MTAZAMO NDIPO NGUVU YETU ILIPO.

Miaka imeendelea kwenda na mambo yameendelea kubadilika sana na kwa kasi kubwa, mabadiliko haya yanakwenda kwa kasi sana na yanapelekea mabadiliko pia ya mienendo na tamaduni zetu siku baada ya siku. Mabadiliko haya yamekuwa na matokeo chanya na hasi kwa namna ambazo tunaweza kuyatafsiri kadiri tunavyozitambua thamani kwa mitazamo na imani tulizojengewa.

Tukija kwa upande wa tamaduni zetu sisi wachagga mabadiliko kwa sehemu kubwa yamekuwa na matokeo hasi zaidi kwa sababu yanadhoofisha na kuelekea kuondoa tamaduni hizo bila kujali ni chanya au ni hasi. Lakini kwa kuwa wote tunakubaliana kwamba kila jamii ina tamaduni zenye athari chanya na hasi, basi wote tunakubaliana pia kwamba tuna jukumu la kuzitunza zile zenye athari chanya na kuachilia zile zenye athari hasi.

Changamoto tuliyonayo ni kwamba mwenendo uliopo sasa unapuuza na kudhoofisha zote, zenye athari chanya na zenye athari hasi na mbaya zaidi ni kwamba watu aidha kwa ujinga wao au kwa makusudi wanatumia zile hasi kuhukumu na kuharamisha tamaduni zote kwa ujumla, zenye athari chanya na hasi. Na hapa ndipo tunapokutana na mzizi wa tatizo ulipo, unaotumika kama silaha ya kudhoofisha na kuua kila kitu chetu chema bila kujali faida na umuhimu wake kwetu. Na silaha hiyo inayotumika kuhakikisha inaangamiza kila kitu chetu bila kujali kama kina athari chanya au hasi ni MTAZAMO.

MTAZAMO ndio mzizi wa tatizo, na mtu anapoelewa undani na athari za MTAZAMO basi anaweza kuepuka ufuataji mkubwa sana wa mkumbo ambao hutumika sana na watu mbalimbali wenye nia na malengo mbalimbali katika kuhadaa watu kwa manufaa yao tofauti tofauti.

Pengine kabla hatujaenda mbali sana kwanza tukumbushane tafsiri sahihi ya MTAZAMO. MTAZAMO kama jinsi inavyojulikana pia kwa kiingereza “ATTITUDE”, ni zile fikra ambazo mtu anakuwa nazo kichwani juu ya kitu chochote kinachoweza kuingia kwenye fikra za mtu. Yaani yale mawazo yanayokuja kichwani mara moja pale kitu chochote kinapotajwa, kinaweza kuwa ni kitu, mtu, jamii, taasisi, falsafa fulani, nchi fulani, dini fulani, mnyama fulani yaani chochote kile. Sasa MTAZAMO umegawanyika katika makundi makubwa mawili ambayo ni MTAZAMO CHANYA na MTAZAMO HASI.

MTAZAMO CHANYA ni pale mtu anapokuwa na hisia nzuri au hisia za upendeleo juu ya kitu fulani na MTAZAMO HASI ni pale mtu anapokuwa na hisia mbaya au hisia za kuchukia na kukataa kitu fulani.

Sasa tuangalie ni nini kinachopelekea MTAZAMO wa mtu kuwa chanya au hasi juu ya jambo lolote? MTAZAMO wa mtu kuwa chanya au hasi juu ya jambo lolote lile inatokana na zile hadithi ambazo mtu amekuwa akielezwa au kuzisikia juu ya jambo hilo. Hadithi zozote zile ambazo mtu yeyote anapewa hasa na watu wake wa karibu au watu anaowaamini au kuwaheshimu, iwe ni za kweli au sio za kweli ndizo hujenga uelekeo wa MTAZAMO wa mtu aidha kuelekea upande chanya au upande hasi.

Hadithi hizi zinavyoendelea kurudiwa rudiwa kwenye akili au fikra za mtu kwa muda mrefu hukomaa na kuwa ndio ukweli na uhalisia wa imani ya mtu katika jambo husika ambapo hufikia mahali na kugeuka kuwa sehemu ya hisia zake kabisa. MTAZAMO unapofikia kuwa sehemu ya hisia basi mtu huyo akisikia jambo hilo limetajwa tu anapata hisia chanya au hasi ndani yake na anaweza hata kuzionyesha wazi wazi kwa lugha ya mwili wake. Japo ni kwa baadhi ya vitu alivyovisikisa sana lakini mtu anaweza kuonyesha uso wa huzuni au furaha, hofu au ujasiri, tabasamu au hasira n.k.,. mara tu baada ya kusikia au kuona kitu ambacho tayari ana mtazamo fulani juu yake. MTAZAMO huathiri hata hukumu nyingi ambazo watu hutoa juu ya vitu mbalimbali.

Hata leo ukifuatilia mitazamo mingi uliyonayo kwenye fikra zako utakuta imetokana na hadithi ulizokuwa ukiambiwa juu ya watu au vitu husika tangu ukiwa mdogo na kwa sehemu kubwa ndivyo unavyotumia kuhukumu pia. Kwa sababu watu wachache wajanja wanafahamu nguvu ya MTAZAMO wamekuwa wakiitumia kuhakikisha wanaijenga kwa namna yenye manufaa kwao au kuharibu mambo ya wengine kwa namna mbalimbali. Hiyo ndio kwa sababu unaweza kukuta watu wanafanya mambo yanayowaumiza hata wao wenyewe moja kwa moja kwa sababu tu wamejengewa mitazamo ya namna hiyo kwa muda mrefu.

Maeneo yanayoongoza kwa kutumia propaganda katika kuathiri mitazamo mbalimbali ya watu kwa manufaa fulani ya mtu au watu ni kwenye siasa, dini na mambo ya kijamii. Hivyo kwa sehemu kubwa hisia ulizonazo juu ya mambo fulani ambayo mara nyingi jamii nzima inashiriki hisia hizo hazipo kwa bahati mbaya tu bali imetumika miaka mingi kuzijenga na kuwa ndio tamaduni za wakati husika.

Hata sasa kuna mjadala tukiamua kuunzisha hapa juu ya mtu fulani au itikadi fulani ya kidini, kisiasa, kijamii au nyingine yoyote tunaweza kubishana hata wiki nzima juu ya uhalali wake kimaadili kwa sababu tu ya utofauti wa KIMTAZAMO ambao umetokana na hadithi ambazo tumekuwa tukipewa tangu zamani kabisa juu ya mtu au itikadi hiyo. Hiyo haimaanishi kwamba kitu hicho ni cha kweli au kina uhalali wa kimaadili bali tu kitu hicho kimekuwa kikipewa hadithi nzuri tangu zamani na hadithi hiyo imeendelea kuingia ndani ya fikra za watu na kuzama kabisa ndani yake ni kuwa ndio uhalisia wa mtu husika.

MTAZAMO umeingia kwa kina sana ndani ya fikra za mtu mpaka umekuwa ni sehemu ya hisia zake juu ya mtu huyo kiasi kwamba pale utakapotaja au kuongelea mtu au kitu hicho basi mtu husika anaweza hata kutaharuki kutegemea namna ulivyokizungumzia na kiasi kilivyoingia ndani ya fikra zake. Hili linaweza kuwa hata moja ya sababu ya kwa nini unakutana pia na picha za wanasiasa wenye mamlaka katika maeneo rasmi ya kitaasisi.

Mpaka hapo tunaweza kuona sasa kwamba hata MITAZAMO yetu juu ya jamii yetu wenyewe ya wachagga haipo vile ilivyo kwa bahati mbaya bali kuna juhudi nyingi za makusudi na nyingine za bahati mbaya zilizofanyika kuifikisha hapa ilipo. Vile tunawaza juu ya sisi wenyewe nah atua yoyote tunayotaka kupiga inachangiwa sana na fikra ambazo zimejengwa kuhukumu chochote tunachotaka kufanya.

Wewe fikiria umefika mahali ukajitambulisha kuwa ni nani na unatokea wapi, unadhani wale watu ni nini kinakuja mara moja kichwani kwako, na unafikiri MTAZAMO huo una athari gani kwa chochote unachokwenda kufanya? Hapo sasa ndipo unapoweza kuona umuhimu wa kujenga upya MITAZAMO sahihi ya watu juu ya jambo lolote kabla ya kuanza kufanya kitu kingine chochote. Mitazamo sahihi inapojengwa inabadili fikra, kuondoa hofu, woga na wasiwasi juu ya mambo fulani na kukuza sana ile hali ya kujiamini binafsi(self-esteem) kwa wahusika kitu ambacho ni muhimu sana katika kufanikisha jambo lolote kubwa au la maana kwenye maisha.

MTAZAMO CHANYA juu ya mambo una athari kubwa katika kukusaidia kuyafanikisha kwa sababu unayafanya kwa kujiamini na kuyafurahia hivyo unaweka nguvu zako zote na bidii yako yote katika mambo hayo na matokeo yake yanakuwa ni makubwa na ya uhakika. Kwenye kitabu kilichoandikwa na Rabbi Daniel Lapin, kinachoitwa “Thou Shalt Prosper”(Ten Commandments of Making Money) akizungumzia namna utamaduni wa kiyahudi ulivyopelekea mafanikio makubwa ya kiuchumi wa wayahudi kwa utamaduni huo kuwa na sehemu kubwa ya MITAZAMO CHANYA juu ya wao wenyewe na juu ya fedha na utajiri, katika sura ya “Believe in the dignity and morality of business” amezungumzia kwa kina sana dhana hii ya MTAZAMO CHANYA na MTAZAMO HASI inavyoweza kurudhisha nyuma juhudi za kufanikisha jambo lolote. Hivyo suala la kuwa na MTAZAMO CHANYA na sahihi juu ya jambo husika katika kufanikisha jambo lolote ni kigezo muhimu sana kwa mafanikio ya jambo hilo.

Hivyo sasa zinahitajika juhudi nyingine kubwa na za makusudi za kuboresha na kuimarisha MITAZAMO yetu wenyewe juu ya yetu wenyewe na mambo yetu. Kazi hii sio kazi rahisi na wala sio kazi ya siku moja au mbili, lakini habari njema ni kwamba mpaka kufikia sasa tumeona kwamba kwa kiasi kuna mwelekeo na fikra za watu zimeendelea kuwa chanya baada ya kuendelea kutanua uelewa wa mambo mengi yanayoihusu jamii yetu.

Lakini hata hivyo ukweli ni kwamba bado kuna kazi kubwa sana iko mbele yetu na kazi hiyo haiwezi kabisa kufanikiwa bila ushirikiano wa dhati na wa karibu sana wa kila mtu mwenye kutamani kuendelea kuona mabadiliko ya kijamii. Ushirikiano huo unahitaji ujasiri mkubwa hata wa kuvunja baadhi ya kanuni na mazoea yanayoaminika na wengi lakini yasiyo na uzito sana ili kuweza kufanikisha, na ikiwa tutaingiza woga, wasiwasi na hofu ambazo hazina mashiko yoyote hatutaweza kupiga hatua yoyote kubwa. Hatua kubwa zinahitaji ujasiri mkubwa lakini ambao ni salama, hakuna jambo lolote la maana lililowahi kufanikiwa bila kuhusisha ujasiri wa hali ya juu na kuvunja baadhi ya kanuni na mazoea yasiyo na mashiko.

Habari njema ni kwamba tayari tumeanza kupata wadau ambao wana zaidi ya utayari wa kuunga mkono harakati hizi na kufanya zoezi lenyewe kupungua ugumu wake lakini bado kazi sio ndogo. Kinachokwenda kufanyika kwa sasa ni kujenga MTAZAMO CHANYA kwa kutumia njia hizo hizo wanazotumia wengine na zenye mafanikio makubwa, kujenga fikra za MSHIKAMANO katika kuelekea kuimarisha upya utamaduni uliosaidia kujenga jamii iliyokuwa inaheshimika sana zamani ambayo kwa sasa imekuwa ya mashaka.

Zile tu fikra za MTAZAMO CHANYA juu yetu wenyewe na MSHIKAMANO imara peke yake, ambavyo ndio agenda ya sasa ni hatua kubwa sana ambayo inaweza kuja na mambo makubwa zaidi kama matokeo yake. Hivyo tunahitaji ushirikiano wako wa hali ya juu na kupitia ushirikiano huo tunaamini tutafanikisha kwa hakika yale tunayolenga.

Karibu kwa Maswali, Maboresho au Mawazo mbadala.

Whatsapp/Call +255 717 452 790

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *