MTI ALIONYONGEWA MANGI MELI MANDARA NA WENZAKE.

GOLGOTA.

Mti huu uliopo katika kijiji cha Tsudunyi, Old Moshi katika wilaya ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro ndio kama Golgota kwa Wachagga kwani ndio mti walionyongwa watawala wa Uchaggani, Kilimanjaro siku ya tarehe 2/Januari/1900.

Wakiongozwa na Mangi Meli Mandara wa Old Moshi, Mangi Molelia Mushi wa Kibosho na Mangi Ngalami wa Siha/Sanya Juu walikutwa na hatia za kupanga njama za kuanzisha vita nyingine ya nne dhidi ya wajerumani wakijaribu kushirikisha watawala wa Meru na Arusha ili kuwaondoa wajerumani moja kwa moja Kilimanjaro.

Mpango huu ulipojulikana walifikishwa mahakamani na kukutwa na hatia na kunyongwa mpaka kufa ambapo kichwa cha Mangi Meli Mandara kilikatwa na kupelekwa Ujerumani na hakijaweza kurudishwa mpaka leo. Hata hivyo juhudi za kurudishwa kwa fuvu la kichwa cha Mangi Meli Mandara bado linaendelea kwa ushirikiano wa familia na taasisi inayohusika huko Ujerumani.

Mti huu upo hata leo katika kijiji cha Tsudunyi, Old Moshi karibu na zilipokuwa ofisi za wajerumani zamani kabla ya mji kuhamishiwa katika eneo la mjini ya sasa. Mti huu pia upo karibu na ilipokuwa shule ya Sekondari Old Moshi zamani kabla ya shule hiyo kuhamishiwa Moshi mjini na majengo hayo kuchukuliwa na shule nyingine iliyokuja kuitwa Shule ya Sekondari Kolila hapo baadaye.

Mti huu pia upo karibu kabisa na mahakama ya mwanzo Old Moshi upande wa pili wa barabara umbali wa kama kilomita 4 kutokea Kiboriloni katika eneo ambapo barabara hii ya Old Moshi inapokutana na barabara kubwa ya Arusha – Moshi – Himo na Dar es Salaam.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

2 Comments

  1. Jerome Joseph Kiwia says:

    Nimefurahi sana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *