UKOO WA MWASHA

– Ukoo wa Mwasha ni ukoo maarufu na mkongwe sana uchaggani hususan katika upande wa magharibi ya Kilimanjaro. Wachagga wa ukoo wa Mwasha ambao wanapatikana kwa wingi zaidi katika kijiji cha Mudio, Masama au Machame ya magharibi kwa ujumla ni watu makini na wenye kujituma sana katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi wanakopatikana.

– Kutoka kwenye historia wachagga wa ukoo wa Mwasha kama zilivyo koo nyingi za upande wa magharibi pengine mwanzoni wakitokea katika eneo la Sienyi walikuwa na makazi ya mwanzoni katika kijiji cha Shari/Uraa, Machame kilichopo katikati ya mto Marire na mto Kikafu. Mzee wa mwanzoni zaidi anayekumbukwa na historia aliyekuwa kiongozi wa ukoo wa Mwasha alijulikana kwa jina la Masare na aliishi katika kijiji cha Shari/Uraa, Machame huko katika karne ya 16 au 17.

– Hata hivyo, mwishoni mwa karne ya 18 au mwanzoni mwa karne ya 19 wakati wa utawala wa Mangi Rengua au Mangi Kiwaria Machame, tawi kubwa la ukoo wa Mwasha likiongozwa na Mzee kiongozi wa ukoo huu aliyejulikana kwa jina la Sukilo walihamisha makazi ya ukoo wa Mwasha kutokea katika kijiji cha Shari/Uraa, Machame wakavuka mto Marire na kuelekea upande wa magharibi wakishuka chini kidogo na kuweka makazi ya kudumu katika kijiji cha Mudio, Masama au Machame ya magharibi ambapo ni takriban miaka zaidi ya 200 mpaka sasa. Huku wengine wa ukoo wa Mwasha wakibaki katika kijiji cha Saawe, Masama kilichopo Ng’ambo ya pili ya kijiji cha Shari/Uraa, Machame ukivuka mto Marire.

– Kwa utafiti wa kihistoria mpaka katikati ya karne ya 20 Mzee wa tawi la ukoo wa Mwasha katika kijiji cha Mudio, Masama anayekumbukwa na historia wa mwisho alijulikana kwa jina Isai. Ukoo wa Mwasha umeendelea kutanuka zaidi upande wa magharibi na mashariki ya Machame na kwenda mpaka magharibi ya mbali.

– Wachagga wa ukoo wa Mwasha wanapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Mudio, Masama au Machame ya magharibi.

– Ukoo wa Mwasha wanapatikana kwa wingi kiasi katika kijiji cha Saawe, Masama.

– Ukoo wa Mwasha wanapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Nkwansira, Masama.

– Ukoo wa Mwasha wanapatikana kwa kiasi pia magharibi ya mbali katika kijiji cha Ng’uni, Masama.

– Ukoo wa Mwasha wanapatikana kwa kiasi pia katika kijiji cha Shari/Uraa au Kyeeri, Machame.

– Tunaendelea kuhimiza michango ya kila mtu juu ya chochote unachoweza kufahamu kuhusu ukoo huu wa Mwasha ndani na nje ya Kilimanjaro. Karibu kwa mchango wa mawazo.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mwasha?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Mwasha?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mwasha?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Mwasha una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani? Wewe ni Mwasha wa kutokea kijiji gani?

5. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Mwasha kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

6. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mwasha?

7. Wanawake wa ukoo wa Mwasha huitwaje?

8. Una rafiki yako yeyote wa ukoo wa Mwasha?

9. Watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Mwasha?

Karibu kwa Maoni na Maswali.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *