiwa kusambaza uislamu licha ya kwamba wakati kanisa lilikuwa tayari limeimarika sana Uchaggani na hususan Machame kwenyewe.

– Shariff Muhsin alifika kwanza katika kituo cha wasomali ambapo alikuta pia kulikuwa tayari na msikiti mdogo uliojengwa kwa fito. Kama alivyokuwa anaamini kwamba atakutana na wenyeji hawa ambao watampa ushirikiano na kufanikisha lengo lako hilo. Anasema waliingia Machame na kukutana na wenyeji akiwemo mtu huyu aliyeitwa Kirama Muro wa kijiji cha Nkuu, Machame ambaye Shariff Muhsin alifanikiwa kumsilimisha yeye na watu wengine kadhaa. Kirama Muro baada ya kusilimu alichagua jina la Rajabu na wengine waliosilimu pamoja naye ni Amin Natai, Abdillah Mwasha, Omari Sengere, Said Mwinyi na Omar Abdillah.

– Mwanahistoria wa uislamu Mohamed Said anaeleza kwamba huyu Kirama Muro kutoka katika kijiji cha Nkuu, Machame anatokea kwenye familia mashuhuri kisiasa na kiutawala katika historia ya wachagga Kilimanjaro. Hii ni kwa sababu babu yake Mboyo Sisya ndiye alikuwa mkuu wa majeshi ya Mangi Rengua wa Machame aliyetawala nusu ya Kilimanjaro. Pia familia ilikuwa inatoa majemedari hodari wa majeshi ya Machame na hivyo ilikuwa ni kati ya familia mashuhuri na zilizokuwa tajiri pia katika historia. Kirama Muro mwenyewe ambaye alibadili jina na kuitwa Rajabu alikuwa ni mtu mashuhuri kwenye jeshi la Mangi Ngulelo wa Machame wakati tayari utawala wa wajerumani umeingia Kilimanjaro 1901 – 1917. Kirama Muro mwenyewe alidai kwamba baba yake Muro Mboyo ambaye aliishi uhamishoni Old Moshi kwa muda mrefu sana baadaye kabla ya kufariki kwake alirudi Machame na kusilimu na kuchagua jina Ibrahim hivyo yeye mwenyewe alijiita Rajabu Ibrahimu Kirama.

– Kirama Muro au Rajabu Ibrahim Kirama alikuwa ni mtu wa mwanzoni kabisa Machame kama sio wa kwanza kabisa Machame kuingia kwenye uislamu katika miaka ya 1930’s. Baada ya kuingia kwenye uislamu Rajabu Ibrahimu Kirama aliazimia kujenga msikiti katika eneo lake katika kijiji cha Nkuu, Machame. Inasemekana kutokana na kutofautiana kisiasa na utawala wa Mangi baba yake Rajabu Ibrahim Kirama aliyeitwa Muro Mboyo alikimbilia uhamishoni Old Moshi. Baada ya baba yake Rajabu Ibrahim Kirama aliyeitwa Muro Mboyo kuondoka Machame na kukimbilia uhamishoni Old Moshi na kwenda kuoa kabisa huko Old Moshi, mama yake Rajabu Ibrahimu Kirama mchagga kutoka Kibosho aliyeitwa Makshani Olotu aliamua kurudi kwao Kibosho akiwa pamoja na watoto wake ambao walikuwa ni wadogo. Hivyo Rajabu Ibrahimu Kirama aliishi sana Kibosho pia wakati wa utoto wake.

– Hata hivyo wakati Rajabu Ibrahimu Kirama anapanga kujenga msikiti katika kijiji cha Nkuu, Machame Mangi Abdiel Shangali alikuwa ameapa hataruhusu kabisa uislamu kuingia Machame. Mangi Abdiel Shangali ambaye alikuwa ni mkristo alikuwa ameanza kuona dalili za majaribio ya uislamu kuingia Machame na hivyo alikuwa ameapa kupambana nao kwa nguvu zote. Hivyo Rajabu Ibrahimu Kirama alivyopeleka barua ya maombi kwa Mangi kwa ajili ya kujenga msikiti Machame aliishia kuzungushwa na kuyumbishwa bila pasipo kupewa ruhusa ya kujenga msikiti Machame.

– Kwa kuwa Rajabu Ibrahimu Kirama naye alitokea kwenye familia yenye umashuhuri katika historia alijaribu kupambana na Mangi Abdieli Shangali katika kufanikisha lengo lake la kujenga msikiti Machame katika kijiji chake cha Nkuu. Mangi Abdieli Shangali ajaribu kusambaza propaganda za onyo kwa Rajabu Ibrahimu Kirama na wafuasi wake kwamba msikiti wowote utakaojengwa Machame utabomolewa. Katika kuendelea kumtishia Rajabu Ibrahimu Kirama Mangi Abdieli Shangali alimkamata Rajabu Ibrahimu Kirama bila kosa lolote akampakia kwenye gari yake na kwenda kumtupa jela ambapo alikaa kwa siku mbili kabla hajatolewa. Hata hivyo bado hilo alikumzuia Rajabu Ibrahimu Kirama kuendelea kupambana katika harakati zake za kujenga msikiti.

– Rajabu Ibrahimu Kirama alienda kwenye ngazi za juu zaidi katika serikali na kuonekana ana haki hiyo ya kujenga msikiti katika eneo ambalo ni mali yake mwenyewe aliyorithishwa na mzazi wake. Lakini Mangi Abdieli Shangali aliendelea kusisitiza kwamba wachagga anaowaongoza yeye hawataki msikiti ujengwe Uchaggani na yeye kwa kuwa anawasikiliza wale wengi anaowaongoza hawezi kuruhusu msikiti kujengwa katika eneo lake la utawala. Inasemekana kwamba inawezekana kuna misikiti mingine ilishatangulia kujengwa Machame katika maeneo ya Kalali, Mudio, Uswaa lakini ilibomolewa yote kwa amri ya Mangi Abdieli Shangali.

– Rajabu Ibrahimu Kirama baada ya kupata kibali cha kujenga msikiti alishirikiana na wafuasi wake na wanafamilia kujenga msikiti lakini ulipokamilika walitumwa watu wenye silaha kwenda kuubomoa. Walipofika waliwakuta waislamu hao wakiwa katika eneo hilo katika kijiji cha Nkuu na kuwajulishwa kwamba walikuwa wamekuja kubomoa huo msikiti lakini kwa kuwa wamewakuta wenyewe basi wanawapa siku mbili wawe wameubomoa wenyewe. Haikuchukua muda mrefu Rajabu Ibrahimu Kirama alitupwa tena jela kwa kipindi cha mwezi mmoja bila kosa lolote wala kusomewa.

– Zilizuka propaganda kwamba watu wote wanaomuunga mkono Mzee Rajabu Ibrahimu Kirama watahamishwa Machame, kitu ambacho kilikuwa ni tishio kubwa sana kwa Uchaggani. Hata hivyo Mzee Rajabu Ibrahim Kirama hakukata tamaa kabisa katika harakati na wafuasi wake katika mapambano dhidi ya kueneza uislamu. Baadhi ya waislamu wengine waliotaka kujenga misikiti walinyang’anywa maeneo yao na wengine kufungwa jela huku wakitangaziwa kuwa chanzo cha kuvuruga utulivu. Pamoja na kutaabishwa kote huku waislamu hawakurudi nyuma bali waliendelea kupambana na kusonga mbele kuhakikisha wanasimamia haki zao sawa na dini nyingine ya kikristo.

– Juhudi za kuzuia uislamu kuenea Machame zilishindikana na kwa umoja wao waislamu waliweza kuongezeka na kutanuka zaidi wakajenga misikiti zaidi Machame katika vijiji vingine zaidi tofauti na Nkuu katika maeneo ya Lyamungo, Kalali, Uswaa, Mudio n.k., Waislamu walijenga shule zao Machame ili kuweza kuwapatia elimu watoto na vijana wa kiislamu kama walivyokuwa wanafanya wakristo kwani waliogopa watoto wao wanaweza kubaguliwa kwenye shule za seminari. Hata hivyo waislamu walihangaika sana mpaka shule za kiislamu kuweza kupata ruzuku ya serikali kwani ilichukua miaka mingi mpaka wao kuweza kukubaliwa maombi yao na serikali.

– Waislamu walijaribu kuueneza uislamu Kibosho na maeneo mengine ya Uchaggani kutokea Machame. Kwa Kibosho walikuwa wameshapata wafuasi wengi na ambao walikuwa na umoja lakini misikiti yote iliyojaribu kujengwa Kibosho ilibomolewa kwa amri ya Mangi Ngilisho wa Kibosho. Mangi Ngilisho alipiga marufuku kabisa msikiti kujengwa Kibosho na alionya kwamba msikiti wowote utakaoonekana Kibosho utabomolewa. Katika maeneo mengine ya Uchagga wamangi wengi waligoma kuruhusu kabisa waislamu kueneza injili na kujenga misikiti japo hata hivyo waislamu walijitahidi kujenga angalau msikiti mmoja kwa baadhi maeneo kama vile Kibosho na Uru.

– Mzee Rajabu Ibrahimu Kirama alifariki mwaka 1962 na anahesabika na waislamu wa Uchaggani kama shujaa aliyesimama imara kupigania na kuisimamisha uislamu Uchaggani na hususan katika eneo la Machame.

– Katika kijiji cha Samanga, Marangu kwenye ngome ya ukoo wa Mongi pia uislamu ulienea na kuimarika katika eneo hilo, japo hakuna taarifa za uhakika kama unahusiana na harakati hizi zilizoanzia Machame na kuingia kwa kiasi kidogo sana katika maeneo mengine.

Karibu kwa Maswali au Maoni.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *