– Nyaki ni ukoo mkongwe sana wa wachagga unaopatikana katika maeneo ya baadhi ya vijiji vya magharibi ya karibu na mashariki ya kati ya Uchagga, Kilimanjaro. Wachagga wa ukoo wa Nyaki wakiwa wamesambaa na wanapatikana maeneo mbalimbali ndani na nje ya Uchagga, Kilimanjaro ni watu wanaofanya vizuri katika fani mbalimbali ikiwemo taaluma na ujasiriamali, huku wengine wakiwa kwenye mashirika na taasisi mbalimbali ndani ya nchi na kimataifa.
– Kutoka kwenye historia ukoo wa Nyaki unafahamika kwamba kwa Uchaggani, Kilimanjaro una chimbuko lake katika kijiji cha Kyala, Marangu. Zamani sana takriban miaka 400 iliyopita katika eneo la Marangu kulikuwa na koo mbalimbali zinaishi kila ukoo na kijiji chake. Katika kijiji cha Mshiri kulikuwa na ukoo wa Mtui, kijiji cha Samanga ukoo wa Mongi na kijiji cha Lyamrakana na Sembeti kulikuwa na koo za Mboro, Kinyagha na Tillya n.k.,.
– Wakati huo ukoo wa Lyimo walikuwa na wanaishi katika eneo ambalo sasa hivi ni ndani ya msitu wa mlima Kilimanjaro linalojulikana kama Fuphu Lya Komkuu na maeneo ya vilima vya Kifinika. Haya ni maeneo ambayo kwa sasa yake ndani ya msitu wa mlima Kilimanjaro ukipandisha kupitia njia ya Marangu ni kupanda mlima ni baada ya kituo cha watalii cha Mandara hut. Baadaye ukoo wa Lyimo waliteremka na huku chini na kupigana vita na Makishingo na majeshi yake ni kwa ushirika kutoka koo nyingine za Mwika, Kirua Vunjo na Old Moshi walifanikiwa kushinda na kujiimarisha katika maeneo ya vijiji vya Arisi na Lyasomboro.
– Wakati huo upande wa magharibi katika kijiji cha Kyala yalikuwa ni makazi ya wachagga wa ukoo wa Nyaki. Wachagga wa ukoo wa Nyaki japo walikuwa ni matajiri wakubwa wa mifugo lakini walikuwa ni watu watulivu na wasiopenda mivutano hivyo walipoona ukoo wa Lyimo wameshinda vita na kuweka makazi katika vijiji jirani upande wao wa magharibi walikwenda kufanya mapatano ya amani bila masharti yoyote kwa kufunga undugu wa kuchanjia damu, “bond of blood brotherhood” yaliyokuwa mila maarufu kwa wachagga.
– Lakini haikuchukua muda ukoo wa Lyimo waliokuwa upande wa mashariki kidogo katika maeneo ya vijiji vya Arisi na Lyasomboro waligundua kwamba ukoo wa Nyaki wana utajiri mkubwa hivyo tamaa ikawaingia wakajilaumu kwa nini walikubali kuunga undugu na Nyaki bila masharti yoyote wakati ilikuwa ni fursa ya kunufaika na utajiri huo mkubwa. Hata hivyo ukoo wa Lyimo walipata wazo ambalo walilipeleka kwa ukoo wa Nyaki kwamba ili kuimarisha undugu wao basi wabadilishane mabinti wadogo ambao kila mmoja atatoka kila upande na kwenda kufanya majukumu kwa mwenzake na kurudi mara kwa mara, wazo ambalo lilipitishwa na wote kuridhika.
– Haikuchukua muda mrefu yule binti kutoka kwa Lyimo aliuawa akiwa migombani huko Kyala kwenye ukoo wa Nyaki kwa njama zilizopangwa na watu wa ukoo wa Lyimo wakati binti wa kwa Nyaki akiwa salama kabisa huku kwa Lyimo. Baada ya binti wa kwa Lyimo kutorudi nyumbani watu wa kwa Lyimo walikwenda kumuulizia na kumdai kwa Nyaki na alipokosekana alitafutwa na kukutwa ameuawa na kutupwa shambani kule kule Kyala kwa Nyaki. Hii iligeuka kuwa ni kesi kubwa iliyowakabili ukoo wa Nyaki ambao walilazimika kuamini kwamba binti yule ameuawa na watu wao.
– Ukoo wa Nyaki walikubaliana kuwapa ukoo wa Lyimo kiasi cha utajiri wao na kuanzia siku hiyo ukoo wa Nyaki walikaa chini ya utawala wa ukoo wa Lyimo. Hili liliwaongezea nguvu ukoo wa Lyimo ambao waliendelea kupambana na kutawala maeneo mengine zaidi ya Marangu.
– Ukoo wa Nyaki kutokea katika kijiji cha Kyala, Marangu baada ya hapo licha ya kupungua kwa umashuhuri wao lakini waliendelea kuongezeka na kusambaa zaidi katika maeneo hayo vijiji vya mashariki ya kati ya Uchagga, Kilimanjaro na wengine kuelekea magharibi.
– Hivyo ukoo wa Nyaki unapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Mrawi, Uru.
– Ukoo wa Nyaki unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Nganjoni, Kirua Vunjo.
– Ukoo wa Nyaki unapatikana katika kijiji cha Leghomulo, Kilema.
– Ukoo wa Nyaki unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Lyamrakana, Marangu.
– Ukoo wa Nyaki unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Lyasomboro, Marangu.
– Ukoo wa Nyaki unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Kyala, Marangu.
Karibu kwa mchango zaidi wa Mawazo kuhusu ukoo wa Nyaki.
1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Nyaki?
2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Nyaki?
3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Nyaki?
4. Kama wewe ni wa ukoo wa Nyaki una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu?
5. Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?
6. Wewe ni Nyaki wa kutokea kijiji gani?
7. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Nyaki kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?
8. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Nyaki?
9. Wanawake wa ukoo wa Nyaki huitwaje, na kwa nini?
10. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Nyaki?
11. Ni watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Nyaki?
12. Kuna mnyama yeyote ambaye labda ni mwiko kuliwa na wachagga wa ukoo wa Nyaki?
13. Kuna ukoo ambao hawaruhusiwi kuoana na Wako-Nyaki kwa sababu zilizowahi kuwepo miaka ya zamani au nyingine zozote?
Karibu kwa Mchango zaidi au maswali.
Ahsanteni.
Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.
Urithi Wetu Wachagga (Facebook).
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255 754 584 270.