WACHAGGA WA KIZAZI KIPI WAPO SAHIHI NA WAPI WAMEKOSEA/WALIKOSEA?

– Tunafahamu kwamba miaka ya zamani hususan mpaka kufikia miaka ya 1980’s ilikuwa ni nadra sana kwa jamii ya wachagga kuoana au kuzaa na watu wa jamii nyingine. Sina uhakika kama kuliwahi kuwa na sera iliyowekwa juu ya jambo hilo labda wakati wa utawala wa Mangi Mkuu au hapo kabla lakini ilikuwa mchagga akifikia kuoa hata kama anaishi mbali sana na Kilimanjaro alirudi kupata mke Uchaggani au mchagga aliyekutana naye huko ugenini na kuoa.

– Suala lilizingatiwa na wachagga wa ngazi zote kuanzia wafanyabiashara, wasomi, wajasiriamali, watu wenye mafanikio makubwa na hata wale waliokuwa na mafanikio ya kawaida. Hili ni suala lililozingatiwa kwa umuhimu wa hali ya juu. Japo lilizingatiwa viwango vya juu zaidi na wanaume lakini hata wanawake zamani walilipa uzito mkubwa sana tofauti na hali iliyopo sasa.

– Hata hivyo kwa sasa sera hii ya kwamba mchagga lazima arudi kuoa au kuolewa Uchaggani inaonekana sio tu kwamba imekufa kabisa bali inaonekana haipo kabisa katika vipaumbele vya mchagga anayetafuta kuwa na mwenza wa maisha. Hili limekuwa ni jambo la kushangaza kidogo kutokana na kwamba lilikuwa na nguvu kubwa sana miaka michache iliyopita lakini ghafla moja msukumo huo umepotea kabisa kiasi kwamba inaleta maswali, je ni kitu gani kilifanya jambo hili lipewe uzito zamani na sasa uzito huo umeondoka kabisa. Nini kilichokuwa kinaweka uzito huo kwa miaka ya zamani.

– Yaani ukifuatilia sehemu kubwa ya watu wenye umri wa kuanzia miaka 55 kuendelea utagundua kwamba karibu wote walikuwa wanaoana zaidi wachagga kwa wachagga, lakini ukirudi kwa vijana wenye umri wa miaka 35 kurudi chini utagundua huo utaratibu umekufa kabisa. Hii ni kwa sababu hata wale ambao wanajikuta wameoana wachagga inakuwa tu imetokea kama bahati kwa sababu labda wanafahamiana kwa kusoma pamoja au kutokea maeneo ya karibu, lakini sio kwamba walikuwa wanaendelea kusimamia ile sera walioisimamia wazazi wao miaka iliyopita.

– Utamaduni ule au sera ile imepoteza kabisa msukumo kiasi kwamba suala hilo halipo kabisa kwenye kipaumbele hususan kwa wanawake. Hii inajionyesha pale ambapo hata kama mtu machaguo mawili ya wachumba wanaofanana kwa kila kitu bado utakuta haangalii kwamba yule wa nyumbani labda ndio atampa uzito zaidi badala yake wote wanakuwa sawa kabisa.

– Ukweli ni kwamba mjadala wa suala hili kwa miaka ya sasa unahusisha hisia kali huku watu wakiwa wamegawanyika na kila akijaribu kutetea mtazamo wake. Wengine wanaamini waliotangulia walikuwa sahihi kutochanganyika sana na jamii nyingine huku wengine wakiamini kwamba kuchanganyika ni muhimu na kuna faida zake. Hata hivyo wahafidhina wengi hawapendi sana suala hili la kuchanganyika na kila mtu wakati maliberali wakiwa wanaamini hakuna haja ya kuendelea kushikilia chochote bali kuchanganyika ndio sera bora zaidi.

– Jamii nyingi duniani ambazo zinalenga kulinda tamaduni zao na wengine hata utajiri wao na vipaji vyao vya asili wanaonekana kuwa wakali zaidi katika suala hili na wanashikilia sera za kihafidhina katika suala hili japo hawaweki wazi moja kwa moja kwa watu wa nje ya jamii yao. Japo hata hivyo ndani ya jamii hizo wapo wenye mitazamo tofauti na wasioamini katika kulinda misingi ya jamii hizo.

– Kwa upande wetu wachagga kuna baadhi ambao wanazungumzia suala hilo kwa kuamini kwamba kuchanganyika kumeua zile tamaduni muhimu na maadili na kusababisha matatizo makubwa zaidi katika mahusiano na ndoa kuliko zamani. Kwa mfano Bwana mdau mmoja anaitwa Isaac Temba anasema wanawake wengi wa kichagga waliozaa watoto na hawana ndoa(single mothers) kwa sehemu kubwa sana wamezaa na wanaume wasio wachagga, Bwana Isaac amefika mbali zaidi na kusema kwa utafiti wake ndoa za mchanganyiko zinavunjika zaidi kuliko zile za wachagga kwa wachagga kwa sababu ya utofauti mkubwa wa kimtazamo na utamaduni.

– Mdau mwingine kwa jina la Felix Swai anasema ile asili, ari na zile thamani zilizowekewa misingi na wazee zinapotea na kuacha jamii ambayo haijui asili wala misingi yake kutoka na mchanganyiko. Kutokujua huko asili wala misingi yake ndio kunapelekea wa tu kuvamia na kuthamini tamaduni za wengine kama wazungu, wasia na wahindi na kudharau kabisa za kwao kwa sababu hazipewi nafasi ya kuenziwa. Kwa sababu wenzetu kama vile wahindi wametunza za kwao basi kuna wachagga wamefikia mahali wanajiita hata majina ya kihindi kwa kutothamini na wakati mwingine kuchukia kabisa za kwao.

– Felix Swai anaenda mbali zaidi na kusema ukilinganisha na jamii nyingine, wanaume wanaofanya vizuri zaidi katika ndoa ni wanaume wa kichagga na ndio waliosaidia kujenga familia imara sana za kichagga kwa vizazi vilivyopita, hivyo sera ya kuoana zaidi wachagga itasaidia kuimarisha ndoa na familia nyingi za wachagga kuliko kinyume chake ukilnganisha na hali ilivyo sasa.

– Lakini hata hivyo wako watu wengine wanaamini kwamba kuchanganyika ni kuzuri kwani kunatoa fursa ya kupata vizazi vinavyorithi tabia na vipaji vingine ambavyo haviko kwa jamii ya wachagga sambamba na kutoa nafasi ya kupata mwenza sahihi zaidi kwa sababu mtu anakuwana uwanja mkubwa wa kuchagua. Hili suala la kupata mwenza bora zaidi kwa kuwa na uwanja mkubwa wa kuchagua linaonekana kutetewa zaidi na wanawake ambao wao ndio wanaonekana kutojali kabisa kuhusu sera. Hata hivyo ni sera ambayo ilihitaji ushirikiano wa pande zote mbili za kiume na kike kuifanikisha.

Karibu kwa Maoni, Ushauri, Maswali au Ufafanuzi zaidi.

– Je, una mtazamo gani juu ya wachagga kuachana na sera au utamaduni wa kuoana zaidi wenyewe kwa wenyewe na sasa wanaonekana kutoweka kabisa kipaumbele katika hilo, hususan wanawake?

– Je, unafikiri kuna umuhimu au kulikuwa na umuhimu wowote katika kuzingatia sera hiyo?

– Unafikiri ni nini kimeharibika au ni nini kimekuwa faida iliyotokana na kupuuzwa kwa sera hiyo?

– Unaamini propaganda za kisiasa na kijamii zimechangia kuua ile ari ya wachagga katika sera hiyo? Kama jibu ni ndio ni kwa namna gani?

– Unaamini jamii mbalimbali za dunia hii zinazojitahidi kujilinda dhidi ya mchanganyiko mkubwa na jamii nyingine kuna manufaa makubwa wanayopata?

– Unafikri kuna haja ya wachagga kurudi kusambaza propaganda za kuturudisha kuweka kipaumbele zaidi kwenye kuoana wenyewe zaidi kama ilivyokuwa zamani au kuacha mambo yaende kama yanavyokwenda?

– Je, una maoni yako mengine binafsi ya tofauti?

Karibu kwa mjadala huru bila kufungwa na upande wowote.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *