UKOO WA MBORO NA UTATA JUU YAKE.

Ukoo wa Mboro ni kati ya koo kubwa, kongwe na mashuhuri sana katika historia ya wachagga Kilimanjaro.

Ukoo wa Mboro ulikuwa ni ukoo mashuhuri tangu miaka ya 1600. Ukoo wa Mboro ulikuwa ndio ukoo mashuhuri na wenye nguvu zaidi Marangu mpaka kufikia karne ya 17 baadaye wakahamishia ngome yao katika kijiji cha Sembeti kutokea Lyamrakana.

Ukoo wa Mboro ulikuwa ndio ukoo wenye nguvu na wenye ushawishi mkubwa zaidi katika eneo la Masama au Machame Magharibi mpaka katikati ya karne ya 20. Ni ukoo mashuhuri na wenye nguvu uliotawala eneo la Masama kwa karne nyingi zilizopita ambapo kiini chao kwa sasa Masama ni katika kijiji cha Mbweera, Masama kati. Machame ukoo wa Mboro uliweza kumhifadhi na kumlinda Mangi ilipotokea hali ya hatari.

Ukoo wa Mboro ni ukoo unaopatikana karibu kila mahali Uchaggani, Kilimanjaro kuanzia magharibi mpaka mashariki. Huu ni ukoo ambao kwa sehemu kubwa ulikuwa unatoa watu imara sana na mashuhuri katika historia ya wachagga, Kilimanjaro. Ulitoa watu wapambanaji na walioheshimika. Huko Kirua Vunjo ukoo wa Mboro ndio uliokuwa unaongoza masuala ya tohara na uliheshimika mpaka na watawala(wamangi) na kupewa nafasi ya kipekee.

Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu cha “Africa’s Dome of Mystery”, Eva Stuart Watt, Mboro maana yake ya moja kwa moja ya kichagga ni “mzinga mkubwa wa asali” ambapo tafsiri hii ilimaanisha kama mtu jasiri mwenye muonekano thabiti na mwenye kuheshimika sana. Hizi zote ni tafsiri zenye dalili kwamba ukoo huu wa Mboro ulihusishwa na ushujaa, umashuhuri na heshima ya kipekee.

Hata hivyo kwa bahati mbaya, baada ya lugha ya kiswahili kuendelea kupata nguvu na baadaye kusambaa na kisha watu kuhimiza na kufananisha tafsiri tofauti ya jina la ukoo huu na kiungo nyeti cha mwili taharuki ilianza kutokea ndani ya ukoo wa Mboro. Watu wa ukoo wa Mboro wakaanza kujihisi aibu au fedheha kuitwa kwa jina hilo na hata baadaye ulianza kutokea ubaguzi katika taasisi mbalimbali kwa watu wenye jina la ukoo wa Mboro.

Taharuki hiyo iliathiri sana ukoo wa Mboro na hata kuudhoofisha na hivyo kupelekea kufifisha utambulisho wake. Watu wengi wa ukoo wa Mboro walianza kuukana ukoo wao na wengi kuanza kuanzisha majina mengine yanayokaribiana kufanana na ukoo huu na mengine yaliyo tofauti kabisa. Watu wengine pia wa ukoo wa Mboro wakaamua kuhama ukoo na kujiunga kwenye koo nyingine kabisa.

Hizi zote zikiwa ni juhudi za kuondokana na jina lao la asili ili kujenga utambulisho mpya ambao hawauonea aibu pamoja na kukubalika kwenye taasisi ambazo zilionekana kuwabagua. Japo hata hivyo bado kuna ambao wamebaki katika ukoo huu asili na wanajivunia kujiita kwa jina lao hilo hilo la asili hususan Kibosho. Huku kuna wengine mpaka leo bado wanajisikia aibu kuitwa kwa jina lao asili la ukoo.

Ukoo wa Mboro kama sio kukutana na changamoto hiyo ulikuwa ni ukoo mkubwa kama ilivyo kwa Massawe, Tarimo, Kimaro au Swai n.k. na zaidi ulikuwa ni ukoo wa watu mashuhuri sana. Lakini nafikiri badala ya ukoo huu kusambaratika na kutokea matawi madogo madogo yanayoathiri utambulisho wao na hata kupoteza historia yake ni bora wangekutana wote na kufanya maamuzi ya pamoja.

Aidha wangebadili herufi moja ya jina la ukoo wao au wanabaki na msimamo wa jina hilo na watu wawazoee hivyo na kuacha kubadilisha maana na kuipeleka kwenye tafsiri nyingine. Kwa sababu kuna majina mengi ya aina hiyo yenye tafsiri tata lakini msimamo kwenye matumizi yake umepelekea majina hayo kuzoeleka na kukubalika na kisha kufuta ile dhana tata iliyotaka kujengeka mwanzoni.

Hata hivyo watu wengi wa ukoo huu hawapendi sana utani juu ya jina hilo kwa sababu ya tafsiri potofu iliyotengenezwa, hivyo nitangulize samahani kwa yeyote atakayekwazika kwa mjadala huu. Ni mjadala unaolenga kujenga zaidi na hauna lengo la kukejeli, kufanya utani au kutweza utu wa mtu yeyote kwa namna yoyote ile.

Baadhi ya majina ambayo ukoo wa Mboro umeyarithi kutokea kwenye jina asili.

1. Machame magharibi/Masama Mboro wanatumia Ndosi.

2. Machame ya Mashariki wanatumia Muro, lakini inasemekana hata ukoo Mbowe wa Nshara na Narumu, Machame pia ni Mboro. Huko Kimbushi, Machame ukoo wa Mboro wanaitwa Mbonika.

3. Kibosho ukoo wa Mboro wanatumia Mboya na wengine Kilawila na Kimathi.

4. Uru ukoo wa Mboro wanatumia Kimathi na wengine Sangawe.

5. Mbokomu haijulikanai Mboro wamepotelea wapi.

6. Old Moshi ukoo wa Mboro inasemekana kuna waliojiunga kwenye ukoo wa Ringo japo kuna tawi lingine linatumia Makirita.

7. Kirua Vunjo haijulikani ukoo wa Mboro wapotelea wapi.

8. Marangu Mboro walihamishia ngome yao katika kijiji cha Sembeti na eneo takatifu katika kitongoji cha Kirefure baada ya kuondoshwa Lyamrakana, lakini nao wamepotea sana. Hata hivyo kuna wengine wanatumia Maleko eneo hilo.

9. Kwa upande wa Mamba ukoo wa Maleko pia unahusishwa na ukoo huu wa Mboro.

Ulikuwa ni ukoo wenye utajiri mkubwa sana pia zamani.

Je kuna majina gani mengine ambayo matawi ya ukoo huu mashuhuri na uliokuwa maarufu na mkubwa sana umeyachukua?

Vipi kwa maeneo mengine ya Kilimanjaro ukoo wa Mboro unatumika kwa wingi kiasi gani au wamehamia kwenye jina gani?

Karibu kwa Maoni, Maswali na Ushauri.

You may also like...

Popular Posts

12 Comments

  1. Ahsante sana kwa historia nzuri ya ukoo huu wa Mboro. Kweli umetafiti mno. Hongera.

    Kimachame, ni kweli ukoo huu ni wa zamani sana kama zilivyo koo zingine mfano, Massawe, Kimaro, na Shoo. Ni vigumu kujua hasa asili yao ingawa wameonekana kushabihiana sana na koo hizo zingine nilizozitaja hapo. Labda hii inaonyesha kuwa asili zao zilifanana.

    Historia ya Machame imegawanyika kufuatia mto Kikafu, wa upande wa mashariki na magharibi (na wazee walipotumia jiografia hiyo walimaanisha zaidi kwa mpaka wa mto Kikafu). Magharibi ya mto Kikafu kwa asili iliitwa Sinde (yaani, uwanda wa chini), na wamashariki ya mto ilijulikana kama uwanda wa juu, kutokana na kuwa kilimani. Jina Machame lilikuja kuitwa hivyo baada ya muda wa mgawanyiko huo.

    Kutokana na vita vya Ndesserua wa Machame, kule Sinde ukoo wa Mboro ulikaribia kupotea, wengi wakiwa wameuawa na wachache waliobaki walikimbia makazi yao (ndiyo asili ya jina Masama, yaani, kuliko hamwa). Kuepuka utambulisho wenye shida kisiasa, walibadili majina yao na ama kujiita kwa kutumia majina ya wazazi, mfano, Ndosi, Makere, na Muro.

    Hata hivyo, mashariki mwa Kikafu wameendelea kutumia jina la Mboro mpaka miaka ya karibuni ya karne ya 20 ambapo wengine walibadili kutokana na sababu ulizozitaja hapo juu na kutumia majina kama vile Mbonika.

    Ukoo wa Mboya wa Kibosho asili yao ni wamasai (kama walivyo wakibosho wengine). Hata hivyo, Kabla ya kukimbilia Kibosho, waliishi Masama na kukaribishwa na ukoo wa Mboro kule, na hivyo kuchukua jina lao. Wakati wa vita vya Mangi Ndesserua kule Masama, ambavyo wakazi walitawanyika, waliokimbilia Mashariki zaidi (Kibosho) walibadili jina lao na kuitwa Mboya. Hawa hata hivyo walikuwa ni wachache sana.

    Wengine wenye asili hiyo ambao waliishi Masama, walioitwa Tarimo, baadhi yao walikimbilia Mashati Rombo, wakaanzisha utawala wao kule Mashati ambao hata hivyo walishindana kwa muda na ukoo wa Shirima Lyimo ambao kutokana na kuwa na nguvu waliwashinda na kuwa chini ya utawala wa ukoo wa Shirima wa Mashati.

  2. Nna utata mmoja swai n ya rombo au ni machame

  3. Ukoo wa sariko ni kibosho sehemu gani

    1. Sariko ni tawi, ukoo mkuu ni upi?

  4. Naomba kuuliza anaefahamu ukoo wa Masimba na historia yoyote tafaadhali naomba anijulishe.
    0763194643
    Nickson

    1. Masimba ni mkataba gani?

  5. Nafurahia historia ya wachaga na koo mbalimbali. Kuna huu ukoo qa lema, kuna nchi mbalimbali na hasa europ ikiwepo uingereza,Italy ukraine pia ukienda afrika maqharibi hili jina hasa kwenye biashara linatumika sana pia mahoteli makubwa hapa itakuaje. Nimeona maeneo mengi ya ulaya.

    1. Yeah! Nafikiri itakuwa ni ufanano wa majina

  6. Naomba kuuliza kiongozi wa ukoo wa laswai aliitwa nani?

    1. Huo bado haijajulikana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *